Haki na Wajibu Muhimu
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya wajibu wa Kulinda Taifa. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya wajibu wa kila mwanajamii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.
Maana ya Haki na Wajibu Muhimu
Katiba ya JMT inaanisha juu ya haki na wajibu muhimu kwa kila mwananchi wa Tanzania katika Ibara ya 29 (1) ya Katiba ya JMT inaeleza
‘Kila mtu katika Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu, na matokeo ya kila mtu kutekeleza wajibu wake kwa jamii, kama zilivyofafanuliwa katika ibara ya 12 hadi ya 28 za sehemu hii ya Sura hii ya Katiba’
Ufafanuzi
Raia wote wa Tanzania wanayo haki ya kupata matunda ya haki za kibinadamu ambazo tumezijadili katika makala zilizotangulia. Haki hizo ni pamoja na haki ya kuishi, uhuru wa mawazo, uhuru wa imani, haki ya kufanya kazi, haki ya kumiliki mali na n.k.
Hata hivyo ni muhimu kukumbushana kuwa matunda au faida za haki hizi za kibinadamu ni matokeo ya kutimiza wajibu kwa kila mwananchi. Siku zote hakuna haki inayokuja peke yake pasipo wajibu, hivyo mahali penye kudai haki au kutaka kutendewa haki ni lazima kujiuliza kwanza ni wajibu gani ambao umetekeleza ili kupata haki hiyo. Haki ni matokeo ya wajibu ambao umetekelezwa na mtu katika eneo Fulani. Hivyo kwa msingi wa kuwa raia zipo haki ambazo unastahili kuzipata na wajibu wa kutekeleza ili haki hizo zipatikane.
Katiba inaendelea kufafanua juu ya usawa raia wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 29 (2), (3), (4),
‘Kila mtu katika Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kupata hifadhi sawa chini ya sheria za Jamhuri ya Muungano’
‘Raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano hatakuwa na haki, hadhi au cheo maalum kwa misingi ya nasaba, jadi au urithi wake’
‘Ni marufuku kwa sheria yoyote kutoa haki, hadhi au cheo maalum kwa raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano kwa misingi ya nasaba, jadi au urithi’
Ufafanuzi
Katiba inaweka wazi kuwa raia wote ni sawa na kila mmoja ana hadhi na uwezo wa kushika madaraka au cheo kutokana na vigezo vya kitaaluma au vingine vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.
Katiba imeweka marufuku juu ya kupata haki yoyote ikiwa ni ya madaraka au cheo kwa misingi ya kabila au jadi au hadhi au nasaba. Kila mmoja apate haki kwa mujibu wa vigezo husika vya kazi au shughuli husika.
Halikadhalika Katiba inaweka mazingira ya kila mtu kuweza kufaidi haki zinazotolewa katika Katiba kwa kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi kwa namna ambayo haingiliia haki za mwengine. Ibara ya 29 (5) inaeleza;
‘Ili watu wote waweze kufaidi haki na uhuru vilivyotajwa na Katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haingilii haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma’
Muhimu kwa wananchi kutambua kwamba pale ambapo haki yako inaanzia ndipo pale wajibu wako wa kulinda haki ya mwengina unaanzia. Si sahihi katika kutekeleza uhuru na haki zako za kikatiba na wakati huo huo katika kutekeleza huko unaingilia haki na uhuru wa watu au mtu mwengine.
Hitimisho
Kama tulivyosema kuwa haki na wajibu ni vitu vinavyoendana sana ni kama pande mbili za shilingi huwezi kuvitenganisha. Ni muhimu sana kufahamu haki zako kama raia wa Tanzania ili uhakikishe haki hizo zinalindwa. Lakini ni vyema zaidi kufahamu wajibu wako ili utekeleze kila siku na kuhakikisha haki zako zinatimizwa.
‘Usiulize Tanzania itakufanyia nini, jiulize wewe utaifanyia nini Tanzania, timiza wajibu wako upate haki yako.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili