Haki ya Faragha na Usalama wa Mtu

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Haki ya Uhuru  wa Mtu Binafsi. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze

Maana ya Haki ya Faragha na Usalama

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anayo haki ya Faragha na Usalama. Ibara ya 16 (1) ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi’

Katika kujenga jamii iliyostaarabika na yenye kujali maslahi mapana ya kila mwanajamii heshima ni kitu muhimu sana. Heshima inayozungumzwa kwenye Katiba ya JMT ni ile ambayo haibagui mtu yeyote ikiwa ni kwa haiba yake, wadhifa, hali ya kiuchumi, eneo analotoka au kabila lake, binadamu wote ni sawa na wanastahili heshima.

Katiba inaenda mbali zaidi kuelezea juu ya umuhimu wa uhifadhi wa nafsi ya kila mmoja maisha yake binafsi na familia yake na mahusiano yake ya kindoa. Hili ni jambo muhimu sana katika jamii ambapo heshima inajengwa na watu wenye staha.

Hivi karibuni tumeshuhudia matukio mengi ya kuvunjiwa heshima wakubwa kwa wadogo, mambo ya kutisha yanafanyika kwenye jamii zetu, ukatili dhidi ya watoto au wanajamii. Mahusiano ya kingono yasiyoruhusiwa baina ya ndugu au watoto na wazazi haya ni mambo ambayo yanakiuka misingi ya ujenzi wa taifa bora linalojitambua na kujiamini. Mfumo wa kijamii lazima ujengwe kuanzia kwa watoto wetu hata watu wazima ili kujiletea maendeleo.

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia upashanaji wa habari umekuwa rahisi na wa kasi kubwa sana. Mitandao ya kijamii imeshika hatamu juu ya upashanaji wa habari. Haya yote ni mazuri, changamoto kubwa ni matumizi yasiyo sahihi kwenye vyombo hivi vya kisasa kwani watumiaji hawana uwezo wa kuchuja ni taarifa zipi ziende kwenye jamii na zipi ni binafsi. Kwa kukosa weledi huu tunashuhudia picha nyingi za kutisha na zenye kuweza kuleta msongo wa mawazo kwa watu wanaoziona na kufikiria. Pamekuwa na taarifa nyingi za uongo na kuzusha siku kwa siku kiasi watu kupoteza dira na kujishughulisha na mambo yasiyo na msingi.

Hata hivyo Katiba kupitia Ibara ya 16 (2) inaeleza mazingira ambayo haki hii inaweza kuingiliwa na Mamlaka za nchi;

‘kwa madhumuni ya kuifadhi haki ya mtu kwa mujibu wa ibara hii, Mamlaka ya Nchi itaweka utaratibu wa sheria kuhusu hali, namna na kiasi ambacho haki ya mtu ya faragha na usalama wa nafsi yake, mali yake na maskani yake, yaweza kuingiliwa bila kuathiri ibara hii’

Kama tunavyoona hakuna uhuru ambao hauna mipaka, kwa jinsi binadamu tulivyo tungependa kutumia uhuru wote tulionao katika kufanya kile tunachoona kinatufaa. Hata hivyo kwa kuwa hatuwezi kuutumia vizuri uhuru sheria inaweka utaratibu wa kuratibu uhuru huu kwa malengo mapana ya kunufaisha jamii.

Ni haki ya kila mmoja kuwa na mawasiliano na uhifadhi wa maisha yake binafsi hata hivyo endapo katika kutekeleza haki hii mtu ataingilia uhuru na haki ya mtu mwengine, sheria itakuwepo kwa ajili ya kumwajibisha.

Hitimisho

Ni muhimu kwetu kama jamii nzima kuthamini kila mtu na jirani yake na kutoa heshima inayostahili na kustahi maisha yaw engine na makazi yao na mawasiliano yao. Ni vyema kwetu kujenga kwa pamoja jamii iliyo na malengo muhimu ya kutimiza katika ujenzi wa taifa letu. Tupunguze au tuache kabisa tabia ya kutumia uhuru wetu juu ya mawasiliano katika kushusha au kuharibu hadhi ya mtu mwengine bali tuutumie katika kuungana na kusaidia kufikia malengo ya nchi.

 ‘Uhuru wako unapoishia ndio mwanzo wa haki ya mwenzako hivyo thamini maisha binafsi ya mwenzako naye atathamini yako’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili