75. Mkataba wa Upangishaji wa eneo au nyumba

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kuangalia juu ya mkataba wa upangishaji wa eneo au nyumba. Karibu tujifunze.

Mkataba wa Upangishaji

Katika mfululizo wa makala hizi tumekuwa tukiangalia mambo mbalimbali kuhusiana na masuala ya ardhi. Mojawapo ya kigezo muhimu ambacho tulikigusia kwenye mahusiano baina ya mmiliki na mpangaji ni kuwepo kwa mkataba wa maandishi.

Mkataba wa upangishaji ni makubaliano ya kisheria baina ya mpangaji na mmiliki ambayo yatawaongoza katika kipindi chote cha upangishaji. Mkataba unaweza kuwa wa maandishi au wa mdomo. Hatahivyo kutokana na umuhimu na changamoto zinazojitokeza katika mahusiano haya ni vyema mkataba ukaandaliwa kuwa wa maandishi.

Hivyo katika makala hii tunakwenda kuangalia mambo ya msingi yanayopaswa kuwepo katika mkataba wa upangishaji baina ya mmiliki na mpangaji.

Mambo ya Msingi katika Mkataba wa Upangishaji

Yapo mambo ya msingi na muhimu ya kuzingatia katika kuandaa mkataba wa upangishaji baina ya mmiliki na mpangaji ambayo yanapaswa kuzingatiwa.

  1. Majina na anauani za Mmiliki na Mpangaji

Katika mkataba wa upangishaji ni muhumu yakawepo majina ya mmiliki na mpangaji pamoja na anuani zao au mawasiliano yao. Mmiliki na mpangaji ndio watu wenye nguvu ya kisheria ya kuingia makubaliano ya upangishaji. Hivyo hakikisha majina yao yanaonekana kwenye mkataba kwani endapo utatokea mgogoro huwezi kumshitaki mtu asiye mmiliki au asiye mpangaji.

  1. Lengo la mkataba

Mkataba lazima uoneshe dhumuni lake ni nini. Je, upangishaji huo ni kwa ajili ya eneo la kilimo au makazi au biashara au kiwanda n.k. kuonesha lengo la upangishaji katika mkataba kunasaidia kila upande kuheshimu dhumuni hilo na kuhakikisha linafuatwa wakati wote. Mkataba usionesha dhumuni lake mara nyingi unaweza kusababisha mgogoro kwani mpangaji anaweza kuanzisha shughuli nyingine katika eneo hilo na kutofautiana na mmiliki.

  1. Kiasi cha kodi

Kodi ya pango ndio kiunganisho baina ya mpangaji na mmiliki kwani mmiliki anatoa eneo na mpangaji analipa kodi kwa matumizi ya eneo husika. Kiasi cha kodi lazima kiwe bayana na kinalipwa kulingana na muda gani mfano kwa siku, au wiki au mwezi n.k. mara kwa mara mikataba mingi ya upangishaji kodi inalipwa kwa mwezi. Ni lazima kodi ilipwe kama ilivyokubaliwa ikiwa ni mwisho wa mwezi au kwa kuwekwa kwenye akaunti au taslimu n.k.

  1. Masharti maalum

Mkataba ni lazima uoneshe masharti maalum yanayozibana pande zote. Mkataba unapaswa kuonesha wajibu na haki za mmiliki kwa upande mmoja na pia haki na wajibu wa mpangaji. Pia unapaswa kuonesha masharti ya jumla kwa pande zote.

  1. Muda wa Mkataba

Mkataba wowote unapaswa kuwa na muda maalum. Hakuna mkataba wa moja kwa moja katika upangishaji. Hivyo pande zote lazima zikubaliane juu ya kipindi cha upangishaji. Kuna upangishaji katika kipindi cha mwezi au mwaka au miaka kadhaa. Muhimu zaidi mkataba uoneshe mwanzo wa upangishaji na mwisho wake. Kama pande zote zitaridhia mkataba unaweza kuonesha namna ya kuhuisha mkataba.

  1. Mashahidi

Mkataba ni lazima uwekwe sahihi na pande zote yaani mmiliki na mpangaji. Ikiwa mkataba umeandaliwa na mmiliki na mpangaji basi ni vyema kukawa na sehemu ya mashahidi wa pande zote. Mashahidi wanaweza kuwa ndugu wa karibu au viongozi kwenye eneo yaani mjumbe au viongozi wa serikali ya mtaa. Iwapo mkataba utakuwa umeandaliwa kwa Wakili basi wakili ataweza kuwa shahidi wa pande zote.

  1. Utatuzi wa mgogoro

Katika jambo lolote la kimkataba ni wazi mgogoro unaweza kujitokeza, hivyobasi ni muhimu sana mkataba ukaainisha namna ya utatuzi wa mgogoro endapo utajitokeza. Mikataba mingi ya upangishaji inaeleza juu ya usuluhishi wa migogoro na endapo usuluhishi unashindikana basi mgogoro utakwenda kutatuliwa katika vyombo vya utatuzi vya kisheria.

Hitimisho

Katika mahusiano ya upangishaji baina ya mmiliki na mpangaji mkataba wa maandishi ni kiungo muhimu sana. Wengi tunapuuzia juu ya uwepo wa mkataba kwani tuna kawaida ya kuaminiana kwamba hakutajitokeza tatizo lolote baina ya mmiliki na mpangaji, jambo hili si zuri kwani hatuwezi kujua ya kesho kama hatuweka kumbukumbu vizuri.

Hivyobasi mmiliki na mpangaji chukua hatua ya kuhakikisha kabla hujaanza kipindi cha upangishaji umeandaa mkataba au waone wanasheria wakuandalie mkataba husika ili haki na wajibu wako ziweze kulindwa kisheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili