Wajibu wa Mmiliki katika Upangishaji wa ardhi/jengo
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kuangalia juu ya wajibu wa mmiliki katika suala la upangishaji wa ardhi au jengo. Karibu tujifunze.
Upangishaji wa ardhi
Kama tulivyotangulia kueleza katika makala iliyopita kuhusiana na upangishaji ambao ni mahusiano baina ya pande mbili yaani mmiliki wa ardhi au jengo na mpangaji. Pande hizi zinaingia katika makubaliano ya kimkataba.
Kimsingi mahusiano yanayojengwa baina ya mmiliki na mpangaji katika ardhi ni mahusiano ya kisheria. Sheria ya ardhi imeweka mwongozo juu ya wajibu wa pande zote mbili na haki zao. Katika makala hii tunakwenda kutazama mambo ya msingi ya mmiliki anayopaswa kuzingatia kama wajibu wake wakati wa upangishaji wa ardhi au jengo lake.
Wajibu wa Mmiliki wa ardhi katika upangishaji
- Wajibu wa kumpa mpangaji uhuru wa kutumia eneo alilopanga
Mmiliki wa nyumba au eneo la ardhi anapaswa kujua kwa kipindi kile ambacho eneo hilo amepangisha linakuwa chini ya umiliki wa mpangaji iwapo mpangaji atakuwa amelipa kodi ya pango na kuzingatia masharti yote ya upangaji. Mmiliki au wakala wake hapaswi kuingilia uhuru wa mpangaji kwa namna yoyote ile katika kipindi cha upangaji wake. Sheria inalinda uhuru wa mpangaji dhidi ya matendo yoyote ya mmiliki au wakala wake. Ipo tabia baadhi ya wamiliki kuingilia maisha au shughuli za wapangaji kwa kigezo wao ni wamiliki hii si sahihi kwani mpangaji anayo haki ya kutoingiliwa katika maisha yake au shughuli zake anazofanya alimradi zipo kwa mujibu wa sheria na kulingana na mkataba.
- Wajibu wa kuhakikisha eneo jirani haliingilii uhuru wa mpangaji kwa namna yoyote.
Iwapo mmiliki ana eneo ambalo ni jirani na la mpangaji inampasa kuhakikisha kuwa shughuli katika eneo hilo haziingilii uhuru wa mpangaji. Mmiliki anapaswa kuhakikisha eneo jirani na lile alilopangisha linakuwa katika mazingira mazuri ya kumuruhusu mpangaji kufurahia uhuru wa upangaji wake. Mmiliki ahakikishe njia inayoenda kwenye eneo la mpangaji inapitika vizuri.
- Kuhakikisha eneo lililokodishwa lipo salama na limerekebishwa ipasavyo kwa ajili ya lengo la upangaji.
Ni wajibu wa mmiliki kuhakikisha eneo la upangaji limerekebishwa kukidhi viwango vya upangaji kwa kusudi husika. Mpangaji hapaswi kuingia gharama za kurekebisha eneo la upangaji huo ni wajibu wa mmiliki. Tumeona migogoro mingi baina ya wamiliki na wapangaji inatokana na wamiliki kutotimiza wajibu wao kwa kuwaachia wapangaji uhuru wa kufanya marekebisho ya eneo kwa miadi ya kukatana kweny kodi na mwisho wake wanakosa maelewano.
- Kuhakikisha kodi za majengo na ardhi zinalipwa
Huu ni wajibu muhimu sana wa mwenye eneo yaani mmiliki. Tunajua kuwa ardhi ni mali ya umma na wamiliki wana wajibu wa kuhakikisha kodi ya ardhi na majrngo inalipwa ndani ya wakati kama sheria zinavyoongoza. Mpangaji kwa kawaida hausiki na malipo ya kodi za majengo na ardhi mpaka pale kutakapokuwa na makubaliano vinginevyo.
Hitimisho
Mmiliki ana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa kila kitu kiko sawa ili eneo lake linapopangishwa lisiwe katika migogoro ya aina yoyote baina yake na mpangaji au mamlaka za serikali na majirani. Wajibu wa mmiliki unapotekelezwa vizuri ni haki za mpangaji. Mmiliki akitimiza wajibu wake anastahili kupata kodi yake kwa wakati kutoka kwa mpangaji.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili