21. Usitishaji wa Ajira wa Kujiuzulu kwa Lazima

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Katika makala ya Uchambuzi wa Sheria.15. Aina za Usitishaji Ajira Kihalali tulizungumzia Aina za Usitishaji wa Ajira Kihalali. Mojawapo ya usitushaji huo ni ule unaofanywa na mfanyakazi. Leo tunakwenda kuangalia mazingira ambayo mfanyakazi anaweza kusitisha ajira kwa kujiuzulu kwa lazima. Karibu tujifunze.

Usitishaji Halali wa Ajira

Kama tulivyoandika katika makala zilizopita kuwa zipo aina mbalimbali za usitishaji wa ajira. Mfano usitishaji wa ajira kulingana na kumalizika kwa mkataba, au usitishaji unaotokana na kifo au usitishaji unaofanywa na mfanyakazi na ule unaofanywa na mwajiri.

Usitishaji wa ajira unaofanywa na mfanyakazi

Mfanyakazi kama ilivyo kwa mwajiri anayo haki ya kusitisha ajira wakati wowote kama ataona inafaa kwa mujibu wa mkataba wake na sheria za kazi. Mfanyakazi anawajibika kutoa taarifa kwa mwajiri wake, endapo anakusudia kusitisha ajira kabla ya muda wa mkataba kumalizika au kabla ya kustaafu. Kusitisha huku ajira kunaitwa kujiuzulu kazi.

Mara nyingi katika kujiuzulu kazi kwa mfanyakazi kunahesabiwa kuwa ni jambo la hiyari na halitarajiwi baada ya muda kuibua mingongano baina ya pande mbili kwani inaonekana kuwa limefanyika kwa hiyari.

Hatahivyo, sheria inatambua kuwa yapo mazingira yanayoweza kuwa yametengenezwa na mwajiri au eneo la kazi na kusababisha mfanyakazi kulazimika kujiuzulu. Kujiuzulu huku kwa mfanyakazi kutokana na mazingira ya kazi au uhusiano ulioharibika baina yake na mwajiri au wafanyakazi wengine hakuwi hiyari yake bali analazimika. Hivyo sheria ya Ajira inaweka bayana mazingira haya na namna ambavyo yanaweza kushughulikiwa kisheria ili mfanyakazi asipoteze haki zake.

Mathalani unaweza kukuta mfanyakazi anafanya kazi zake vizuri kwa muda mrefu, mara baada ya kiongozi mpya wa kazi kuingia inawezekana kiongozi yule hana uhusiano mzuri na mfanyakazi yule ingawa kazi zake zinafanyika vizuri, anaamua kutengeneza mazingira magumu ya mfanyakazi ili aamue mwenyewe kuomba kujiuzulu au kutishiwa ajiuzulu badala ya kufukuzwa. Wengi wa wafanyakazi wanaangukia katika mtego huu wanaamua heri kujiuzulu ili upate chochote kuliko kusubiri kufukuzwa kwa sababu yoyote ile itakayoonekana inafaa.

Mazingira yanoyoweza kusababisha kujiuzulu kwa lazima

Sheria ya Ajira inaonesha kuwa yapo mazingira ambayo inayatambua yanasababishwa na mwajiri au wafanyakazi wengine ambayo yanaweza kupelekea mfanyakazi kujiuzulu kazi. Usitishaji huu wa ajira kwa mfanyakazi unajulikana kama Kujiuzulu kwa Lazima au kwa kiingereza ‘Constructive termination’ au ‘Forced resignation’ yaani kuacha kazi kutokana na mazingira yaliyotengenezwa au kulazimishwa dhidi ya mfanyakazi.

  1. Unyanyasaji wa kijinsia kwa mfanyakazi au kushindwa kuzuia unyanyasaji wa kijinsia mahali pa kazi.

Nyakati hizi kumekuwa na vitendo vingi vya unyanyasaji hasa kwa wanawake, ingawa haimaanishi kuwa wanaume nao hawanyanyaswi. Wengi wa waajiri wamejihusisha na kuwataka kingono wafanyakazi wao na imekuwa shida kubwa pale mfanyakazi anapokataa visa vinaibuka na matishio ya kufukuzwa kazi. Hatimaye mfanyakazi anakosa utulivu wa maisha yake binafsi na mustakabali wa ajira yake unakuwa mashakani. Wengine wanaingia katika mtego huo na kuwa wahanga wa waajiri wao au viongozi wa eneo la kazi lakini wengine wanaamua kujiuzulu kazi.

Katika mazingira haya kwa sura ya nje unaweza kuona ni mfanyakazi mwenyewe ameacha kazi ingawa kuna sababu nyingine ndani yake ambayo ndiyo ilimsukuma kujiuzulu yaani kulinda heshima ya utu wake kwa kukataa kufanya mambo yaliyo kinyume na maadili.

 

  1. Uonevu kwa mfanyakazi pasipo sababu zozote.

Eneo la kazi pia limegubikwa na hali za uonevu kwa baadhi ya wafanyakazi huku wengine wakioneshwa upendeleo dhahiri. Sheria ya Ajira inaeleza juu ya uonevu mahali pa kazi unaweza kusababisha mfanyakazi akachukua hatua ya kujiuzulu kazi. Zipo namna mbalimbali ambazo waajiri au viongozi wa kazi wanatumia kuwaonea wafanyakazi, kwa mfano kuwanyima muda wa kupata chakula, kuwanyang’anya vifaa vya kazi, kuwagombeza pasipo sababu, kuwapa adhabu pasipo kuwa na kosa, kuwakata mishahara au posho pasipo maelezo yoyote na vitendo vingine vingi. Nia hii ya uonevu mahali pa kazi ni kumsababishia mfanyakazi msongo wa mawazo ashindwe kutekeleza majukumu yake na hatimaye aamue kujiuzulu.

 

Hatua za kisheria dhidi ya kujiuzulu kwa lazima

Wafanyakazi wengi wanaokuwa wameacha kazi kwa kujiuzulu kwa lazima wanapoteza haki zao kwa kudhani kuwa kwa sababu ni wao wameandika barua ya kuacha kazi hawawezi kupata haki zao mbele ya chombo cha kisheria.

Mfanyakazi ambaye amejiuzulu kazi kutokana na mazingira ambayo yameainishwa kwenye sheria hapo juu anayo haki ya kufungua shauri la mgogoro wa ajira na kuomba Tume itamke kuwa amesitishiwa ajira yake na mwajiri kutokana na mwajiri kusababisha mazingira ya kazi kutovumilika kwa upande wake. Muhimu aweze kudhibitisha madai yake mbele ya Tume na ikidhibitika, mfanyakazi atapata stahili zake zote kwa mujibu wa sheria kama mtu aliyeachishwa kazi isivyo halali.

Hitimisho

Usitishaji wa ajira kwa njia ya kujiuzulu kwa mfanyakazi kunaweza kuwa kumetokana na hiyari yake au kulazimishwa kwa mazingira au vitisho vinavyotolewa mahali pa kazi. Muhimu kwa waajiri na wafanyakazi kufahamu kuwa kinachowakutanisha mahali pa kazi ni ile kazi waliyokubaliana ifanyike kwa mujibu wa mkataba na si vinginevyo. Waajiri waache kunyanyasa wafanyakazi na kutaka kupata faida isiyo haki pia wafanyakazi wafanye kazi na si kujiwekea mazingira ya kujenga mahusiano na waajiri au viongozi wa kazi wapate upendeleo. Kila mmoja akitimiza wajibu wake kulingana na taaluma, uwezo na bidii, mabadiliko, ufanisi na tija mahali pa kazi vitaonekana.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.