23.B. Usitishaji wa Ajira kwa Utovu wa Nidhamu

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa Utovu wa Nidhamu. Karibu tujifunze.

Utovu wa Nidhamu

Katika makala iliyopita tulipata utangulizi juu ya utovu wa nidhamu kuwa sababu mojawapo ya kuweza kupelekea mwajiri kusitisha ajira ya mfanyakazi. Pia tulizungumzia maana ya utovu wa nidhamu na masharti yanayopaswa kuwepo kabla ya hatua hazijachukuliwa na mwajiri kusitisha ajira kwa sababu husika.

Halikadhalika, katika makala zilizotangulia tulizungumzia kuwa suala la kusitisha ajira ni suala la mchakato ambalo unahusisha sababu za msingi na halali pia kufuatwa utaratibu wa haki. Leo tunaangalia namna sababu ya kusitisha ajira kutokana na utovu wa nidhamu inavyoweza kuwa halali.

Mambo Muhimu ya Kuzingatia ili kuhalalisha sababu ya Utovu wa Nidhamu

Ili utovu wa nidhamu uthibitike kama ni sababu halali ya kusitisha ajira ya mfanyakazi mbele ya sheria, mwajiri ni lazima ahakikishe yafuatayo;

 

  1. Endapo mfanyakazi amevunja kanuni za utendaji mahali pa kazi

Kama tulivyoeleza katika makala iliyopita umuhimu wa uwepo wa kanuni za utendaji mahali pa kazi. Kwamba kila mwajiri ni lazima awe ana kanuni za kuongoza utendaji bora mahali pa kazi. Hivyo suala la nidhamu linakuwa ni sehemu ya kanuni ambazo mfanyakazi anapaswa kuzizingatia. Katika kumchukulia hatua za kinidhamu mfanyakazi ni lazima ziwepo kanuni ambazo amekiuka.

  1. Endapo kanuni husika ni ya haki na msingi

Kanuni za utendaji bora mahali pa kazi ni lazima zionekane kuwa ni kanuni za haki wala si kwa ajili ya kuonea. Sheria inazitaka kanuni hizo kuwa zenye mantiki, zipo wazi wala si zenye utata wa maana, kwamba mfanyakazi anazijua au alipaswa kuwa anazijua, kwamba zimekuwa zikitumika mara kwa mara na kwamba kanuni iliyovunjwa adhabu yake mwafaka ni kusitisha ajira.

  1. Mfanyakazi awe amefanya aina ya vitendo vinavyoweza kusababisha kusitishiwa ajira

Kwa kawaida kosa la kwanza la mfanyakazi halipaswi kusababisha kusitishwa kwa ajira, mpaka pale itakapoonekana kuwa kosa husika lilikuwa kubwa kiasi cha kusababisha uhusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri kuharibika sana. Makosa ambayo yanaweza kuhalalisha kusitishwa ajira hata kama ni kosa la kwanza ni kwa mfano;

  • Kukosa uaminifu kwa mfanyakazi kwa kiasi kikubwa
  • Kuharibu mali ya mwajiri kwa makusudi
  • Kutishia usalama wa wafanyakazi wengine kwa makusudi
  • Uzembe uliokithiri
  • Kupigana na mfanyakazi mwengine au kushambulia mgavi, mteja au mwanafamilia wa mwajiri au mtu wa karibu wa mwajiri
  • Kudharau au kukwamisha kazi kwa makusudi

Endapo itathibitika kuwa sababu zilizotajwa hapo juu au mwenendo wa mfanyakazi uliooneshwa hapo juu basi mwajiri anayo haki ya kuchukua hatua za kinidhamu kutokana na sababu husika.

Mwajiri anapaswa kuhakikisha utaratibu au adhabu ya kisitisha ajira inatolewe kama vile ilivyowahi kutolewa katika siku za nyuma katika mazingira ya kosa lililofanana la wafanyakazi. Hii ina maana mwajiri hapaswi kubagua wafanyakazi wake, endapo yupo mfanyakazi alitenda makosa hayo hapo awali na adhabu ilikuwa ya kusitishiwa ajira basi hata mfanyakazi ambaye ametenda kosa hilo sasa adhabu yake iwe kusitishiwa ajira yake.

Hitimisho

Sababu ya utovu wa nidhamu inapaswa kudhibitishwa na mwajiri kwa kuhakikisha kanuni za utendaji bora mahali pa kazi zipo na zinatekelezwa ipasavyo kwa kufahamika na wafanyakazi ikiwa ni za haki. Ni muhimu kuhakikisha mwajiri unafuatilia sababu za kinidhamu na kuzitumia kama zilivyotumika kwa wafanyakazi wengine pasipo kubagua.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

 

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

 

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili.