Nifanye nini eneo langu likivamiwiwa na wavamizi wa ardhi?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu  kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kujibu moja ya changamoto ambayo zinawakuta wamiliki endapo litavamiwa na watu wengine. Karibu tujifunze.

Uvamizi wa Maeneo

Kama tulivyoona katika makala iliyopita juu ya hatua za kuchukua ili kulinda eneo lako la ardhi lisivamiwe na wavamizi. Leo tunaangalia hatua za kuchukua endapo tayari kuna mvamizi au wavamizi katika eneo lako.

Mambo ya msingi ya kuzingatia

  1. Hakikisha unaitambua mipaka ya eneo lako sahihi

Watu wengi wanakuwa na maeneo wala hawatambui mipaka yao katika eneo husika. Katika makala iliyopita nilieleza umuhimu wa mipaka. Hakikisha unalitambua eneo lako vizuri ili hata uvamizi unapojitokeza uweze kuchukua hatua za haraka kuwaondosha wavamizi kwa kufuata taratibu za kisheria na hata kijamii.

  1. Toa notisi kwa wavamizi maramoja

Mara upatapo taarifa za uvamizi na kudhibitisha kuwa eneo lako limevamiwa na wavamizi wa ardhi toa notisi ya kutaka kuwatoa katika eneo na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao. Hili ni jambo la msingi sana, wengi hawazingatii katika kuchukua hatua za awali za kurejesha eneo lao chini ya udhibiti wao. Wengi wanabaki kulalamika na kuacha kuchukua hatua muafaka. Fuatilia majina yao au taarifa zao kisha toa notisi ya maandishi kwa kila mmoja hakikisha na uongozi wa mtaa au kijiji una taarifa juu ya notisi hiyo. Endapo wavamizi watachukua hatua ya kuondoka basi utakuwa umerudisha eneo lako chini ya udhibiti wako.

  1. Wasilisha malalamiko katika uongozi wa eneo ili kusuluhishwa

Iwapo wavamizi au mvamizi anakaidi kuondoka eneo lako mara moja, basi chukua hatua ya kuwasilisha malalamiko yako katika uongozi wa serikali ya Mtaa au Kijiji juu ya uvamizi huo ukiambatanisha na nakala yako ya notisi ya kumtaka au kuwataka wavamizi husika kuondoka eneo la uvamizi. Endelea kufuatilia namna ya serikali ya eneo inavyoweza kushughulikia tatizo hilo. Zipo kamati maalum katika kila serikali ya mtaa na kijiji zinazohusika na masuala ya ardhi ambazo zinaweza kuwaita wahusika na kujaribu kutafuta suluhu ya mapema katika mgogoro husika.

  1. Wasilisha shauri katika vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi

Endapo itajitokeza kutokupatikana suluhu kupitia uongozi wa serikali ya mtaa au kijiji, chukua hatua ya kuwasilisha mgogoro wako wa ardhi katika chombo chenye mamlaka ya uamuzi juu ya masuala ya ardhi. Hii ni hatua ya mwisho kabisa endapo mvamizi au wavamizi wanakataa kuondoka ikiwa notisi wamepata, uongozi wa mtaa au kijiji umeshindwa kusuluhisha basi fungua mgogoro wa ardhi. Katika masuala ya ardhi yapo mabaraza yanayohusika na utatuzi kutegemea na thamani ya eneo au iwapo ni ardhi ya kijiji au ya jumla. Ngazi ya chini ya kufungua mgogoro kwa ardhi ya kijiji ni Baraza la Ardhi la Kijiji na kwa ardhi ya mjini/jumla ni Baraza la Kata la Ardhi. Vyombo hivi vinauwezo wa kusikiliza mashauri ya ardhi na kuchambua ushahidi juu ya umiliki wa eneo husika.

Watu wengi kwa kukosa ushauri au kushauriwa vibaya kwenye utatuzi juu ya migogoro ya ardhi wamekuwa wakiwasilisha matatizo yao kwenye vituo vya Polisi. Kimsingi mambo ya ardhi yana vyombo maalum hasa linapokuja suala la kujua ni nani mmiliki. Chombo cha Polisi kazi yake ni kushughulikia suala la kijinai lililotendeka katika eneo husika. Hivyo ni muhimu sana kutokupoteza muda katika kutafuta suluhu mahali isipopatikana bali kwenye vyombo husika.

Hitimisho

Kama nilivyoeleza uvamizi wa maeneo imekuwa moja ya changamoto kubwa katika siku za hivi karibuni. Ukosefu wa umakini na uangalizi dhabiti katika maeneo yetu ni moja ya sababu za kuvamiwa kwa maeneo yetu. Ni muhimu sana kuhakikisha maeneo yanalindwa vizuri na kuna alama za mipaka za kudumu ambazo zitasaidia wavamizi kuogopa kuingia kwenye eneo.

Endapo utaacha uvamizi kuendelea kwa kipindi kirefu katika eneo lako, kunaweza kusababisha hatari ya kupoteza eneo lako lote au sehemu au kuingia hasara ya kuwa na migogoro ya muda mahakamani.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili