12.A. Majadiliano ya Pamoja
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tulijifunza juu ya Haki za Chama cha Wafanyakazi na kuzijadili nama zinavyoweza kutekelezwa. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Majadiliano ya Pamoja. Karibu tujifunze.
Maana ya Majadiliano ya Pamoja
Majadiliano ya pamoja ni mazungumzo yanayofanywa baina ya chama cha wafanyakazi kinachotambuliwa na mwajiri kama wakala wa wafanyakazi katika majadiliano na mwajiri au jumuiya ya waajiri kwa lengo la kuboresha maslahi ya pande zote na kuepusha migogoro mahali pa kazi.
Katika majadiliano ya pamoja vyama vya wafanyakazi vinaweza kuunda mseto na kuwa wakala wa wafanyakazi katika majadiliano na upande wa mwajiri.
Majadiliano ya pamoja yanaweza kufanyika kuhusisha sehemu moja ya kazi au sehemu nyingi zaidi mahali pa kazi. Hivyo katika utaratibu wa majadiliano ya pamoja kinaainishwa kitengo cha majadiliano yaani kundi la wafanyakazi ambalo litahusika na makubaliano yoyote yatakayofikiwa baina ya chama na mwajiri baada ya majadiliano.
Kutambuliwa kwa Chama kama Wakala wa Wafanyakazi
Katika mahali pa kazi kunaweza kuwa na wanachama wa vyama vya wafanyakazi mbalimbali, hivyo mchakato wa utambuzi ili chama kiweze kuteuliwa kama wakala wa wafanyakazi lazima ufanyike. Sifa kuu ya kuwezesha chama kutambuliwa kama wakala wa majadiliano kuwa kimesajiliwa na kina wanachama wengi zaidi ya vyama vingine mahali pa kazi.
Utaratibu wa chama kutambuliwa
Chama cha wafanyakazi kinachotaka kutambuliwa kama wakala wa wafanyakazi kwenye majadiliano ya pamoja kinapaswa kufanya yafuatayo;
- Kujaza fomu maalum na kuiwasilisha kwa mwajiri au jumuiya ya waajiri ikipendekeza kitengo cha majadiliano na kuambatanisha ushahidi wa nyaraka juu ya uwakilishi wao wa wafanyakazi wengi
- Mwajiri anapaswa ndani ya siku 30 baada ya kupokea fomu kukutana na chama na ikiwezekana wafikie mwafaka wa kukitambua chama kama wakala pekee wa wafanyakazi katika kitengo cha majadiliano
- Ikiwa baada ya siku 30 hakuna mwafaka wa utambuzi wa chama kama wakala, chama kinaweza kuwasilisha mgogoro mbele ya Tume kwa usuluhishi
- Tume itafanya usuluhishi ndani ya siku 30 baada ya kupokea mgogoro na kufikia makubaliano ya pande zote. Ikishindikana usuluhishi basi chama kinaweza kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kazi kwa uamuzi.
- Mahakama ya Kazi inaweza kuiagiza Tume isimamie zoezi la upigaji kura iwapo mgogoro unahusu uwakilishi au idadi ya wanachama katika kitengo cha majadiliano.
Mambo ya Msingi ya Majadiliano
Yapo maswala mengi yanayoweza kuhusika katika majadiliano ya pamoja baina ya mwajiri na chama cha wafanyakazi. Baadhi ya mambo hayo yameainishwa
- Mishahara na aina nyingine za ujira
- Masharti ya hali ya ajira kwenye mkataba wa ajira kama vile saa za kazi, muda wa likizo, muda wa notisi, n.k
- Masharti ya hali ya ajira kama vile nidhamu mahali pa kazi, huduma za afya na usalama mahali pa kazi n.k
- Posho, marupurupu na mafao ya ajira
- Sera na mazoea ya ajira kuhusiana na ajira mpya, uteuzi, mafunzo, uhamisho, kupanda vyeo, kusimamisha wafanyakazi n.k
- Uhusiano kazini ikiwemo haki za chama, taratibu za majadiliano na utatuzi wa migogoro, malalamiko, nidhamu na usitishaji ajira.
- Mambo mengine ambayo pande zote zitaafikiana
Itaendelea…
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili