Wajibu wa Kulinda Mali ya Umma

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Utii wa Sheria. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya wajibu wa kila mwanajamii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Wajibu wa Kulinda Mali ya Umma

Wajibu ni jambo ambalo mtu anawajibika au analazimika kulifanya. Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anawajibu wa kulinda mali ya Umma Ibara ya 27 (1) ya Katiba ya JMT inasema

Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine’

Ufafanuzi

Katiba inaeleza juu ya wajibu au sharti kwa kila mwananchi kulinda na kutunza mali ya Umma. Mali za uuma zinahusisha mali asilia ya Tanzania, mali zinazomilikiwa na serikali na pia zile ambazo zinamilikiwa kwa pamoja na wananchi. Mali hizi zinahusisha mali za kale, misitu, hifadhi za wanyama, miundombinu kama barabara, reli, mabomba ya mafuta au gesi.

Katiba inaendelea kufafanua juu ya ulinzi huo katika Ibara ya 27(2) inaendelea kufafanua zaidi juu ya;

Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadae ya taifa lao’

Hapa Katiba inatoa wajibu kwa wananchi na watu wote ambao watakuwa katika hali ya matumizi ya mali ya umma kuwa na umakini katika kutunza na kuzitumia kwa namna ya kuhakikisha haziharibiwi.

Kumekuwa na hali ya watu wanaokabidhiwa dhamana ya kusimamia mali za umma kuzifuja na kuzifanya kwa matumizi binafsi au maslahi yao. Katiba inamtaka kila mtu ambaye anaifahamu mali ya umma kuhakikisha inatunzwa vizuri na kutumiwa kwa maslahi mapana ya taifa kwa ujumla.

Endapo mwananchi atabaini ufujaji wa mali ya umma au ubadhilifu wa mali husika ni muhimu kutoa taarifa kwa vyombo husika ili upotevu huo usiendee kwani madhara yake ni kwa watu wote.

Hitimisho

Ni muhimu kila mmoja wetu kuzitazama mali za umma kama zetu binafsi ambavyo tunazitunza na kuziwekea ulinzi. Mali hizi ni za gharama kubwa na nyingine tumepewa kwa asili na Mwenyezi Mungu ikiwa ni madini au gesi au misitu na maji. Tuhakikishe kama vizazi vilivyotangulia viliweza kutunza kwa kutufikiria sisi wa kizazi cha sasa na sisi tunapaswa kuondoa ubinafsi ili kuwajali vizazi vijavyo ili nao ziwafae katika maendeleo yao.

mali ya umma inakuhusu, timiza wa wajibu wako kwa kuitunza na kuilinda isiharibiwe na kufujwa’.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili