Njia ya Umiliki wa Ardhi katika Tanzania

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kuangalia njia mbalimbali za umiliki wa ardhi katika Tanzania. Karibu tujifunze.

Umiliki wa Ardhi

Katika taifa la Tanzania moja ya rasilimali muhimu ambayo inahitaji ulinzi na utunzaji mkubwa ni ardhi. Ardhi yote ya Tanzania ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ipo chini ya mamlaka ya Rais wa Jamhuri kama mdhamini. Hivyo ardhi ni mali ya umma si ya mtu binafsi kama nchi nyingine kwa mifumo yao. Katika Tanzania uhalisia wa umiliki wa ardhi si wa moja kwa moja bali umiliki kwa ajili ya matumizi kwa muda maalum.

Katika makala hii tunakwenda kuangalia njia mbalimbali za kisheria ambazo mtu anaweza kuwa mmiliki wa ardhi.

Namna za umiliki wa ardhi katika Tanzania

Katika kuchambua namna za umiliki wa ardhi katika Tanzania zipo namna kuu mbili ambapo ardhi inaweza kumilikiwa, yaani umiliki wa kimila na ule wa kisheria. Katika aina zote hizi mamlaka na sheria za nchi zinatambua kuwa huu ni umiliki halali.

  1. Urithi

Raia wa Tanzania anaweza kumiliki ardhi kwa njia ya urithi. Sheria ya ardhi na zile zinazoongoza maswala ya mirathi zinatambua uwezo wa mmiliki kurithisha mali zake ikiwapo na ardhi. Kulingana na tamaduni za makabila mbalimbali, mwanamke hakuwa na uwezo wa kurithi mali hasa hasa ardhi. Hatahivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria zinaonesha kuwa haki ya kumiliki ardhi kwa njia ya urithi ni haki ya raia wote wa Tanzania bila kujali jinsia zao.

  1. Kugawiwa na Mkuu wa Familia au Ukoo

Sheria za kimila zinatambua mamlaka ya kifamilia na ukoo katika kugawa ardhi ya ukoo au familia. Raia wa Tanzania anayo haki ya kupewa ardhi na kuimiliki kutokana na familia au ukoo. Tamaduni za makabila mbalimbali zinaonesha kuwa ardhi inaweza kumilikiwa kifamilia au kiukoo na mkuu wa ukoo anao wajibu wa kuwagawia wanaukoo ardhi husika. Hivyo mwananchi anaweza kumiliki ardhi kwa njia hii ya kupewa kifamilia au kiukoo.

  1. Kupewa zawadi

Mtu anaweza kupata ardhi kwa kupewa zawadi na mtu anayehusiana naye. Sheria ya ardhi inatambua uwezekano wa watu wenye mahusiano ya karibu kumilikishana ardhi kwa njia ya zawadi. Mfano baba anaweza kumpatia mtoto zawadi ya eneo kumiliki. Tunayo mifano mingi mara baada ya kijana kuanza maisha ya ndoa wazazi wanaweza kumpatia mtoto zawadi ya kiwanja. Pia mume anaweza kumpatia mke zawadi ya kiwanja au shamba n.k. hii ni njia nyingine ambayo mwananchi anaweza kupata umiliki wa ardhi.

  1. Kugawiwa na Serikali

Serikali inayo mamlaka juu ya ardhi yote. Kupitia mipango mbalimbali ya miji Serikali inapima viwanja na kugawa maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama makazi, viwanda na biashara au mashamba. Katika kugawiwa maeneo na Serikali inapima maeneo na kugawa kwa wanachi kwa gharama nafuu. Katika ugawaji wa viwanja hivi mwananchi anapewa hati maalum yenye miaka 33 au 66 au 99 ya umiliki.

  1. Kununua kwenye soko

Pia mwananchi anaweza kupata umiliki wa ardhi kwa njia ya ununuzi wa ardhi. Hii ni njia iliyozoeleka kwa wengi hasa maeneo ya mjini. Watu wengi wanahamia na kuanzisha shughuli za maendeleo ambazo kwa kawaida zinategemea uwepo wa ardhi. Hivyo kuna biashara kubwa sana ya ardhi ambapo muuzaji na mnunuzi wanakubaliana gharama na kuuziana ardhi husika hivyo umiliki kuhama kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine.

  1. Kusafisha eneo la kichaka

Sheria za ardhi zinatambua kuwa mtu anaweza kumiliki ardhi kwa njia ya kusafisa eneo na kuanza kufanya shughuli katika eneo hilo. Yapo maeneo ndani ya nchi ambayo hayana umiliki wa mtu moja kwa moja. Maeneo ya namna hii yanapatikana hasa vijijini au maeneo ya porini. Muhimu kuhakikisha eneo ambalo unasafisha na kufanya shughuli zako si eneo la hifadhi.

  1. Uvamizi pasipo kuingiliwa na mmiliki

Uvamizi katika eneo wa muda mrefu pasipo ruhusa na mmiliki wala kuingiliwa na mmiliki ni mojawapo ya njia ambazo inatambuliwa katika umiliki wa ardhi. Kitendo hiki kinaitwa kwa lugha ya kisheria ‘adverse possession’ kwa maana mtu ni mvamizi katika eneo na anafanya shughuli katika eneo hilo kwa muda mrefu pasipo kuruhusiwa na mmiliki wala asiingiliwe na mmiliki kwa kipindi kisichopungua miaka 12 mfululizo. Hii inampa haki yule aliyeliendeleza na kuonekana kuwa mmiliki amelitelekeza eneo lake.

Hitimisho

Kama tulivyojadili njia na namna mbalimbali za umiliki wa ardhi Tanzania zinazotambuliwa kisheria ni muhimu kuzingatia kuwa umiliki huu wa ardhi ni kwa raia wa Tanzania tu, hazihusiani na mtu ambaye si raia wa Tanzania.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili