22. Usitishaji wa Ajira kwa Wafanyakazi katika kipindi cha Majaribio.

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Leo tunaangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa wafanyakazi walio katika kipindi cha majaribio. Karibu tujifunze.

Ajira na Kipindi cha Majaribio (Probation Period)

Sheria ya Ajira inatambua hitaji la mwajiri katika kumpima mfanyakazi endapo anakidhi viwango na vigezo vya kumwajiri moja kwa moja. Hivyo sheria inaruhusu kuwepo kwa kipindi cha majaribio (Probation Period).

Katika kipindi hiki mfanyakazi anakuwa ameajiriwa ingawa anawekwa chini ya unagalizi maalum kwa muda kutokana na kazi anazopaswa kuzifanya endapo atazimudu au la. Waajiri wanaweza kuamua ni kipindi au muda kiasi gani mfanyakazi anakuwa katika majaribio. Kipindi hiki kinaweza kuwa kuanzia mwezi mmoja au mitatu au miezi sita. Kipindi cha majaribio kwa kawaida hakipaswi kuzidi miezi 12.

Lengo la Kipindi cha Majaribio

Kama ilivyoanishwa katika Sheria ya Ajira kwamba lengo kuu la kumweka mfanyakazi katika kipindi cha majaribio ni kumsaidia mwajiri kufanya maamuzi sahihi kuhusu uwezo wa mfanyakazi katika kazi aliyopewa au la.

Mambo Muhimu ya Kuzingatia katika kipindi cha Majaribio

  • Lazima mfanyakazi awe na taarifa kuwa yupo katika kipindi cha majaribio na kitakuwa cha muda gani
  • Masharti muhimu ambayo mfanyakazi anapaswa kuyazingatia katika kipindi cha majaribio lazima ayafahamu
  • Mwajiri kumfuatilia na kutathmini utendaji wa mfanyakazi kulingana na vigezo walivyokubaliana wakati wa kuajiriwa.
  • Mwajiri anapaswa akutane na mfanyakazi na kufanya naye mazungumzo na tathmini ya pamoja juu ya utendaji wake. Mwajiri anapaswa kutoa mwongozo kwa mfanyakazi ambao unaweza kuwa ushauri, maelekezo, semina n.k katika kipindi cha majaribio.
  • Endapo kipindi cha majaribio kitaongezwa tofauti na kile kilichokubaliwa kwenye mkataba ni lazima mfanyakazi apate taarifa.

 

 

Utaratibu wa usitishaji wa Ajira kwa Mfanyakazi aliye katika kipindi cha Majaribio

Kama tulivyoeleza kuwa lengo kuu la kipindi cha majaribio ni mwajiri kujiridhisha iwapo mfanyakazi husika anakidhi vigezo na ana uwezo wa kumudu majukumu ya kazi kutokana na utendaji wake wa kazi. Hivyo baada ya kipindi cha majaribio kunategemewa hatua mbili kuchukuliwa aidha kuajiriwa moja kwa moja (confirmation of employment) au kusitisha mahusiano ya ajira.

Endapo mwajiri hajaridhika na utendaji wa mfanyakazi katika kipindi cha majaribio anapaswa kufuata utaratibu ufuatao;

  • Mwajiri anapaswa kumtaarifu mfanyakazi juu ya kutokuridhika na utendaji wake kulingana na vigezo au masharti waliyokubaliana wakati wa kuanza kipindi cha majaribio
  • Mwajiri anapaswa kumpa mfanyakazi fursa ya kujibu hoja za mwajiri ambazo amezileta juu ya utendaji wake. Mfanyakazi ana haki ya kuandika utetezi wake kwa nini asiondolewe katika kipindi cha majaribio.
  • Mwajiri anapaswa kumpa ruhusa mfanyakazi kutetewa na mfanyakazi mwengine au mwakilishi wa chama cha wafanyakazi kuhusu suala lake la utendaji

Baada ya kufanya mchakato huu na kubainika kuwa mfanyakazi hajakidhi vigezo husika basi mwajiri anaweza kusitisha ajira ya mfanyakazi.

Muhimu

Mwajiri kabla ya kumwachisha kazi mfanyakazi lazima azingatie masharti haya

  • Kwamba mfanyakazi anajua yupo katika kipindi cha majaribio na anafahamu juu ya masharti ya kazi husika na viwango anavyopaswa kufikia
  • Kwamba mwajiri amechukua hatua za kushauriana na mfanyakazi na kumhimiza ikiwa ni pamoja na kumpa mafunzo ya kutosha lakini bado mfanyakazi anashindwa kufikia vigezo
  • Mwajiri anaanzisha mchakato wa kusitisha ajira na mfanyakazi anapata fursa ya kujitetea.

Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri kufuata utaratibu huu wa kusitisha ajira ya mfanyakazi katika kipindi cha majaribio kisichopungua miezi 6. Hivyo mwajiri hana haki ya moja kwa moja kusitisha ajira ya mfanyakazi kwenye kipindi cha majaribio bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Mfanyakazi aliye kwenye kipindi cha majaribio cha kuanzia miezi 6 na ajira yake kusitishwa pasipo kufuata utaratibu kama ilivyoelewa basi anayo haki ya kupinga uamuzi wa mwajiri mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.

 

Hitimisho

Kipindi cha majaribio wakati wa mchakato wa mahusiano ya ajira ni muhimu kwa pande zote kujiridhisha juu ya tija, manufaa na ufanisi utakaozalishwa mahali pa kazi. Hatahivyo, waajiri wengi hawajui msingi wa kipindi hiki na majukumu yao zaidi ya kukiandika kwenye mkataba tu, na mara wanapoona hawaridhiki na utendaji wa mfanyakazi pasipo kufanya tathmini ya haki wanasitisha ajira. Hali hii inazalisha migogoro ya kazi isiyo ya lazima mahali pa kazi na kupoteza muda ambao ni rasilimali muhimu.

Ni rai yangu kwa mwajiri kutafuta ushauri wa kisheria kwa wataalam wa sheria ya kazi ili waepuke makosa katika masuala ya kazi. Pia mfanyakazi fahamu unazo haki za msingi hata katika kipindi cha majaribio.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.