Hifadhi kwa Haki na Wajibu
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Mipaka ya Haki na Uhuru. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya wajibu wa kila mwanajamii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.
Maana ya Hifadhi kwa Haki na Wajibu
Katiba ya JMT inaeleza juu ya hifadhi juu ya haki na wajibu wa raia kama inavyoonekana katika Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya JMT inaeleza
‘Mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika Sehemu hii ya Sura hii ya Sura hii katika sheria yoyote inayohusu haki yake au wajibu kwake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote popote katika Jamhuri ya Muungano, anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu’
Ufafanuzi
Hifadhi juu ya haki na wajibu wa raia itakuwa juu ya Mahakama Kuu. Mahakama Kuu imepewa madaraka na Katiba ya kuangalia jinsi haki na wajibu wa raia unavyopaswa kutekelezwa. Mtu yeyote akiona haki yake na uhuru wake wa kikatiba unavunjwa basi anapaswa kufungua shauri Mahakama Kuu.
Mahakama Kuu itakuwa na mamlaka ya kusikiliza kwa mara ya kwanza na kuamua shauri lolote lililoletwa mbele yake kwa kufuata ibara hii. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 30 (4) ya Katiba ya JMT.
Kwamba mamlaka za Nchi zinaweza kuweka sheria kwa ajili ya;
- Kusimamia utaratibu wa kufungua mashauri kwa mujibu wa ibara hii
- Kufafanua uwezo wa Mahakama Kuu katika kusikiliza mashauri yaliyofunguliwa chini ya ibara hii;
- Kuhakikisha utekelezaji bira wa madaraka ya Mahakama Kuu, hifadhi na kutilia nguvu haki, uhuru na wajibu kwa mujibu wa Katiba hii.
Katiba inaeleza juu ya mamlaka ya Mahakama Kuu endapo kuna sheria ipo kinyume na katiba basi itatamka hivyo na kutoa fursa kwa Serikali kufanya marekebisho husika.
Hitimisho
Haki inatafutwa Mahakamani si mahali pengine. Tuna wajibu wa kufuatilia sheria na kufahamu mchakato mzima juu ya haki zetu zinapokiukwa na kuchukua hatua stahiki. Mahakama ndio chombo pekee kilichopewa wajibu wa kutafsiri sheria na Katiba na kuhakikisha haki za watu zinatimizwa na wajibu wa kila mmoja unasimamiwa.
‘Haki ikivunjwa au kutishiwa kuvunjwa hutafutwa mahakamani si mahali pengine popote’
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili