23.A. Usitishaji wa Ajira kwa Utovu wa Nidhamu

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Leo tunaangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa Utovu wa Nidhamu. makala kuhusu usitishaji wa ajira kutokana na utovu wa nidhamu zitakuwa kwa mfululizo ili kuweza kupata picha nzuri na uelewa mpana kwa waajiri na wafanyakazi juu ya utaratibu na sababu zinazotakiwa kuwepo endapo usitishaji wa ajira utakuwa ni kutokana na utovu wa nidhamu. Karibu tujifunze.

Utovu wa Nidhamu

Sheria ya Ajira inatambua kuwa mojawapo ya sababu ambazo zinaweza kusababisha mwajiri kusitisha ajira ya mfanyakazi ni utovu wa nidhamu. Utovu wa nidhamu inahusisha matendo au makosa ambayo anafanya mfanyakazi kinyume na taratibu za kazi kama zilivyoelezwa kwenye sera au kanuni za mahali pa kazi.

Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri kabla ya kufikia kuchukua uamuzi wa kumwachisha mfanyakazi kwa sababu ya utovu wa nidhamu, anapaswa kuchukua hatua kidogo kidogo za kinidhamu kama kushauri, nasaha na maonyo. Hatahivyo mwajiri anaweza kuchukua hatua kali ya kinidhamu ya kusitisha ajira endapo kosa litadhibitika kuwa haliwezi kurekebishika au limepelekea mahusiano ya kiajira kuharibika kwa kiasi kikubwa.

Mambo Muhimu ya Kuzingatia kwa Mwajiri katika kushughulikia mambo ya Kinidhamu

  1. Kuwepo kwa kanuni za mahali pa kazi

Lazima mwajiri awe na sera na mwongozo wa kanuni mahali pa kazi. Ni vigumu kwa mwajiri kumchukulia hatua za kinidhamu mfanyakazi pasipo kuonesha ni kanuni ipi au zipi mfanyakazi amevunja. Waajiri wengi ima kwa kupuuzia au kutokujua hawana mwongozo au kanuni za utendaji bora mahali pa kazi, kiasi kwamba hata makosa yakijitokeza.

  1. Wafanyakazi wafahamishwe juu ya kanuni

Kanuni za utendaji mahali pa kazi ni lazima zifahamike kwa wafanyakazi. Haina maana kuwa na kanuni ambazo wafanyakazi wanapaswa kuzizingatia katika utendaji wao wa kila siku lakini hawana taarifa juu ya uwepo wake. Mwajiri anapaswa kuwafahamisha wafanyakazi juu ya kanuni hizo wakati wa kuajiriwa, wakati wa vikao na hata kuzibandika katika ubao wa matangazo kwa lugha inayoeleweka kwa wafanyakazi.

Hitimisho

Kama tulivyoona katika makala hii ya utangulizi juu ya usitishaji wa ajira kutokana na utovu wa nidhamu, kwamba upo utaratibu maalum ambao mwajiri anapaswa kuzingatia. Tumeona lazima kuwepo na kanuni za mahali pa kazi za kuongoza wafanyakazi na ni lazima wafanyakazi wazifahamu. Huu ndio msingi ambao mwajiri anapaswa awe nao mahali pa kazi. Waajiri wengi wanakuwa wepesi wa kuchukua hatua za kinidhamu pasipo kuweka msingi huu wa kanuni na mwisho wake ni kujikuta wanashindwa katika migogoro ya kiajira inayofikishwa mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.