Nifanye Nini wakati wa Kununua Ardhi?
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kujibu moja ya changamoto inayowakuta watu wengi wanapoamua kununua eneo/ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Karibu tujifunze.
Biashara ya Ardhi
Kama tunavyofahamu kuwa ardhi ni mali ya umma na inamilikiwa na Jamhuri chini ya udhamini wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Tunafahamu kuwa shughuli zote ya binadamu zinategemea ardhi iwe biashara, makazi, viwanda au shughuli za kilimo.
Vizazi na vizazi ardhi hii imekuwepo na watu wameendelea kubadilishana kwa njia mbali mbali ikiwa pamoja na kuuza, kurithi au kupewa n.k. Hatahivyo kutokana na shughuli za kibinadamu na maendeleo maeneno mbalimbali ardhi imekuwa inapanda thamani na kubadilishana umiliki kila kukicha. Biashara hii imekuwa kubwa kiasi kwamba hali ya watu kutokuwa waaminifu katika masuala la kuuza na kununua ardhi yameibua migogoro mingi na watu wengi kutapeliwa.
Kama biashara nyingine yoyote, mauzo na manunuzi ya ardhi yana mchakato na mambo ya msingi ya kuzingatia ili kuepuka hasara na udanganyifu.
Makala hii inakwenda kujadili baadhi ya mambo ya msingi ya kuzingatia endapo unakusudia kukunua ardhi kwa matumizi yako binafsi au makazi au shughuli za kilimo.
Kanuni za msingi za kuzingatia
Kanuni ya msingi sana katika manunuzi yoyote inamtaka Mnunuzi kuwa na umakini wa hali ya juu kabla ya kuingia kwenye manunuzi asije kupata hasara. Kwa lugha ya kigeni inasema ‘Buyer be aware’. Mnunuzi anawajibika kuwa na taarifa zote za msingi kabla ya kuchukua uamuzi wa kununua ardhi.
- Mnunuzi jiridhishe juu ya matumizi ya ardhi husika
Watu wengi wanakimbia haraka baada ya kutajiwa bei ya ardhi na kuona wanaimuda na kuamua kununua pasipo kuchukua hatua za kujiridhisha juu ya matumizi ya ardhi. Katika makala Sheria Leo.34: Mgawanyo wa Makundi ya Ardhi na Sheria Leo.35: Je, Unazijua Ardhi za Hifadhi? nilizungumzia juu ya makundi ya Ardhi na hasa ardhi ya Hifadhi. Ni jukumu lako mnunuzi kuhakikisha kuwa una ufahamu endapo matumizi ambayo unakusudia kufanya kwenye ardhi husika yanaruhusiwa eneo hilo. Wengi wameingia kwenye mtego wa kupewa taarifa za uongo na kwa kuona kuwa ipo nyumba au kuna shughuli inaendelea kumbe eneo hilo linaweza kuwa ni hifadhi ya barabara au tayari mmiliki alishalipwa fidia na Serikali ina matumizi mengine.
Unaweze kupata taarifa husika kupitia mamlaka zilizopo katia mji kama Halmashauri za miji na Manispaa mbali mbali au kupitia msajili wa hati endapo eneo husika lina hati ya umiliki.
- Mnunuzi jiridhishe juu ya umiliki wa ardhi unayotaka kununua
Hili ni jambo muhimu sana pia kwani wengi wa wanunuzi wanauziwa na watu ambao si wamiliki halali. Wapo watu wanaweza kueleza na kuleta nyaraka kudhibitisha juu ya umiliki wake lakini si kweli. Kisheria manunuzi kwa mtu asiye mmiliki si halali na mnunuzi anapata hasara ya kutapeliwa. Mnunuzi fanya kazi yako vizuri, hakikisha unayenunua kwake ni mmiliki halali kwa wakati huo unaonunua. Wapo watu wasio waaminifu wanauza eneo moja kwa watu zaidi ya mmoja na kusababisha migogoro isiyoisha.
Kudhibitisha uhalali wa umiliki, hakikisha unafanya utafiti kwa msajili wa hati kwenye wizara ya Ardhi endapo ardhi hiyo imesajiliwa. Kama ardhi haijasajiliwa unaweza kufanya utafiti kupitia majirani au nyaraka nyingine zozote ambazo unaweza kuzidai kutoka kwa muuzaji. Muhimu mambo ya kununua hayahitaji haraka bali ufanye uamuzi ambao una uhakika kuwa hupati hasara, mara nyingi watu wanapoteza kutokana na kuwa na haraka.
- Mnunuzi hakikisha unafahamu ikiwa ardhi hiyo imesajiliwa kwa kuwa na hati/leseni au haijasajiliwa.
Eneo kubwa la ardhi ya Tanzania bado haijasajiliwa yaani hazina hati miliki. Serikali inafanya jitihada ya kuhakikisha ardhi hasa za kwenye miji zinapata usajili. Hivyo watu wengi wanamiliki ardhi kwa njia za kimila hata zikiwa kwenye miji. Kupata taarifa hizi zinaweza kukusadia hasa kwa zile ambazo hazijasajiliwa kwani inawezekana ardhi ikawa inamilikiwa na zaidi ya mtu mmoja anayetaka kukuuzia. Matatizo mengi yanajitokeza hasa pale ardhi husika ni matokeo ya urithi ndipo warithi wanataka kuuza huku wengine wakiwa kwenye mgongano. Mnunuzi unapaswa kujihakikishia kuwa anayeuza au wanaouza ni wamiliki halali au wana haki zote za kufanya mauzo hayo pasipo baadae kuibuka migogoro juu ya uhalali wa mauziano.
- Mnunuzi jiridhishe iwapo ardhi husika haijawekwa rehani
Watu wengi pia wamekuwa si waaminifu katika kutoa taarifa juu ya ardhi wanazouza endapo zimewekwa rehani kutokana na mikopo. Ni kazi yako mnunuzi kutafuta taarifa sahihi na kuuliza maswali ya msingi endapo ardhi husika inahusishwa kama rehani mahali popote pale. Kumeibuka utapeli mkubwa sana nyakati hizi watu wanachukua mikopo kwenye vyombo mbali mbali vya fedha na kisha kuuza ardhi kwa watu wengine. Hakikisha kabla ya kununua una taarifa hizo za msingi.
- Mnunuzi hakikisha manunuzi yanafanyika kwenye mkataba wa maandishi na mashahidi muhimu.
Hili ni jambo la muhimu kabisa kwa mnunuzi kuhakikisha unaandaa mkataba wa maandishi. Usimwamini muuzaji yoyote kwa maneno kuwa eneo ni lake pasipo kuandika na kuwa na mashahidi muhimu. Kuhusu mashahidi endapo unauziwa na mtu mwenye ndoa hakikisha mwenzi wake anahusika na ametoa kibali cha mauziano hayo, pia upate walau majirani wa mipaka ya eneo unalonunua wajue na kushuhudia umenunua kwenye mkataba husika.
Hitimisho
Yapo mambo mengi ya kuzingatia wakati wa ununuzi wa ardhi ambayo mnunuzi anapaswa kuzingatia. Hali ya uaminifu imeondoka miungoni mwa watu hivyo kabla hujapata hasara na kuingizwa kwenye migogoro ya ardhi jihakikishia mambo hayo ya msingi.
Nikushauri ndugu yangu kutafuta ushauri wa kisheria kwa wanasheria kabla hujachukua maamuzi ya kununua na endapo utafikia maamuzi ya kununua mwanasheria anaweza kukuandalia mkataba wenye manufaa kwako endapo itajulikana taarifa ulizopewa hazikuwa sahihi na hapo utakuwa na uwezo wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mhalifu husika.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili
Naomba msaada kuna mama ameniuzia kiwanja tangu March 2012 document ya uthibitisho ipo lkn 2017 aliingia tamaa akauza kwa mtu mwingine bila ridhaa yangu na yeye akakiri kuwa ameuza ila nimpe muda amalizane na mtu aliyemuuzia ndipo anikabidhi eneo langu. Je nifanye nini now? Na kama itatokea aliyeuziwa kashapatiwa hati miliki nawezaje kurudisha eneo langu
Karibu sana ndugu Robert nilijibu maswali yako kupitia e-mail nadhani ulipata kitu cha kukusaidia kwenye changamoto hii
Sheria inasemaje! Bibiyangu alitoa sehem yashamba lake kwa taasisi ya dini wajenge msikiti buree pasina kutoa hata sent yaani buree ila hapakuwa namaandishi yamakabidhiano wala mashahidi mudaulivyo enda taasisi wanataka kudhulum sehem yote yashamba iliyobaki wakidai huyo bibi amewauzia.na bibi amekataa kwamba hajauza nakutokana na usumbufu wa wanataasisi bibi anataka kudai hadiilesehem aliyo wapa kama sadaka je kisheria inawezekana?naikumbukwe hawana mkatabawamauziano
Karibu sana ndugu yetu Abdulrasul Mustafa
Awali ya yote niombe radhi kwa kuchelewa kuleta majibu ndani ya wakati kutokana na changamoto zilizotukuta kwenye mtandao wetu.
Ni kweli sheria za kiislam zinaruhusu muumini kutoa sehemu ya ardhi au mali yake kuwa ‘Wakf’ kwa ajili ya matumizi ya Taasisi ya Kidini. hatahivyo, ni vyema na sheria inashauri kuwa utoaji huo ufanyike kwa maandishi. katika swali lako juu ya endapo waliopewa wanaweza kuchukua sehemu yote, ni dhahiri hilo haliwezekani maadamu aliyetoa bado yupo hai basi busara itumike wafanye kwa maandishi. Sidhani kama itakuwa jambo la busara kwa bibi kurudisha ardhi yote kwa sababu tu hawakuandikiana, naamini alitoa kwa nia njema ingawa nia hiyo ilitaka kutumiwa vibaya. nashauri waonwe viongozi wengine wa dini mbali na wa eneo hilo wanaweza kusuluhisha jambo hilo na kuisha kwa heri kwa pande zote.
Asante sana na karibu tena