Uhuru wa Mtu kwenda atakako

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Haki ya Faragha. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Uhuru wa Mtu kwenda akakako

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anao na Uhuru wa kwenda mahali anapotaka. Ibara ya 17 (1) ya Katiba ya JMT inasema

kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano’

Ufafanuzi

Mwanadamu ameumbwa kuwa huru na eneo moja wapo la uhuru ni kwenda mahali anapotaka. Tanzanzia ni nchi moja inayounganisha Tanzania Bara na Zanzibar. Haki hii ya uhuru wamepewa raia wote wa Tanzania.

Moja wapo ya hali inayosababisha utangamano au umoja wa taifa hili ni matumizi makubwa ya haki hii. Katika kila eneo la Tanzania utakuta watu kutoka maeneo mbali mbali ya nchi hii. Utaona waliotoka kaskazini wapo kusini, waliotoka mashariki wapo magharibi, na waliotoka kanda ya kati wapo kila mahali. Hii ni tunu kubwa kwa taifa. Tanzania ni moja wapo mwa mataifa machache ya kiafrika ambayo yamechanganya utamaduni wake kwa watu kuoana pasipo kuzingatia makabila yao au eneo wanalotoka.

Katika taifa hili zipo fursa nyingi kila kona ambazo kila mwananchi anaweza kuzitumia endapo atachukua hatua ya kwenda mahali husika.

Katiba pia inatoa uhuru wa raia kuingia na kutoka nchini kwa mujibu wa sheria. Zipo tararibu ambazo zitakutaka uwe na pasi ya kusafiria ambayo itakutambulisha uraia wako.

Hata hivyo Katiba kupitia Ibara ya 17 (2) inaeleza mazingira ambayo haki hii inaweza kuingiliwa na Mamlaka za nchi;

(2) kitendo chochote cha halali au sheria yoyote yenye madhumuni ya-

  • kupunguza uhuru wa mtu kwenda atakako na kumweka chini ya ulinzi au kifungoni; au
  • kuweka mipaka kwa matumizi ya uhuru wa mtu kwenda anakotaka ili-
  1. kutekeleza hukumu au amri ya mahakama; au
  2. kumlazimisha mtu kutimiza kwanza wajibu wowote anaotakiwa na sheria nyingine kuutimiza; au
  • kulinda manufaa ya umma kwa jumla au kuhifadhi maslahi fulani mahususi au maslahi ya sehemu fulani ya umma. Kitendo hicho hakitahesabiwa au sheria hiyo haitahesabiwa kuwa ni haramu au ni kinyume cha ibara hii’

Hitimisho

Uhuru wa kwenda unakotaka ni muhimu sana kwa wananchi kuutambua na kuutumia. Muhimu sana katika uhuru huu kuhakikisha huko unakokwenda ni kwa ajili ya manufaa yaani wewe unufaike na jamii ambayo umeenda inufanike kutokana na kile utakachokuwa umeenda kufanya katika eneo hilo. Uhuru huu ni lazima utekelezwe kwa njia ambayo sheria na kanuni hazivunjwi na muhusika.

 ‘tumia uhuru wa kwenda utakako katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uvumbue fursa mpya za kimaisha’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies

Comments are closed.