Nini cha kufanya kuzuia uvamizi wa eneo langu?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kujibu mambo ya msingi ya kufanya ili kuzuia eneo lako lisivamiwe. Karibu tujifunze.

Maana ya Uvamizi wa Eneo/ Ardhi

Mvamizi wa eneo ni mtu ambaye anaingia katika eneo la mtu mwengine pasipo ridhaa ya mmiliki na kufanya shughuli zake mahali hapo kama kwake.

Katika siku za hivi karibuni uvamizi wa maeneo umekuwa ni changamoto kubwa sana ikiwa maeneo ya mjini au vijijini. Watu wanaongezeka kwa kasi kubwa na wanajenga makazi au kuanzisha shughuli holela maeneo ambayo si yao. Watu wanamiliki maeneo zaidi ya moja na mara kadhaa maeneo ambayo hayana uangalizi wa kutosha yana hatari ya kuvamiwa.

Tumekuwa tukisikia juu ya migogoro baina ya wafugaji na wakulima, watu kuvamia mashamba makubwa ya wamiliki n.k. hii ni tabia ambayo imeendelea kujengeka miungoni mwa jamii yetu na inapaswa kuona jinsi gani tunaweza kuipunguza au kuikomesha kabisa.

Leo tunakwenda kujadili mambo kadhaa ya msingi ambayo yanaweza kukusaidia mmiliki wa eneo/ardhi kuweka ulinzi au kuhakikisha eneo lako halivamiwi na wavamizi wa maeneo.

Mambo ya msingi ya kuzingatia

  1. Hakikisha umeweka alama za mipaka yako vizuri

Katika makala iliyopita tulijadili kwa kina hitaji muhimu kwa kila mmiliki juu ya mipaka ya eneo. Tuliangalia mambo ya msingi kukusaidia kuweka ulinzi madhubuti kupitia mipaka. Hivyo mipaka ya eneo ni jambo la msingi sana katika kuhakikisha eneo halivamiwi na wavamizi.

  1. Toa notisi kwa watu wote

Ikiwa unamiliki eneo kubwa au mbali na makazi yako kiasi ambacho hakuna shughuli za mara kwa mara zinazokulazimu kuwa katika eneo lako, basi njia moja wapo ni kuweka notisi juu ya umiliki wa eneo katika ardhi husika. Wengi wanaandika mabango katika maeneo yao na kuyajengea wakionesha taadhari kwa wananchi wote kuwa eneo hilo ni mali ya mtu au kampuni au taasisi fulani. Hii kwa kiasi kikubwa inasaidia kufukuza wavamizi na watu wasio waaminifu wanaouza maeneo ya watu.

  1. Anzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji katika eneo lako

Watu wengi wananunua au kumiliki maeneo makubwa na madogo lakini hawachukui hatua za kuanzisha shughuli za uzalishaji mahali hapo. Katika mazingira hayo eneo linaonekana ni pori na wavamizi wanaweza kuanza kulinyemelea na kuanzisha shughuli zao. Kinachowavuta wavamizi katika maeneo mbalimbali ni ukosefu wa shughuli katika maeneo husika. Kuzuia uvamizi weka mipango wakati wa kununua eneo na anza kuwekeza shughuli kidogo kidogo. Ikiwezekana unaweza kufanya kilimo au upandaji wa miti n.k. shughuli katika eneo zitakuvuta kuwa unatembelea mara kwa mara.

  1. Weka ratiba maalum ya kutembelea eneo lako

Mara kadhaa tumekuwa tukinunua na kumiliki maeneo mengi lakini hatuna muda wa kuyatembelea na kuhudumia. Wengi wananunua ardhi kwa lengo la kufanya biashara ya ardhi endapo thamani yake itaongezeka hapo baadae. Hii dhana inafanya watu kukosa msukumo wa kuwekeza shughuli za kufanya katika maeneo hayo na zaidi kukosa muda wa kutembelea mara kwa mara. Ni muhimu sana kupata muda wa kutembelea eneo lako kwani ni mali yako ya uwekezaji ukiiacha utaingia gharama kubwa endapo itavamiwa kutafuta namna ya kuikomboa.

  1. Weka ulinzi au usimamizi

Kwa watu wenye maeneo makubwa wanashauriwa kuweka mlinzi au msimamizi wa eneo. Mbinu hii inasaidia sana katika kuwa na mtu ambaye anawajibika kulitunza eneo na kuhakikisha halivamiwi kwa wakati wowote. Hatahivyo changamoto kwa siku hizi walinzi au wasimamizi wamekuwa si waaminifu wamegeuka na kuanza kuuza maeneo ambayo wamewekwa kusimamia. Muhimu kwa wamiliki kuwa na mbinu za kisheria za kuwabana wasimamizi hawa kwa kuwaandikia mkataba ikiwa ni mwajiriwa au mamlaka ya usimamizi wa eneo kwa mtu ambaye si mwajiriwa. Hakikisha taarifa za usimamizi au ulinzi wa mtu huyo zipo katika serikali ya Mtaa au kijiji. Muhimu zaidi wewe mmiliki kupata nafasi ya mara kwa mara kutembelea eneo lako na kuanzisha shughuli za uzalishaji au ujenzi wa nyumba za makazi kwa ajili ya kupangisha kutasaidia kulinda eneo lako.

Hitimisho

Wengi wetu tunatamani kuwa na maeneo mazuri na tunaingia gharama katika kuyanunua. Hatahivyo changamoto kubwa ni katika namna ya kuyatunza maeneo husika, tunaingia hali ya uzembe na kudhani kuwa yapo salama. Kumbuka ile ni fedha ambayo umeweka katika ardhi ni lazima ikuzalishie na kukufaa katika maisha ya baadae.

Pia katika kuweka usimamizi wa kieneo ikiwa ni kwa kumwajiri mlinzi au jirani yako katika eneo ambaye yupo umemkabidhi hakikisha unafanya kwa maandishi na serikali husika katika eneo iwe na taarifa usije ukapoteza mali yako. Wamiliki wanapaswa kuwa waaminifu kwa kuwalipa stahiki zao wale ambao wanalinda maeneo au wanaangalia isiwe inachukuliwa kama hisani tu ifanye kuwa ni wajibu wako kulipa na ikiwezekana tunza kumbukumbu za malipo hayo ili yakufae endepo muhusika ataingia nia ya kuuza eneo lako.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili