Upangishaji wa Ardhi au Majengo

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kuangalia suala la upangishaji wa ardhi na majengo. Karibu tujifunze.

Upangishaji wa ardhi

Katika matumizi ya ardhi na majengo ambayo yamejengwa juu yake kuna huduma pia ya kupangisha au kukodisha ardhi kwa matumizi ya watu wengine. Ardhi inaweza kukodishwa kwa madhumuni ya kilimo au makazi au biashara n.k. hii inadhihirisha kuwa si wote wanaotumia ardhi au majengo ni wamiliki wa majengo hayo au ardhi hizo. Biashara nyingi na hata makazi ambayo watu wanakaa wanaingia makubaliano baina ya mmiliki na mpangaji.

Ukodishaji huu unahusisha pande mbili yaani mmiliki na mpangaji ambao wanaingia kwenye makubaliano ikiwa ni yam domo au maandishi.

Katika makala hii tunakwenda kuangalia mambo ya msingi ambayo pande zote mbili zinapaswa kuzingatia kabla na wakati wa kipindi cha upangishaji.

Mambo ya Msingi ya kuzingatia katika upangishaji

Yapo mambo mengi ambayo pande zote zinapaswa kuzingatia kabla na wakati wa upangishaji wa ardhi au majengo au vyumba vya biashara ili kuhakikisha wanaishi kwa amani kwa kipindi chote. Katika makala hii tunaangalia baadhi ya mambo.

  1. Uhakika wa umiliki wa ardhi au jengo

Hili ni jambo la msingi na muhimu kuzingatia kabla ya kuingia katika mahusiano ya upangishaji. Mmiliki lazima athibitishe kuwa yeye ndiye mmiliki na mpangaji ana wajibu wa kujiridhisha kuwa anayempangisha ni mmiliki au wakala ambaye ana mamlaka juu ya eneo husika. Siku hizi watu wamekosa uaminifu anaweza kukupangisha eneo au ardhi si yake na ukajikuta umeingia hasara. Ni vyema ukahakikisha ikiwezekana kama eneo lina hati basi mmiliki aioneshe kuwa ina jila lake na anayo mamlaka ya kukupangisha. Wapangaji wengi wanakuwa na hofu ya kuhoji mambo ya msingi kama hayo wakati ni haki yao. Wengi wametapeliwa kwa kutokuchukua hatua madhubuti kujiridhisha. Ipo migogoro mingi katika nyumba za urithi unakuta kila mrithi anapangisha chumba chake wakati kuna msimamizi wa mirathi. Hii inapelekea mpangaji kupoteza fedha zake na kupata usumbufu usio na lazima. Kama mmiliki amempa mtu mamlaka ya kupangisha kwa niaba yake ni muhimu mamlaka hiyo ikawa kwa maandishi ili mpangaji aweze kuona nakala yake na kujiridhisha.

  1. Eneo la upangaji likidhi kusudi la upangishaji

Hakikisha kuwa eneo la upangishaji linakidhi matumizi ambayo mpangaji amekusudia kufanya shughuli zake. Hii ina maana kama unakodisha eneo kwa ajili ya kilimo basi mazingira na mamlaka ziwe zinaruhusu eneo hilo kwa kilimo. Ikiwa unakodisha kwa shughuli za biashara basi eneo hilo liwe linaruhusiwa shughuli husika. Kuna maeneo hayaruhusu shughuli za viwanda au kumbi za starehe kitu ambacho kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani miongoni mwa jamii.

  1. Kodi/ pango

Kinachowaunganisha baina ya mmiliki na mpangaji ni suala zima la kodi ya pango yaani kiasi cha fedha wanachokubaliana kwa lengo la kupangishwa eneo. Ni muhimu sana kiasi cha kodi kikafahamika mapema na namna pande hizo zinaweza kulipana pasipo mgongano. Pamejitokeza malumbano baina ya wapangaji na wamiliki hasa pale mpangaji anapochukua jukumu kurekebisha eneo la upangaji kwa gharama zake kwa ahadi kuwa watakatana kwenye kodi. Suala hili limezua mzozo kwani pande zote haziaminiani mmiliki anaona gharama za marekebisho ni kubwa na mpangaji anatafuta nafuu ya kodi kutokana na gharama za ziada alizoingia. Muhimu mmiliki kukamilisha kazi zake kuhusiana na eneo ili mpangaji aje kupanga kama lilivyo.

  1. Muda wa upangishaji

Suala la upangaji ni suala la muda halipo moja kwa moja kwani hata umiliki wa eneo tunapatiwa hati za umiliki kwa muda maalum. Wapangaji na wamiliki wengine wanaingia katika makubaliano pasipo kuweka muda wa ukomo wa upangaji au upangishaji. Baada ya muda mizozo inaibuka kwani mpangaji anasahau wajibu wake wa kulipa akidhani ni kwake na mmiliki pia anasahau hata kufanya marekebisho ya eneo husika kiasi kwamba kila upande unalaumu mwenzake. Kuweka muda katika makubaliano ya upangishaji kutasaidia kupata nafasi ya kutathmini juu ya mahusiano yenu na suala la gharama za uchumi ikiwa zimepanda kwa kiasi gani zinaathiri kodi.

  1. Mkataba

Mkataba wa maandishi ni jambo la muhimu sana katika kuhakikisha mahusiano ya upangaji yanakuwa ya amani na kuheshimiana. Kila upande katika mkataba wa maandishi utapata nafasi ya kujua wajibu wake na haki zake ili wasikoseane kwa namna yoyote. Mkataba wa maandishi unawasaidia kufahamu masuala ya kodi, muda na wajibu wao. Mkataba utakusaidia endapo upande utakiuka masharti basi kuna haki ya kwenda kwenye vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Hitimisho

Mahusiano ya mmiliki na mpangaji yapo kwa mujibu wa sheria ya ardhi ambapo kila upande una haki na wajibu wa kutimiza. Tusifanye biashara ya ukodishaji kwa mazoea bali tufuate sheria ili itusaidie kutuongoza katika mahusiano haya. Kokosa kufuata sheria na miongozo katika upangishaji mwisho wake ni hasara kwa pande zote mbili.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili