Jinsi ya kuepusha Mgogoro wa Mipaka katika Ardhi?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu  kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kujibu moja ya changamoto zinazowakuta wamiliki wa ardhi katika matatizo ya mpaka. Karibu tujifunze.

Nini maana ya Mpaka

Mpaka ni alama zinazoonesha eneo la umiliki wa mtu katika ardhi. Mpaka unatofautisha eneo moja na mengine juu ya umiliki wake.

Katika masuala ya ardhi na umiliki wake, suala la mipaka limekuwa linaleta changamoto kubwa na kuibua migogoro kila kukicha. Mizozo ya mipaka haishii tu kwa watu binafsi bali linakwenda hata ngazi za kimatifa. Tumekuwa tukisikia mara kwa mara nchi kadhaa zimekuwa na mgogoro wa mipaka. Hivyo suala la mipaka ni suala nyeti katika kuhakikisha jamii inakaa kwa amani na utulivu wakati wote.

Katika makala hii ya leo tunakwenda kuangalia mambo ya msingi ambayo yataweza kukusaidia mmiliki wa ardhi kuyafanya ili kuepusha migogoro ya mipaka inayoibuka kila siku.

Mambo ya msingi ya kuzingatia

  1. Mmiliki wa ardhi tambua hakuna ardhi/eneo lisilo na mipaka

Hili ni jambo la msingi sana kwa mmiliki kulifahamu mara anapomiliki eneo lolote ikiwa ni kwa kupewa au kununua. Kwa jinsi nchi ilivyo na mipaka kadhalika kila eneo ndani ya nchi husika lina mipaka yake. Hivyo unapomiliki au kumilikishwa eneo fulani hakikisha unauliza juu ya mipaka ya eneo na unaitambua.

  1. Mmiliki wa ardhi tambua mipaka ipo sehemu kuu nne.

Mipaka ya eneo kwa kawaida imegawanyika katika sehemu kuu nne ambazo ni pande za dunia. Katika kiwanja chochote ni lazima angalau kita kuwa na mipaka sehemu nne yaani mpaka wa mashariki, mpaka wa magharibi, mpaka wa kaskazini na mpaka wa kusini. Hivyo mmiliki hakikisha eneo lako unalikagua na kuifahamu mipaka hiyo kwa hakika pasipo kuwa na mashaka. Wengi wanamiliki maeneo lakini hawatilii maanani juu ya mipaka yao. Unakuta mtu anasema eneo langu linapakana na barabara au mto au shamba la mtu fulani. Wengi hawana ufahamu wa mipaka yote ya sehemu nne inayozunguka eneo lake.

  1. Fanya vipimo vya eneo lako hata kama halijapimwa na Serikali

Hili ni jambo muhimu sana kwa mmiliki wa eneo kulifanya. Kama tulivyoeleza katika makala zilizopita kuwa ardhi kubwa katika nchi hii bado haijapimwa, hii haimaanishi ardhi hiyo haimilikiwi na watu. Wapo watu wanamiliki maeneo makubwa sana zaidi ya hekari 1,000 wanachukua wajibu wa kupima maeneo yao, lakini watu wengine hawana hata robo ekari hawajui vipimo vya eneo lao. Wengi wanabaki kusema ‘ kinapoishia kiwanja cha fulani ndio changu kinaanzia hapo’ huu ni ukosefu wa umakini na unaweza kusababisha migogoro ya mipaka baadae endapo mmoja wapo atauza eneo lake au kurithisha au kuamua kuingilia eneo la mwingine. Siku hizi kufanya vipimo ni jambo rahisi sana unaweza kufanya hata mwenyewe kwa kununua kipimo cha mita na kupima. Kuna dhana ya vipimo ambayo inatumiwa na watu wengi kudhani ni vipimo sahihi wanasema labda kiwanja ni ‘miguu 20 kwa miguu 20’ huu mfumo ni wa zamani sana wakati hapakuwa na uwezo wa kupima maeneo kwa vifaa vya kisasa. Changamoto itakuja miguu hiyo ya kupima ni ya nani na ni kwa hatua zipi zitadhibitisha ni mguu mmoja? Fanya maamuzi ya busara pata vipimo vya eneo lako.

  1. Tengeneza mchoro wa eneo lako

Jambo lingine la msingi linaloweza kutusaidia kulinda maeneo na kuhakikisha hakuibuki migogoro isiyo ya lazima ni kuwa na mchoro wa eneo lako. Kama nilivyotangulia kusema maeneo mengi bado hayajapimwa lakini haikuzuii mmiliki kutengeneza mchoro wa eneo lako ‘sketch map’ ramani ya kawaida na kunesha vipimo ambavyo umevipima katika eneo husika. Hii itakusaidia kuwa na kumbukumbu sahihi mara mgogoro unapoweza kuibuka katika eneo lako na kuwasaidia wengine wenye haki katika eneo hilo.

  1. Weka alama za kudumu kwenye mipaka yako

Umuhimu wa mipaka ni kuhakikisha umeweka eneo hilo mipaka sahihi na alama za kudumu. Wengi wanaamini kuwa mipaka inatambuliwa na majirani zao lakini siku hizi watu wamepoteza uaminifu na wamekuwa wakijimegea mipaka ya majirani zao mara kwa mara pasipo wengine kujua. Usichukulie mtu mwengine atakuwa mwaminifu kama wewe, huwa wanaanza kidogo kidogo, anaweza kukuomba kuweka vitu kwenye eneo lako au akapanda mazao yasiyo ya kudumu kisha akapanda na miti akisema matunda mtakula wote n.k hizo zote ni mbinu za kuongeza mpaka wa eneo lake. Hivyo chukua taadhari mapema na uweke mipaka yako katika eneo husika ili yasije yakajitokeza mambo ya kuibua migogoro pasipo na sababu za msingi. Unaweza kuweka mipaka ya kudumu kwa kupanda miti kuzunguka eneo, au kuweka nguzo za zege au kuweka ukuta n.k.

  1. Tambua na jenga uhusiano mzuri na majirani unaopakana nao

Hili ni jambo la msingi lingine ambalo hupaswi kulikosa. Ni muhimu sana kwa mmiliki kufahamu majirani zake ambao wanaopakana naye ili kujenga uhusiano mwema. Kufahamiana na majirani zako wanaweza kukusaidia kulinda eneo lako na mipaka yako endapo kutajitokeza tatizo lolote. Ni muhimu sana kuwafahamu watu wanaokuzunguka katika eneo lako ili kusadia hatma ya eneo lako na umiliki wako kutokuingiliwa na mvamizi au jirani yako.

 

Hitimisho

Mipaka katika eneo ndio msingi wa umiliki wa eneo la mtu. Hakikisha unafahamu mipaka yako na unailinda ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Kwa kuwa maeneo mengi hayajapata kupimwa ni muhimu kuchukua hatua nilizokueleza katika makala hii lakini pia hakikisha unaanzisha mchakato wa upimaji wa eneo lako ikiwa ni kwa makazi au shamba au shughuli zozote ili upate hati miliki ya Serikali ambapo utapata ulinzi zaidi wa eneo lako na kuongeza thamani katika eneo husika.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili

1 reply

Comments are closed.