Wajibu wa Mpangaji katika Upangishaji wa ardhi/jengo

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kuangalia juu ya wajibu wa mpangaji katika suala la upangishaji wa ardhi au jengo. Karibu tujifunze.

Upangishaji wa ardhi

Kama tulivyotangulia kueleza katika makala iliyopita kuhusiana na upangishaji ambao ni mahusiano baina ya pande mbili yaani mmiliki wa ardhi au jingo na mpangaji. Pande hizi zinaingia katika makubaliano ya kimkataba.

Katika makala iliyopita tulijadili kwa mapana juu ya wajibu wa mmiliki katika zoezi zima la upangishaji wa eneo au nyumba. Mambo muhimu ambayo anapaswa kuzingatia. Leo tunaangalia juu ya wajibu wa mpangaji anaopaswa kuzingatia katika upangishaji.

Wajibu wa Mpangaji wa ardhi katika upangishaji

  1. Kulipa kodi ya pango kwa wakati na namna ilivyokubaliana

Uhusiano wa mmiliki na mpangaji unajengwa kwa mpangaji kupewa eneo la upangaji na yeye kuhakikisha analipa kodi ya pango kama ilivyokubaliwa katika mkataba wao. Huu ni wajibu mkubwa na muhimu sana kwa mpangaji kulipa kodi kwa wakati. Mzozo mkubwa baina ya pande mbili unatokana na wapangaji kuwa wazito kulipa kodi kwa wakati.

  1. Wajibu wa kutumia eneo alilopangishwa kwa makusudi ya matumizi ya eneo hilo tu

Mpangaji anawajibika kutumia eneo la upangishaji kwa madhumuni yale tu ambayo yanaruhusiwa na sheria ya Ardhi pamoja na kile walichokubaliana na mmiliki katika mkataba wa upangishaji. Ikiwa umepanga kwa madhumuni ya makazi basi hairuhusiwi kutumia eneo hilo kibiashara.

  1. Kuhakikisha eneo linakuwa katika hali ile ambayo alipangishwa wakati wa kumaliza muda wa upangaji

Ni wajibu wa mpangaji katika kipindi chote cha upangaji kuhakikisha analitunza eneo la upangaji ili lisipate uharibifu wa aina yoyote. Ikitokea mpangaji amefanya uharibifu basi atawajibika kulipa au kufanya marekebisho husika. Uaribifu huu ni ule unaohusiana na kubadili mwonekano wa eneo kwa namna ambayo matumizi ya upangaji kwa mtu mwengine hayatowezekana pasipo kuingia gharama kwa mmiliki.

  1. Kuhakikisha mipaka inatunzwa wakati wote

Mmiliki mara tu anapomkabidhi mpangaji eneo la upangishaji anawajibika kumwonesha mipaka yake na ni wajibu wa mpangaji kuhakikisha anaitunza mipaka husika ya eneo.

  1. Kutoa ruhusa kwa mmiliki au wakala wake kufanya ukaguzi kwa taarifa

Sheria ya Ardhi inamruhusu mmiliki kufanya ukaguzi katika eneo lake ya umpangishaji. Hata hivyo ukaguzi huo ni lazima ufanywe kwa taarifa kwenda kwa mpangaji. Lengo la ukaguzi ni kuona hali ya eneo ikiwa linahitaji marekebisho au la.

  1. Kutokukodisha au kuhamisha upangaji wake kwa mtu yeyote pasipo ruhusa ya mmiliki

Mpangaji haruhusiwi kwa namna yoyote kuhamisha haki zake za upangaji kwa mtu mwengine au kukodisha sehemu ya eneo la upangishaji kwa mtu mwengine pasipo makubaliano ya awali na mmiliki wa eneo.

Hitimisho

Kama tulivyoeleza katika makala iliyopita kuwa wajibu wa mmiliki ndio haki za mpangaji na hali kadhalika wajibu wa mpangaji ndio haki ya mmiliki. Kila upande ukitimiza wajibu wake basi mahusiano ya pande zote yatadumu kwa amani na utulivu katika kipindi chote cha upangaji na kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili