12.B. Majadiliano ya Pamoja


Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiishambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita  tulijifunza sehemu ya kwanza ya Majadiliano ya pamoja. Leo tunakwenda kuona sehemu ya pili ya majadiliano ya pamoja. Karibu tujifunze.

 

Wajibu wa Kujadiliana kwa nia njema

Pande zote zinazohusika na majadiliano ya pamoja zinapaswa kufanya majadiliano haya kwa nia njema. Katika wajibu huu wa kujadiliana kwa nia njema pande zote zinapaswa kuonesha yafuatayo;

 • Heshima kwa wawakilishi wa pande zote
 • Maandalizi ya pande zote kabla ya majadiliano
 • Kutokubadili wawakilishi pasipo sababu za msingi
 • Kuhudhuria vikao kwa wakati
 • Kutoa sababu ya kila pendekezo linalowasiliswa na kupokea mapendekezo kwa nia ya kuyatafakari na ikiwa hayakubaliwi kutoa sababu za msingi.

Vipo viashiria ambavyo vinaweza kuoneshwa na upande wowote kudhihirisha kuwa hawana nia njeama katika majadiliano. Viashiria hivyo ni kama

 • Kutoa madai makubwa yasiyotekelezeka
 • Kukataa bila sababu za msingi kupunguza baadhi ya mapendekezo
 • Kutokutoa taarifa muhimu za kuwezesha majadiliano kufanyika
 • Kutotumia lugha ya staha, mfano matusi, kejeli na dharau
 • Kuchelewesha majadiliano pasipo sababu
 • Kuweka masharti yasiyo ya msingi ili kuruhusu majadiliano kuendelea
 • Kuwazunguka wawakilishi wa upande mwengine wakati majadiliano yanaendelea
 • Kuanza kuchukua hatua za upande mmoja wakati majadiliano hayajakamilika. Mfano hatua ya kugoma.

Jukumu la kutoa Taarifa Muhimu

Sheria ya Kazi inaelekeza katika majadiliano ya pamoja endapo zipo taarifa muhimu zitakazosaidia majadiliano kufanyika kwa ufanisi basi mwajiri ana wajibu wa kuzitoa taarifa hizo. Lengo la sheria ni kuhakikisha majadilino yanafanyika kwa nia njema, yanakamilika haraka iwezekanavyo na kujenga hali ya kuaminiana kwa pande zote.

Mwajiri atawajibika kutoa taarifa zile ambazo zinahusika kwenye majadiliano na si vinginevyo. Hata hivyo mwajiri hatolazimika kutoa taarifa ambazo;

 • Ana kinga ya kisheria kutozitoa
 • Akizitoa atakuwa anakiuka amri au zuio alilowekewa na sheria au Mahakama
 • Ni za siri na zinazoweza kusababisha madhara kwa mfanyakazi au mwajiri iwapo zitatolewa
 • Ni taarifa binafsi za mfanyakazi bila ridhaa ya mfanyakazi husika

Upo utaratibu wa kuomba kupatiwa taarifa muhimu kwa ajili ya majadiliano ambao chama kinapaswa kuufuata.

 • Kutoa taarifa ya maandishi mapema iwezekanavyo, ili kutoa nafasi kwa mwajiri kuandaa na kuwasilisha taarifa hizo
 • Taarifa zinazotolewa kwa chama zikiwa za siri kina wajibu wa kuzitunza

Mchakato wa majadiliano unahitimika kwa njia mbili yaani kufikiwa kwa makubaliano au upande mmoja kutangaza kukwama kwa majadiliano.

Makubaliano ya Pamoja

Huu ni mkataba baina ya pande mbili yaani chama cha wafanyakazi ambaye anatambulika kama wakala wa wafanyakazi na mwajiri baada ya kufikia mwafaka kwenye mambo waliyojadiliana.

Sifa ya makubaliano ya pamoja

 • Yanapaswa kutiwa saini na pande zote
 • Yawawabana pande zote kutekeleza masharti yaliyoanishwa katika makubaliano hayo
 • Yanawabana wanachama wa chama husika kilichokuwa wakala wa wafanyakazi
 • Yanawabana pia wafanyakazi wasio wanachama ingawa walihusishwa kwenye kitengo cha majadiliano
 • Makubaliano hayo yanawabana waajiri na wafanyakazi waliokuwa sehemu ya makubaliano hayo wakati yanaanza kutumika hata kama watajiuzulu baada ya makubaliano
 • Makubaliano haya yatawabana pia waajiri na wafanyakazi watakaojiunga na jumuiya ya waajiri au chama cha wafanyakazi baada ya makubalinao hayo kuanza kutumika
 • Makubaliano yanaweza kusitishwa ikiwa upande wowote utatoa notisi
 • Nakala ya makubaliano lazima iwasilishwe kwa Kamishna wa Kazi

Kuondolewa kwa Utambuzi

Utambuzi wa chama cha wafanyakazi kama wakala pekee wa wafanyakazi katika kitengo cha majadiliano unaweza kuondolewa endapo wanachama wa chama hicho watapungua kwa zaidi ya nusu ya wafanyakazi katika kitengo cha majadiliano. Hata hivyo utambuzi huo hauwezi kuondolewa kabla ya miezi 6 kuanzia tarehe ya chama kutambuliwa.

Utaratibu wa kuondoa utambuzi kwa chama ambacho ni wakala wa majadiliano;

 • Mwajiri anapaswa kukipatia notisi ya miezi 3 kiongeze uwakilishi wake
 • Ikiwa chama kitashindwa kuongeza idadi ya uwakilishi wake mara baada ya notisi ya miezi 3 basi mwajiri atakiondolea utambuzi
 • Chama kinachotambuliwa kikipoteza uwakilishi basi chama kingine chenye idadi kubwa ya wafanyakazi kwenye kitengo cha majadiliano kinaweza kuomba kutambuliwa.

 

Hitimisho

Majadiliano ya pamoja baina ya mwajiri au chama cha waajiri na chama cha wafanyazi ni sehemu ya kusaidia kuleta tija na manufaa mahali pa kazi. Ikiwa majadiliano yatalenga katika kuleta ushirikiano basi pande zote zitanufaika yaani wafanyakazi na waajiri. Majadiliano ya pamoja yanalenga kuondoa au kupunguza uwezekano wa migogoro mahala pa kazi. Ni muhumu pande zote kuzingatia fursa hii ya kufanya mazungumzo.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili