Haki ya Uhuru wa Mawazo

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu  kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Uhuru wa Mtu kwenda atakako. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Haki ya Uhuru wa Mawazo

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anayo Haki ya Uhuru wa Mawazo. Ibara ya 18 ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu-

  • Anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake;
  • Anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi;
  • Anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake; na
  • Anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii’

Ufafanuzi

Uhuru wa maoni na kueleza fikra zake

Kama tunavyofahamu sisi wote tumezaliwa huru na haki hii ya uhuru tumepewa na Mungu mwenyewe. Haki hii si zao la Katiba pekee bali ni asili ya mwanadamu. Tunafahamu kuwa binadamu hatufanani ikiwa kwa sura, haiba au utu wetu yaani tupo tofauti. Kwa msingi huu ni vyema tukatambua hata mawazo yetu na fikra ni tofauti hatuwezi kufanana na haitotokea sote tukawa na fikra sawa.

Hivyo ni muhimu sana sisi sote, wakubwa kwa wadogo, wananchi kwa viongozi kutambua na kuheshimu haki hii ambayo si tu ni ya asili bali inadhibitishwa na Katiba ya JMT. Kutofautiana kimawazo au kifikra si dhambi ndio afya yenyewe ya kuweza kujenga kwa pamoja.

Haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi

Nyakati tunazoishi zimegubikwa na utawala wa sayansi na teknolojia kila mahali na kila kukicha. Ulimwengu umekuwa na kasi kubwa sana hasa kwenye masuala ya upashanaji habari. Katiba ya JMT inadhibitisha kuwa mwananchi yeyote ana haki ya kupata taarifa haijalishi zinapotoka na pia anayo haki ya kusambaza taarifa.

Muhimu kuzingatia katika utekelezaji wa haki hii kwa mwananchi ni lazima kutumia haki hii pasipo kuvunja sheria. Pamekuwa na uenezaji wa taarifa zisizo za kweli nyakati kama hizi au taarifa zenye kuamsha chuki au taharuki maeneo mbali mbali, hivyo uhakika wa taarifa na ukweli wa taarifa husika ni wa kuzingatia mara zote. Zipo sheria zinazoanisha usambazaji wa taarifa kupitia mitandao na makosa yanayoweza kujitokeza katika usambazaji huo.

Uhuru wa kufanya mawasiliano na kutokuingiliwa kwa mawasiliano yake

Kama ilivyoanishwa kwenye Katiba ya JMT pia kupitia Ibara 16 (1) inavyozingumzia haki ya faragha ya mtu binafsi. Kadhilika kila mmoja ana haki ya kufanya mawasiliano na mawasiliano hayo yanalindwa kwa mujibu wa sheria.

Changamoto inayojitokeza katika utekelezaji wa haki hii ni watu kutokutumia uhuru huu vizuri kwa mawasiliano kutumika kwa nia ovu ya kutenda uhalifu. Ikiwa mtu atatumia mawasiliano vibaya basi vyombo vya sheria vinaweza kuingilia mawasiliano hayo ili kubaini makosa yaliyotendwa na mtu husika.

Muhimu kuzingatia haki hii ni lazima itumiwe kwa nia njema ya kupeana taarifa mbalimbali ambazo zinakuza mahusiano ya kijamii na zenye tija kwa taifa.

Haki ya kupewa taarifa kuhusu matukio mbalimbali ya kijamii

Mwanadamu ni kiumbe wa kijamii ambaye mara zote anataka kujua kile kinachoendelea katika mazingira yake. Hitaji la taarifa kwa mwanadamu ni hitaji la msingi mno kwani kwa njia moja ama nyingine linaathiri uwezo wake wa kufanya maamuzi au kutokufanya maamuzi. Hivyo ni muhimu kuwepo na mfumo wa kisheria kama ilivyo hapa kwetu kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusiana na mambo mbalimbali ya mwenendo wa taifa lao.

Hitimisho

Haki ya uhuru wa mawazo katika nyakati hizi imekumbwa na changamoto nyingi sana. Kwa vyovyote vile bado ni muhimu kwetu kujenga mfumo wa kuaminiana na kuwa na nia ya dhati katika mawazo tunayotoa au taarifa zinazotolewa kwa nia ya kujenga na si kubomoa. Kama nilivyosema hatuwezi kufanana katika mawazo yetu lakini lazima tuwe na misingi tunayoisimamia kama taifa ili tuweze kutoa mawazo ambayo yanashajiisha kujenga umoja, utangamano, amani na hali ya kuvumiliana katika tofauti tulizonazo.

 ‘Uhuru wa mawazo ni wako, tumia uhuru huo kwa nia ya kujenga umoja’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili