17. Sababu za Kusitisha Ajira

 

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tulitaja kwa kifupi vigezo ambavyo mwajiri anapaswa kuvizingatia endapo anakusudia kusitisha ajira ya mfanyakazi. Katika makala ya leo tunaanza kuvichambua vigezo hivyo kila kimoja peke yake. Karibu tujifunze.

Maana ya Sababu za Usitishaji wa Ajira

Hakuna usitishaji wa ajira ambao hauna sababu. Kama kuajiri kwenye nafasi ya kazi kunakuwa na sababu, vivyo hivyo usitishaji wa ajira lazima uwe na sababu.

Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri pale anapoamua kuchukua hatua ya kusitisha ajira ya mfanyakazi atoe sababu za msingi na halali za usitishaji. Waajiri wengi wamekuwa na dhana potofu kuwa kama wanaweza kuajiri pia wanaweza ‘kumfukuza’ au kusitisha ajira ya mfanyakazi wakati wowote pasipo kutoa sababu yoyote, jambo ambalo si kweli. Nipende tu kuwa kumbusha waajiri kuwa mara unapoajiri tayari umeingia katika mahusiano ya kisheria ya mkataba baina yako na mfanyakazi iwe umeandikwa au hujaandikwa. Hivyo kuna wajibu na haki za kisheria zinazosimamia pande zote. Mwajiri hupaswi kufikiri kuwa una uwezo na mamlaka ya kusitisha ajira au ‘ kumfukuza’ mfanyakazi kazi kama upendavyo.

Hii haijalishi ni aina gani ya ajira yaani inaweza kuwa ni ajira ya ofisini, kwenye biashara, dukani, ajira za wasaidizi wa nyumbani- house girls na house boys au shamba boy n.k. alimradi yapo mahusiano ya kiajira baina yenu kuna matakwa ya kisheria ya kufuata ili kusitisha ajira.

Sheria ya Ajira inatamka wazi kuwa, ili usitishaji wa ajira ya mfanyakazi unaofanywa na mwajiri uwe halali ni lazima iwepo sababu ambayo ni ya;

  • Haki
  • Sababu ya Halali; ambayo inaweza kuhusiana na utendaji wa mfanyakazi, uwezo au kutokuhitajika au inayohusiana na kupunguza wafanyakazi.
  1. Nini maana ya sababu ya Haki

Kama nilivyoeleza hapo awali kuwa mwajiri lazima atoe sababu ya msingi na sababu hiyo lazima iwe ya Haki. Isiwe sababu ya kumwonea mfanyakazi bali iwe ya haki yaani ambayo ikiletwa katika mizania ya kisheria inakubalika. Mfano wa sababu ya haki inaweza kuwa tabia mbaya ya mfanyakazi kama kupigana, kutukana au kuharibu mali ya mwajiri n.k

  1. Sababu Halali

Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri kuhakikisha kuwa sababu hiyo ni halali. Sheria inaainisha kuwa sababu kuwa halali ni zile zinazohusiana na

  • utovu wa nidhamu wa mfanyakazi,
  • uwezo mdogo wa kazi
  • kutohitajika
  • mahitaji ya uendeshaji

hizi ni sababu ambazo kisheria zinahesabika kuwa ni halali. Katika makala zinazofuata tutaziangalia kwa undani na namna zinavyoweza kutumika. Kwa kuwa kila sababu ina mchakato wake na namna ambavyo inaweza kutumika.

Sababu ambazo si Halali Kisheria

Haitahesabika kuwa ni sababu halali iwapo mwajiri atamwachisha kazi mfanyakazi kwa mojawapo ya sababu zifuatazo;-

  • Mfanyakazi katoa taarifa ambazo anapaswa kuzitoa kwa mujibu wa sheria
  • Mfanyakazi kushindwa au kukataa kufanya jambo lolote linalokatazwa na sheria
  • Mfanyakazi kutekeleza haki zake kwa mujibu wa sheria
  • Mfanyakazi kuwa mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi
  • Mfanyakazi kushiriki katika shughuli halali za Chama cha Wafanyakazi ikiwemo mgomo halali
  • Ulemavu
  • Ujauzito
  • Ubaguzi

Mwajiri lazima azingatie wakati wote kuwa sababu lazima iwe ya haki na halali ili kusitisha ajira kuwe kwa mujibu wa sheria.

Hitimisho

Sababu za msingi na halali lazima zitolewe na mwajiri pindi anapokusudia kumwachisha kazi mfanyakazi. Mwajiri hapaswi kuchukua maamuzi ya kumfukuza au kumwachisha kazi mfanyakazi pasipo kutoa sababu. Moja ya malalamiko mengi mbele ya Tume ni wafanyakazi wengi kuachishwa kazi pasipo sababu yoyote. Waajiri wanaona kuwa hawana wajibu wa kutoa sababu kwa mfanyakazi ya kumwachisha kazi. Wadau wa ajira lazima kujua kuwa kusitisha ajira lazima ziwepo sababu.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.