18. Utaratibu wa Haki katika kusitisha Ajira

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tuliangalia kigezo cha Uwepo wa Sababu za halali katika usitishaji wa ajira. Katika makala ya leo tunaangalia kigezo kingine cha Utaratibu wa Haki. Karibu tujifunze.

Maana ya Utaratibu wa Haki katika Usitishaji wa Ajira

Kama tulivyozungumza kwenye makala zilizopita kuwa kama ilivyo wakati wa kuajiri ilivyo mchakato basi kadhalika suala la kuachisha ajira ni la mchakato. Hivyo ni muhimu sana kwa mwajiri kuzingatia mchakato husika.

Utaratibu wa haki unahusisha hatua mbali mbali ambazo zinazingatia sheria za kazi, kanuni na mazoea katika zoezi la usitishaji wa ajira.

Sheria ya Ajira inaeleza wazi kuwa, moja ya vigezo ambavyo mwajiri ni lazima azingatie katika kusitisha ajira ya mfanyakazi ni kufuata utaratibu wa haki.

Zipo hatua mbali mbali zinazopaswa kuchukuliwa na mwajiri endapo ananuia kusitisha ajira ya mfanyakazi. Hatua hizi zinategemea hasa ni sababu ipi ambayo inapelekea usitishwaji wa ajira husika. Katika makala iliyopita tulijadili kwa kina juu ya ulazima wa sababu za kusitisha ajira. Hivyo kwa kila sababu ya kusitisha ajira upo mchakato au utaratibu wa haki ambao mwajiri analazimika kuufuata ili kuhalalisha usitishaji wa ajira.

Mfano wa sababu zinazoweza kupelekea usitishaji wa ajira ni kama ifuatavyo;

  • Utovu wa kinidhamu
  • Kutohitajika
  • Uwezo mdogo wa kazi – kwa sababu ya ugonjwa, au ajali n.k
  • Mahitaji ya mwajiri – kupunguzwa kazi
  • Usitishaji wa ajira wakati wa majaribio (Probation employees)

Katika kila sababu ambazo zimeorodheshwa hapo juu, kuna utaratibu ambao mwajiri anapaswa kuufuata. Wengi wa waajiri wanachukua tu sababu yoyote ile na kumwachisha mfanyakazi mara moja pasipo kuzingatia utaratibu.

Utaratibu wa Haki

Upo utaratibu wa jumla ambao mwajiri anapaswa kuzingatia wakati anapositisha ajira ya mfanyakazi. Kama tulivyoeleza kuwa kila sababu ina utaratibu wake, hata hivyo yapo mambo ya msingi katika utaratibu lazima yazingatiwe kwa kila sababu.

Endapo mwajiri anakusudia kumwachisha kazi mfanyakazi ni lazima azingatie mambo kadhaa ya utaratibu;

  • Taarifa; mwajiri analazimika kumpatia taarifa ya maandishi mfanyakakazi pale anapokusudia kuanza mchakato utakaopelekea kusitisha ajira. Taaifa hii itaainisha sababu za mwajiri kutaka kusitisha ajira. Mfano kuna kosa la kinidhamu, mwajiri ni lazima amwandikie mfanyakazi tuhuma hizo na endapo kutahitajika kikao cha kinidhamu na tuhuma kudhibitishwa basi adhabu inaweza kuwa kuachishwa kazi.
  • Haki ya kujieleza; mwajiri lazima ampatie mfanyakazi haki ya kujieleza endapo suala la usitishaji wa ajiri litakuwa katika mjadala au masuala ya kinidhamu. Mwajiri hawezi kusitisha ajira ya mfanyakazi pasipo kumpa fursa ya kujieleza. Hii ni haki ya kiasili
  • Haki ya kuwakilishwa; endapo suala la usitishaji wa ajira litahusisha tuhuma za kinidhamu, basi mfanyakazi anaweza kuwakilishwa na mfanyakazi mwenzake katika kuandaa utetezi wake.
  • Haki ya kuhoji ushahidi na mashahidi wa mwajiri; mfanyakazi anapaswa kupatiwa haki ya kuhoji mashahidi na ushahidi wowote dhidi yake katika mchakato wa kuachishwa kazi endapo ni suala la kinidhamu
  • Ripoti ya uchunguzi; mwajiri ni lazima aandae ripoti ya uchunguzi katika suala la uachishwaji wa ajira ikiwa ni kwa tuhuma za kinidhamu. Mfanyakazi ana ruhusa ya kupata ripoti ya uchunguzi na kuhoji.
  • Haki ya kukata rufaa; mwajiri anapaswa kuhakikisha, mfanyakazi anayo haki ya kupinga maamuzi ya kusitisha ajira kwa kuweka mfumo wa kukata rufaa.
  • Malipo na stahiki za mfanyakazi; mwajiri anawajibika kuhakikisha mfanyakazi analipwa stahiki zake zote ambazo anadai wakati akiwa kazini pindi anapoachishwa kazi.

 

Hitimisho

Kusitisha ajira ni mchakato, si suala la kukurupuka kwa mwajiri hata kama yapo makosa makubwa yamefanywa na mfanyakazi. Mwajiri anapaswa kuchukua muda na kutafakari namna bora ya kuweza kusitisha ajira kwa njia halali ili kuepuka migogoro ya baadae ambayo wafanyakazi wengi wanafungua mbele ya Tume. Mara nyingi unakuta mwajiri ana sababu za msingi za kumwachisha mfanyakazi ajira lakini anakosa maarifa ya utaratibu wa haki, hivyo kuangukia kwenye adhabu mbele ya Tume endapo itaona mchakato haukuwa sawa. Ni muhimu kwa waajiri kutafuta ushauri wa kisheria kwa wataalam wa sheria za kazi ili kuepuka makosa hayo.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.