Mipaka ya Haki na Uhuru

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Haki na Wajibu Muhimu. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya wajibu wa kila mwanajamii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Maana ya Mipaka ya Haki na Uhuru

Katiba ya JMT inaeleza juu ya mipaka iliyowekwa na Katiba juu ya haki na uhuru ambao wamepewa raia kwa mujibu wa Ibara ya 30 (1) ya Katiba ya JMT inaeleza

Haki na uhuri wa binaamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma’

Ufafanuzi

Kama tulivyoeleza katika makala zilizotangulia kuwa haki na uhuru wako binafsi havipaswi kuwa chanzo cha kukosa haki na uhuru kwa watu wengine au umma kwa ujumla. Hivyo hakuna haki au uhuru usio na mipaka. Mipaka au ukomo wa haki na uhuru ni kwa kiwango haki na uhuru wako unavyoweza kuathiri au kuingilia haki na uhuru wa wengine.

Kanuni kuu ya kufahamu juu ya dhana ya haki na uhuru wako ni ile kanuni ya kimaandiko inayosema mpende jirani yako kama nafsi yako mwenyewe’ hii inaonesha kwamba kwa kiwango kile ambacho ungependa haki zako na uhuru wako uheshimiwe na kulindwa basi hakikisha nawe unafanya kwa kiasi hicho kwa jirani yako. Jirani yako  ni mtu yeyote ambaye anaathirika kwa njia moja ama nyingine kutokana na kauli zako au matendo yako. Kama usingependa utu wako udhalilike, au mambo yako ya siri (haki ya faragha) yasijulikane kwa watu vivyo hivyo hakikisha unamstahi jirani yako maana kufanya kinyume chake ni kuvunja haki ya mwenzako.

Katiba inaendelea kuanisha juu ya mipaka ya haki na uhuru kwa kusababisha sheria kutungwa ili kulinda haki za watu wengine na maslahi mapana ya umma kwa ujumla, sawa na Ibara ya 30 (2)

‘Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika Sehemu hii ya Katiba hii, yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, hayaharamishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo kwa ajili ya;-

  • Kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi;
  • Kuhakikisha ulinzi, usalama wa jamii, maadili ya jamii, afya ya jamii, mipango ya maendeleo ya miji na vijiji, ukuzaji na matumizi ya madini au ukuzaji na uendelezaji wa mali au maslahi mengineyo yoyote kwa nia ya kukuza maslahi ya umma;
  • Kuhakikisha utekelezaji wa hukumu au amri ya mahakama iliyotolewa katika shauri lolote la madai au la jinai
  • Kulinda sifa, haki na uhuru wa watu wengine au maisha binafsi ya watu wanaohusika katika mashauri mahakamani, kuzuia kutoa habari za siri; kutunza heshima, mamlaka na uhuru wa mahakama
  • Kuweka vizuizi, kusimamia na kudhibiti uanzishaji, uendeshaji na shughuli za vyama na mashirika ya watu binafsi nchini; au
  • Kuwezesha jambo jingine lolote kufanyika ambalo linastawisha au kuhifadhi maslahi taifa kwa jumla

Ufafanuzi

Hapa tunaona mamlaka pamoja na kuzitambua na kuziheshimu haki na uhuru wa kila raia, zinaweza kutunga sheria kwa ajili ya kulinda na kutetea haki za watu wengine na makundi mengine ikiwepo serikali na mambo yote ya maslahi ya umma. Hivyo mtu kabla hujaamua kutekeleza haki yako yoyote lazima uifahamu mipaka yake na namna ambavyo sheria zinalinda watu wengine na mamlaka za nchi dhidi ya kuharibiwa sifa au udhalilishaji.

Hitimisho

Eneo la mipaka ya haki na uhuru limekuwa na changamoto kubwa sana katika kufikia mwafaka, kwani wapo wanaoamini kuwa haki hizi za kibinadamu hazina mipaka lakini wapo wanaamini kuwa haki zina mipaka. Katiba imeweka wazi kuwa katika kutekeleza haki yako hakikisha upo ndani ya mipaka husika. Hakikisha kwenye uhuru wako wa kujieleza au imani yako au faragha kwa namna yoyote hauingilii haki na uhuru wa watu wengine, shughuli za umma, mamlaka za nchi, hadhi za watu ikiwa ni viongozi au raia wa kawaida.

Ni rai yangu kwa wananchi wenzangu kuwa na taadhari katika maneno na vitendo tunavyofanya kwa kudhani kuwa tuna haki tu ya kufanya chochote, sheria zipo na mamlaka za kutekeleza sheria zipo, tuepuke kuwa na matumizi mabaya hasa ya mitandao kutuma na kupokea jumbe ambazo zinaweza kuingilia haki na uhuru wa watu wengine na mamlaka mbali mbali katika nchi yetu.

 ‘Hakuna Haki na Uhuru usio na mipaka, jua mipaka yako uepuke madhara kwa wengine na juu yako’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili