13. Migomo

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tuliweza kuangalia kuhusu Majadiliano ya Pamoja ambapo chama cha wafanyakazi kinaweza kuwa wakala wa wafanyakazi kujadiliana na mwajiri kwa lengo la kuboresha mahusiano na maslahi ya pande zote. Katika makala ya leo tunakwenda kuangalia juu ya Migomo. Karibu tujifunze.

Maana ya Mgomo

Mgomo ni hali ya kusimamisha kazi inayofanywa na wafanyakazi kwa lengo la kumlazimisha mwajiri wao au mwingine au jumuiya ya waajiri ambayo mwajiri wao ni mwanachama, kukubali madai ya wafanyakazi, au mwajiri kubadili au kuacha madai yake dhidi ya wafanyakazi.

Mgomo ni haki ya kila mfanyakazi. Haki hii ya mgomo hatahivyo inahusiana na mgogoro wa maslahi pekee na si vinginevyo. Katika aina za migogoro ya kiajira ipo mgogoro wa maslahi na lalamiko. Kama aina ya mgogoro ni suala la lalamiko wafanyakazi hawaruhusiwi kugoma bali kufuata tararibu wa uwasilishaji wa lalamiko mbele ya Tume au Mahakama ya Kazi kwa usuluhishi na uamuzi.

Wafanyakazi wasioruhusiwa kugoma

Kiujumla haki ya kugoma ni ya kila mfanyakazi, hata hivyo Sheria ya Kazi imeondoa baadhi ya kada za ajira katika kutumia haki hii kutokana na umuhimu wa sekta zao katika uendeshaji wa maisha ya kila siku.

  • Wafanyakazi katika huduma muhimu. Huduma hizo ni kama maji na usafi, umeme, huduma za afya, huduma za zimamoto, udhibiti wa safari za angina mawasiliano ya ndege na huduma nyingine za usafirishaji
  • Wafanyakazi ambao wanapaswa kuendelea na kazi wakati wa mgomo kwa makubaliano ya pamoja ya utoaji huduma kwa kiwango cha chini
  • Wafanyakazi wanaobanwa na makubaliano ya kupeleka mgogoro huo kwenye uamuzi
  • Wafanyakazi wanaobanwa na makubaliano ya pamoja au Tuzo ya mwamuzi inayosimamia suala la mgogoro
  • Mahakimu, Waendesha Mashtaka au watumishi wengine wa mahakama
  • Wafanyakazi wanaobanwa na Tangazo la Kima cha Chini cha Mshahara na Masharti ya kazi yanayosimamia suala la mgogoro katika mwaka wa kwanza wa kutumika Tangazo hilo

Uhalali wa Mgomo Kisheria

Sheria ya Kazi imeweka mazingira na utaratibu ambao unapaswa kufuatwa ili mgomo wa wafanyakazi uweze kuwa halali. Hivyo wafanyakazi ambao wanahitaji kutumia haki yao ya kugoma lazima wafuate masharti yafuatayo;

  • Mgogoro ni lazima uwe wa maslahi na si lalamiko
  • Mgogoro lazima uwe umewasilishwa Tume kwa ajili ya usuluhishi kwa kutumia fomu maalum
  • Mgogoro uwe umeshindikana kusuluhishwa ndani ya siku 30
  • Kura za kuunga mkono zipigwe na wafanyakazi husika kwa mujibu wa katiba ya chama cha wafanyakazi
  • Notisi ya saa 48 ya kuanza mgomo itolewe kwa mwajiri, saa hizo zitahesabiwa kwa saa za kawaida za kazi na lazima notisi ieleze mgomo utakuwa wa siku ngapi.

Hatahivyo yapo mazingira ambayo mgomo unaweza kufanyika pasipo kufuata utaratibu huo  endapo mwajiri amebalidisha masharti ya kazi bila kushauriana na wafanyakazi. Katika mazingira haya wafanyakazi wanatakiwa kuwasilisha mgogoro kwenye Tume wakimtaka mwajiri kutokutokeleza mabadiliko hayo au kama ameshaanza kutekeleza, kuyarejesha masharti ya awali kabla ya mabadiliko.

Ikiwa mwajiri hatatekeleza madai yaliyoelezwa na wafanyakazi ndani ya saa 48 kuanzia saa aliyopokea nakala ya fomu ya mgogoro, wafanyakazi wanaweza kugoma.

Mambo yanayokatazwa wakati wa Mgomo

  • Kuunga mkono mgomo
  • Kutoajiri na kutumia wafanyakazi wapya mbadala wakati wa mgomo
  • Kufungia waajiri ndani ya eneo la kazi
  • Kuwazuia waajiri kuingia katika eneo la kazi

Kiwango cha chini cha utoaji Huduma

Katika hali ya mgomo chama cha wafanyakazi na mwajiri wanaweza kufikia makubaliano ya pamoja juu ya utoaji wa huduma kwa kiwango cha chini wakati wa mgomo ambapo wafanyakazi wachache wataendelea kutoa huduma wakati mgomo ukiendelea.

Endapo pande zitakosa makubaliano ya pamoja, mwajiri anaweza kuwasilisha maombi kwenye kamati ya Huduma Muhimu, kabainisha au kuomba baadhi ya wafanyakazi waendelee na kazi wakati wa mgomo iwapo kiwango hicho cha chini cha huduma ni muhimu katika kuzuia uharibifu wa mali au mashine wakati wa mgomo.

Madhara ya Mgomo usiofuata utaratibu au kufanya vitendo vilivyokatazwa

Endapo wafanyakazi wanashiriki mgomo ambao umefanyika bila kufuata taratibu na kutenda vitendo vilivyokatazwa basi Mahakama ya kazi itakuwa na mamlaka;

  • Kutoa amri ya zuio kumzuia mtu yeyote kushiriki katika mgomo au kutenda kitendo kilichokatazwa
  • Kuamuru kulipwa fidia kwa hasara iliyosababishwa na mgomo huo au kitendo hicho kilichokatazwa.

Hitimisho

Mgomo ni haki ya wafanyakazi hata hivyo haitakiwi kutumika vibaya kwani itapelekea kuzorota kwa kazi na uzalishaji mahali pa kazi. Haki hii inapaswa kutumiwa kama suluhu ya mwisho kabisa na wafanyakazi. Muhimu pande zote kuhusika kwenye mazungumzo endapo kutajitokeza changamoto za kimaslahi mahali pa kazi.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.