Haki ya Uhuru wa Mtu Binafsi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza zaidi juu ya Haki ya Kuishi na Adhabu ya Kifo. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya haki mbali mbali za kibinadamu kama zilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Haki ya Uhuru wa mtu binafsi

Katiba ya JMT inaeleza wazi wazi kuwa kila mwananchi anayo Haki ya Uhuru binafsi. Ibara ya 15 (1) ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru

Kama Katiba inavyobaisha juu ya haki hii ya muhimu kwa kila mwanadamu ni kuwa huru. Sisi sote tumezaliwa huru hatufanani na tofauti zetu ndizo zinajenga jamii njema kwa kutoshelezana mahitaji yetu.

Mwanadamu amezaliwa huru ili aweze kuutumia uhuru wake vyema katika kujiletea maendeleo na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Katiba inaendelea kufafanua juu ya uhuru wa mtu binafsi kupitia Ibara ndogo ya 15 (2) kama inavyosema;

‘kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo, isipokuwa  tu

  • Katika hali na kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria; au
  • Katika kutekeleza hukumu, amri au adhabu iliyotolewa na mahakama kutokana na shauri au na mtu kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.

Ufafanuzi

Kama inavyojieleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya uhuru wa mtu binafsi ambapo imetoa katazo la dhahiri kwa mtu yeyote au chombo chochote kunyang’anya uhuru wa mtu kwa njia zilizoanishwa.

Hata hivyo katazo hili halitatumika katika mazingira kama yalivyoneshwa hapo juu yaani kwa mtu kukamatwa kwa mujibu wa sheria au ikiwa ni kutekeleza amri ya mahakama mfano mtu amehukumiwa kifungo gerezani.

Ni muhimu sana kwetu wote kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni mbali mbali katika utekelezaji wetu wa majukumu ya kila siku ikiwa ni mwananchi au vyombo mbali mbali vilivyoundwa na sheria ili kutekeleza wajibu wao.

Hitimisho

Uhuru ni jambo jema sana ambalo mtu anazaliwa nalo ni haki ambayo wote tumepewa na Mungu na kila mmoja wetu angependa kufurahia uhuru wake. Sisi kama taifa pia tunafurahia uhuru wetu ambao tunaadhimisha kila tarehe 9/12 tukienzi kazi njema zilizofanywa na waasisi wa taifa hili.

Hata hivyo ili uhuru uwe kamili na wenye manufaa ni vyema ukatumiwa kwa malengo mazuri yaani kujiletea maendeleo na kunufaishwa wananchi wengine na kutoa mchango mwema kwa taifa letu. Uhuru unaotumika vibaya una madhara kwa mtu binafsi na kwa taifa kwa ujumla.

Umezaliwa huru, dumisha uhuru na linda uhuru siku zote kwa kutimiza wajibu wako’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili