Uhuru wa Mtu kuamini Dini atakayo

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Uhuru wa Mawazo. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Uhuru wa Mtu kuamini Dini atakayo

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anayo Haki ya Uhuru wa  kuamini dini atakayo. Ibara ya 19 (1) ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake’

Taifa letu limebahatika kuwa na watu wa aina tofauti tangu kuundwa kwake. Watu hao wanaotoka maeneo tofauti, makabila na hata imani tofauti. Kwa kipindi chote hiki tumeishi kwa pamoja kwa amani na kuheshimiana pasipo kujali tofauti za dini zetu. Uhuru huu wa mawazo na imani upo kwa wote na Katiba inamruhusu mtu hata kubadili imani yake ya kidini kama anaona inafaa kwa wakati huo.

Aidha Katiba inabainisha jinsi uhuru huu unavyoweza kutekelezwa na wananchi wote pasipo kuathiri mahusiano baina ya wananchi na Mamlaka za Nchi au wananchi wenyewe.

Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiyari la mtu binafsi na shughuli za uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi. Hii ni kwa mujibu wa Ibara 19 (2) ya Katiba.

Kwamba serikali haitahusika kwa namna yoyote na shughuli za utangazaji dini na kueneza dini. Kama tunavyofahamu kuwa serikali haina dini yoyote ingawa watu au wananchi au viongozi wana dini zao.

Katika kuhakikisha masuala ya imani na dini yanalinda ustawi wa taifa, umoja na amani yetu taratibu za kisheria zimewekwa kuhakikisha haki hii inalindwa pasipo kuingiliwa na mtu yeyote au kuharibu mahusiano baina ya dini au madhehebu yaliyopo nchini.

Hitimisho

Hivi karibuni kumeibuka kwa wingi madhehebu na dini mbali mbali katika taifa, ni jambo jema watu kumtafuta Mungu katika maisha yao. Hata hivyo ni muhimu kwetu kuzingatia misingi ya taifa letu kuheshimu kila mtu na mwenzake ingawa tofauti za kidini zipo. Tanzania ni sehemu pekee ambayo unaweza kuona ndoa au ndugu wa familia moja wakiwa na imani tofauti na wakiishi kwa furaha na amani kwa kushirikiana. Ni vyema viongozi wa dini na waumini kusaidia umoja na kuvumiliana na kuhakikisha hakuna mmoja anatumia dini yake kukebehi au kukashifu dini ya mwengine.

 ‘Uhuru wa imani ni haki yako, tumia imani yako kwa manufaa na kuunganisha jamii na si kuitenganisha’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili