19. Kigezo cha Kuzingatia Vipengele vya Mkataba katika kusitisha Ajira
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tuliangalia kigezo cha Utaratibu wa Haki katika kusitisha ajira kihalali. Katika makala ya leo tunaangalia kigezo kingine cha Kuzingatia Vipengele vya Mkataba. Karibu tujifunze.
Maana ya Vipengele vya Mkataba
Mahusiano ya kiajira ni mahusiano ya kimkataba, yaani makubaliano baina ya pande mbili, mfanyakazi na mwajiri. Sehemu kubwa ya mkataba wa pande mbili ni kutokana na maelewano binafsi kuliko matakwa ya kisheria.
Mikataba mingi ya kiajira inaanisha maswala ya majukumu, nidhamu, maslahi ya kipato, muda wa kazi, stahiki za kisheria kama likizo, na pia inazungumzia namna mbali mbali za usitishaji wa ajira. Ipo mikataba ambayo inaenda mbali zaidi na kuanisha haki na wajibu wa pande zote mbili endapo kutakuwa na usitishaji wa ajira ni nini pande hizo zinastahili.
Wakati wa usitishaji wa ajira, zipo haki ambazo zimeainishwa kwenye mkataba baina ya mwajiri na mfanyakazi endapo kutatokea suala la usitishaji wa ajira. Mwajiri ni lazima ahakikishe haki hizo zinazingatiwa na kutekelezwa kikamilifu.
Sheria ya Ajira inaongoza kuwa masharti ya kuzingatia vipengele vya mkataba yatategemea aina ya mkataba ambao pande mbili zimeingia ikiwa ni mkataba wa kudumu au mkataba wa kipindi maalum.
- Masharti ya mkataba wa kipindi maalum
- Mwajiri ataweza kusitisha ajira ya mfanyakazi wa mkataba wa kipindi maalum endapo tu mfanyakazi atakuwa amevunja masharti makuu ya mkataba husika.
Ufafanuzi
Kama mfanyakazi ana mkataba wa miaka 3, mwajiri haruhusiwi kusitisha ajira kabla ya muda huo kumalizika, mpaka kuwe na sababu za msingi ambazo mfanyakazi amekiuka mkataba wake kiasi kwamba mwajiri hawezi kuvumilia kusubiri kipindi husika. Mfano mfanyakazi ametoroka kazini kwa muda mrefu bila taarifa, ameharibu mali ya mwajiri, amekosa uwezo wa kutimiza majukumu yake katika kiwango kinachotakiwa. Sababu ya kuvunjwa mkataba lazima itokane na makosa au upungufu wa mfanyakazi.
- Ikiwa mfanyakazi hajavunja masharti makuu ya mkataba husika, basi ili mwajiri aweze kusitisha ajira kabla ya kipindi kumalizika anapaswa kufanya mazungumzo na mfanyakazi ili asitishe ajira mapema kabla ya kipindi chake.
Ufafanuzi
Yapo mazingira yanaweza kusababisha mwajiri kutaka kusitisha ajira ya mfanyakazi kabla ya muda kumalizika. Mfano mkataba wa miaka 3 unaweza kusitishwa kutokana na sababu za mwajiri, kama akishindwa kulipa mishahara, au amepoteza biashara, au mfanyakazi huyo haitajiki katika mfumo mpya wa mwajiri. Katika mazingira haya kwa kuwa si mfanyakazi aliye na upungufu au makosa, mwajiri anawajibika kuingia kwenye meza ya mazungumzo na mfanyakazi ili wakubaliane usitishaji wa ajira kabla ya muda.
- Masharti ya mkataba wa kudumu
- Endapo mkataba baina ya pande mbili ni ule wa kudumu yaani mkataba unaoisha katika kipindi cha kustaafu, basi mwajiri akitaka kusitisha ajira kabla ya muda huo ni lazima awe na sababu halali na kufuata utaratibu wa haki.
Ufafanuzi
Katika makala zilizopita tuliangalia sababu za halali na utaratibu wa haki ambao mwajiri anapaswa kuuzingatia endapo anasitisha ajira. Hivyo ikiwa ni mkataba wa kudumu ni lazima pande zote zizingatie masharti ya kisheria katika kuhakikisha haki inatendeka. Mwajiri hawezi kuingia makubaliano ya kusitisha ajira kama ni mkataba wa kudumu, ni lazima awe na sababu na afuate utatatibu mahsusi kwa sababu hizo.
Katika suala la usitishaji wa ajira, mwajiri anaweza kusitisha ajira kwa kutoa notisi au pasipo kutoa notisi endapo mfanyakazi atakuwa amekiuka masharti ya msingi ya mkataba wa kazi.
Hitimisho
Masharti ya kimkataba ni sehemu ya msingi sana ya kuifahamu kwa pande zote mbili. Wafanyakazi wengi wamekuwa wepesi kuisaini mikataba pasipo kuisoma kwa makini ni kitu gani kipo ndani yake endapo ajira itasitishwa baadae, wanakuja kulalamika baada ya muda mrefu kwa kutokujua yale ambayo walikubaliana. Ni muhimu kwa pande zote kupata muda kabla ya kuingia makubaliano ya kiajira kupata ushauri kwa wataalam juu ya masharti ya kimkataba na athari zake katika mahusiano yao.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili.