Nifanye Nini wakati wa Kuuza Ardhi?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.makala iliyopita tuliangalia juu ya mambo ya msingi kuzingatia wakati wa kununua eneo/ardhi. Leo tunakwenda kujibu moja ya changamoto inayowakuta watu wengi wanapoamua kuuza eneo/ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Karibu tujifunze.

Biashara ya Ardhi

Katika biashara ya aina yoyote zipo pande mbili yaani muuzaji na mnunuzi. Halikadhalika kwenye mauzo ya ardhi yupo anayeuza na anayenunua. Makala iliyopita tulizungumza mambo ya msingi kwa mnunuzi kuyazingatia ili aweze kununua ardhi kihalali na kuepusha migogoro ya baadae.

Hatahivyo yapo mambo ya msingi pia kwa ajili ya muuzaji anayopaswa kuzingatia ili kuhakikisha biashara hiyo inakamilika na haileti mgogoro wa ardhi hapo baadae. Katika makala hii tunakwenda kuangalia baadhi ya mambo hayo anayopaswa kuzingatia.

Kanuni za msingi za kuzingatia

  1. Muuzaji hakikisha kuwa eneo/ardhi unayotaka kuuza ni mali yako kihalali

Kanuni ya msingi sana katika uuzaji wa eneo/ardhi yoyote inamtaka muuzaji awe mmiliki halali wa eneo. Kanuni hii ya kisheria inaeleza kuwa huwezi kuwa na haki ya kuuza kitu wakati huna haki ya kukimiliki. Mauzo yoyote utakayofanya kwa mali ambayo si yako kihalali yatahesabika kuwa batili na kukusababishia matatizo ya kisheria. Wengi wa watu wanaweza kukaa katika eneo hata jamii ya watu inayowazunguka ikajenga dhana kuwa eneo hilo ni lao wakati si kweli. Ni muhimu kuwa mwaminifu katika biashara hii kwani ukweli utajulikana tu kama mali ni yako au si yako. Ikiwa mali inamilikiwa na zaidi ya muuzaji mmoja basi hakikisha wengine wanaufahamu juu ya mauzo hayo na ikiwezekana watoe kibali cha maandishi kuridhia uuzwaji huo.

  1. Muuzaji hakikisha eneo lako halijawekwa rehani kwa dai lolote

Wauzaji wengine wanakosa uaminifu na kufanya biashara ya kuuza eneo wakati wameweka rehani kutokana na mikopo au dai lingine lolote. Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha kabla hujauza eneo lako huna madeni yanayoambatanishwa na eneo hilo. Kama eneo lako limewekwa rehani ni dhahiri utaibua mgogoro na wadeni wako pamoja na yule uliyemuuzia. Gharama utakayoingia katika migogoro ya kisheria ni kubwa sana kuliko kiwango cha fedha ambacho ungepata kutokana na mauzo hayo.

  1. Muuzaji usiuze eneo/ardhi ambayo ipo katika mgogoro mbele ya vyombo vya sheria

Hii imekuwa tabia ya baadhi ya wauzaji wasio waaminifu anauza eneo huku akijua kuwa eneo lake lina mgogoro mahakamani. Tabia hii imezalisha migogoro mingi ya ardhi mara baada ya wanunuzi kukuta kuwa aliyewauzia tayari ameshapoteza haki ya umiliki wa eneo husika. Ni vyema kusubiri hatua zote za mgogoro kumalizika ndipo uweze kuuza. Hapa tunazungumzia mgogoro ulio mbele ya vyombo vya maamuzi juu ya masuala ya ardhi na si migogoro au kupishana kwa maneno juu ya majirani. Lazima uwe mgogoro ambao upo mahakamani.

  1. Muuzaji kabla ya kuuza hakiki mipaka yako na majirani

Hili ni jambo la msingi sana kwa muuzaji kulifanya kabla ya kuuza eneo lake. Wauzaji wengi hawatambui mipaka yao au kuhakiki kabla ya kuuza. Ni vyema ukamtambulisha mnunuzi kwa majirani ambao unapakana nao ili kumsaidia kujua mwisho wa eneo lake asije kubugudhi majirani au yeye kupata bugudha baada ya wewe unayeuza kumaliza kuuza. Migogoro mingi juu ya ardhi inasababishwa na kutotambuliwa mipaka halali ya eneo la mtu. Kuepusha migogoro hii weka alama za kudumu katika mipaka yako na wakati unauza hakikisha majirani wana taarifa na mipaka yako imetambuliwa na kuheshimiwa.

  1. Muuzaji hakikisha umelipia kodi za serikali kabla ya kuuza

Kama tunavyofahamu ardhi ni mali ya umma katika nchi yetu ya Tanzania. Hivyo kila anayemiliki ardhi anapewa kipindi au haki ya matumizi ya ardhi ile na kuna kodi inapaswa kulipwa Serikalini. Muuzaji unawajibika kuhakikisha unalipa kodi za Serikali kama zilivyoainishwa na mamlaka husika ya eneo hilo. Kutokulipa kodi za Serikali kunaweza kusababisha mauzo hayo kubatilishwa na kumwingiza mnunuzi kwenye hasara ambayo haikutarajiwa.

  1. Muuzaji hakikisha unapata ridhaa ya mwenzi katika kuuza eneo/ardhi

Endapo muuzaji ni mwanandoa au anamiliki eneo hilo kwa ubia na mtu mwengine hakikisha anayo taarifa na anatoa kibali husika. Mali au ardhi ikiwa ya pamoja mwezi ana haki ya kupata taarifa juu ya uuzaji huo na kutoa kibali cha uuzaji huo. Usifanye mauzo kwa kificho kumficha mwenzi wako kwani madhara yatakayojitokeza yanaweza kuibua mgogoro na mwenzi pamoja na aliyeuziwa na kusababisha hasara baadae.

 

Hitimisho

Yapo mambo mengi ya kuzingatia wakati wa uuzaji wa ardhi ambayo muuzaji anapaswa kuzingatia. Muhimu katika yote ni lazima muuzaji ajenga hali ya kuaminika na yule anayemuuzia, usiuze tu kwa tamaa ya fedha kwani kupata fedha zisizo za halali baada ya muda kunaweza kukuletea madhara katika maisha yako ya kila siku na kujikuta unaingia kwenye migogoro ya ardhi na hata kutenda kosa la jinai.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili