58. Wajibu wa Kulinda Taifa

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya wajibu wa Kulinda Mali ya Umma. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya wajibu wa kila mwanajamii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Wajibu wa Kulinda Taifa

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kulinda Taifa. Ibara ya 28 (1) ya Katiba ya JMT inaeleza

Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi, na umoja wa taifa’

Ufafanuzi

Raia wote wa Tanzania wanalazimika kuhakikisha uhuru wetu na mamlaka ya nchi vinalindwa. Kila raia ana wajibu wa kutunza ardhi ya Tanzania na umoja wa kitaifa.  Ardhi ya Tanzania ni mali ya umma sote tuna wajibu wa kuhakikishwa inalindwa vyema dhidi ya maadui na inatumika kwa manufaa ya umma.

Katika kutekeleza wajibu huu Bunge lina mamlaka ya kutunga sheria kwa ajili ya kuwezesha wananchi kutumikia katika majeshi na katika ulinzi wa taifa, hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 28 (2) ya Katiba.

Ibara ya 28 (3) ya Katiba inaonesha katazo kwa wananchi wote juu ya kujisalimisha kama taifa kwa adui.

‘mtu yeyote hatakuwa na haki ya kutia sahihi kwenye mkataba wa kukubali kushindwa vita na kulitoa taifa kwa mshindi, wala kuridhia au kutambua kitendo cha uvamizi au mgawanyiko wa Jamhuri ya Muungano au wa sehemu yoyote ya ardhi ya eneo la taifa na bila ya kuathiri Katiba hii na sheria zilizowekwa, hakuna mtu atakayekuwa na haki ya kuwazuia raia wa Jamhuri ya Muungano kupigana vita dhidi ya adui yeyote atakayeshambulia nchi’

Wajibu wa kila mwananchi kama ilivyoaishwa katika Ibara hii ya 28 ni kuilinda Tanzania kwa gharama yoyote. Mwananchi yoyote anakatazwa kushiriki au kuingia mkataba wa kukubali kushindwa au kuitoa sehemu ya Jamhuri ya Tanzania kwa adui yeyote. Ni kosa kubwa ambalo litahesabika kuwa ni uhaini kama inavyoainishwa katika Ibara ya 28 (4) ya Katiba.

Hitimisho

Nchi yeyote ili iweze kustawi na kuwa na maendeleo ni lazima iwe na mfumo wa ulinzi kwa kujilinda dhidi ya maadui wa ndani au wa nje. Kila mwananchi anapaswa kuonesha uzalendo wake kwa kujitoa kwa hali na mali na maarifa ya kuitetea nchi yake, uhuru wake, mamlaka za nchi, ardhi pamoja na umoja wa taifa. Hizi ni nguzo muhimu sana kwa taifa lolote duniani. Watanzania tujivunie taifa letu na kujitoa wakati wote katika kulinda nchi yetu na kuijenga kwa pamoja. Haifai kuendeleza tofauti sizizo na tija bali kila mmoja atumie mawazo yake, taaluma yake, kazi yake katika kujenga taifa. Pia tusipuuze mawazo yaw engine hata kama yana utofauti na yale tunayoona sisi ikiwa tuna nia ya kujenga taifa moja lenye mshikamano bila kuathiri tofauti za kidini, ukabila, vyama na hali za maisha.

 ‘Tanzania ni taifa lako, una wajibu wa kulilinda kwa gharama yoyote, hatuna taifa lingine, timiza wajibu wako.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili