Matumizi ya Madalali katika ununuzi au upangishaji wa ardhi.

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kuangalia nafasi ya Madalali katika matumizi ya ardhi. Karibu tujifunze.

Dalali ni nani?

Watu wengi katika kupata ardhi zao au nyumba za kupangisha wametumia watu wanaoitwa madalali. Tunafahamu kwa uchache juu ya shughuli zao wanazofanya kila siku.

Dalali ni mtu yeyote au taasisi inayofanya kazi ya uwakala ili kufanikisha biashara baina ya mteja na mtoa huduma fulani. Dalali ni mtu wa kati anayewaunganisha mteja na mwenye mali kwa kupata ujira unaotokana na kuwakutanisha pande mbili.

Nafasi ya Udalali

Ni kweli kwamba kwa sasa shughuli nyingi na biashara nyingi zinafanikishwa na uwepo wa madalali. Madalali wamekuwa kiungo kikubwa cha kufanikisha biashara na huduma mbali mbali sehemu za mjini na hata maeneo ya vijijini. Hali ya biashara ya kukutana mteja na mwenye mali imekuwa tofauti, matumizi ya madalali yamekuwa makubwa na yanaongezeka kila kukicha.

Katika sekta ya ardhi yaani ununuzi na ukodishaji wa nyumba, madalali wamekuwa kiungo muhimu katika kuwakutanisha wahitaji wa ardhi na nyumba pamoja na wamiliki na kufanikisha biashara au huduma.

Hata hivyo zipo changamoto kadhaa zinazoambatana na uwepo wa madalai katika biashara ya ardhi na nyumba ambazo kama mmiliki au mteja unapaswa kuzijua na kuzingatia kabla hujachukua maamuzi ya kutumia dalali katika kufanikisha upatikanaji wa nyumba au ardhi.

Changamoto za Madalali

  1. Kutokusajiliwa kisheria

Kazi ya udalali ni kama kazi nyingine ambayo ni rasmi na ina sheria ambazo zinaongoza shughuli hii. Madalali wengi wa mijini hawajasajiliwa na mamlaka za Serikali na hawatambuliki shughuli hiyo wanayoifanya. Wengi wanafanya kwa mazoea tu na si watu ambao unaweza kujua wapi wanapatikana kwani hata ofisi hawana, ni watu wa vijiweni. Ni muhimu sana kwa mteja au mmiliki kutafuta madalali ambao wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria ili yanapojitokeza matatizo yanayohusiana na shughuli yake ya udalali unayo haki ya kisheria dhidi yake. Kama dalali hajasajiliwa shughuli yake ni batili kisheria na hatakama akikushauri kimakosa na kupata hasara ni vigumo kwako kumchukulia hatua za kisheria.

  1. Kutokuwa waaminifu

Kwa kuwa madalali wengi hawaichukulii shughuli hii kama kazi ya heshima na staha, imejikuta kazi yao inavamiwa na watu wasio waaminifu. Wapo watu wanaojifanya madalali lakini ukweli ni matapeli wa viwanja na biashara za nyumba. Wanaweza kuchuka kiasi cha fedha kwa mteja anayetafuta nyumba au kiwanja na kisha kutotimiza kazi waliyotumwa au wakapeleka wateja eneo ambalo tayari lina mmiliki au wakauza eneo ambalo linamilikiwa au lipo kwenye mgogoro. Katika kazi yoyote uaminifu ni msingi wa kujenga biashara na huduma bora kwa wateja. Mteja au mmiliki kabla hujaamua kuingia katika kupata huduma ya dalali chunguza kwanza uaminifu wake kwa kutafuta shughuli alizowahi kufanya hapo awali na kuwa na taarifa zake sahihi.

  1. Kupandisha gharama za ardhi au nyumba

Eneo lingine ambalo madalali wamekuwa na changamoto ni kupandisha gharama za maeneo au ukodishaji wa majengo kuliko kiwango kilichokusudiwa na mmiliki au mteja. Madalali wengi wanakosa misingi ya utendaji kazi bora kwa kuzingatia jambo moja tu yaani faida kubwa ya kazi wanayoifanya. Watu wengi wamejikuta wananunua au wanakodishwa majengo kwa gharama kubwa sana hata mara tatu ya gharama halisi hii ni kwa sababu ya kuongeza kamisheni ya dalali. Yapo matukio ambayo mmiliki anaweza kuuza kiwanja au jingo mathalani kwa kiasi cha Milioni 10 na dalali akaleta mteja wa milioni 30 hapo mzozo unaanza kwamba dalali anataka apate milioni 20 na mmiliki apate milioni 10. Vipo visa vingi vya aina hiyo ambavyo vimesababisha uvunjifu wa amani maeneo mbali mbali na biashara kuharibika.

  1. Kutokufuata misingi ya udalali

Kama nilivyosema kila kazi ina misingi yake ili iweze kutoa huduma bora na yenye manufaa katika jamii. Hali kadhalika kazi ya udalali ina misingi yake ambayo dalali yeyote anapaswa kuizingatia. Misingi ya udalali ni pamoja na kufuata sheria katika usajili, kuhakikisha una ofisi ambayo ni maalum inayotumika kufanya shughuli zako na pia kuzingatia uaminifu na uadilifu wakati wote. Wapo madalali wanaweza kukupangisha kwenye nyumba, lakini baada ya muda kabla mpangaji hajamaliza muda wake wanaleta mteja mwengine kwa mwenye nyumba mwenye fedha zaidi na kusababisha mpangaji wa awali kufukuzwa kwenye nyumba. Huu ni msingi mbaya katika kazi hii ambao hawezi kutenda kazi yenye mafanikio.

Hitimisho

Yapo mambo mengi ya kushirikishana kuhusiana na kazi ya udalali na muhimu zaidi kwa wateja wa madalali kuzingatia changamoto ambazo tumezijadili leo ili kuhakikisha hawapotezi fedha zao na muda hata mahusiano mema ya kijamii kwa kutumia madalali.

Nisisitize kuwa kazi hii ya udalali ni nzuri pia ina tija kwenye jamii lakini wahusika wanapaswa kuifanya kwa kufuata misingi ya kazi ili jamii ikubali na kutofautisha kati ya udalali na utapeli.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili