Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Urithi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji  wa mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya njia mbalimbali za umiliki wa ardhi katika nchi yetu ya Tanzania. Leo tunakwenda kuanza mfululizo wa uchambuzi wa njia moja moja ambazo tulizianisha hapo awali. Karibu tujifunze.

Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Urithi

Urithi ni kitu chochote mtu anachokipokea kutoka kwa marehemu hasa pale panapokuwa na mahusiano ya kindugu au kinasaba baina ya mrithi na marehemu.

Ardhi ni mojawapo ya mali ambayo inaweza kurithishwa kama mali nyingine kutoka wa wazazi kwenda kwa watoto au kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine.

Sheria za mirathi iwe za kimila au serikali au zile za kidini zinatambua suala la marehemu kuweza kurithisha ardhi yake kama sehemu ya mali zake endapo atafariki dunia.

Katika mazingira ya utekelezaji wa mirathi ya marehemu kuhusiana na ardhi, mali ile itagawanywa kwa mujibu wa maelekezo ya marehemu endapo atakuwa ameacha wosia au kwa maelekezo ya mila, dini au utaratibu mwengine endapo hatokuwa ameacha wosia. Soma kwa kubonyeza hapa upate ufafanuzi zaidi kuhusu mirathi Sheria Leo.20: Ijue Sheria ya Mirathi.

Utaratibu wa Urithishaji wa Ardhi

  1. Marehemu lazima awe ni mmiliki halali wa ardhi ambayo inapaswa kurithishwa.

Hili ni jambo la msingi na muhimu sana kulizingatia ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara. Ili ardhi iweze kuhamishwa umiliki kutoka kwa marehemu ni lazima kwanza huyo marehemu awe mmiliki halali wa ardhi husika. Kumekuwa na migongano mingi hasa mtu anapofariki inawezekana eneo alilokuwa anakaa au familia yake inakaa sio lake bali alipewa kwa muda tu, anapofariki familia au watoto kwa kutokujua wanachukua hatua kuingiza eneo husika kwenye mirathi wakati halikuwa la baba au mama yao. Hivyo ni lazima ihakikishwe kuwa marehemu ni mmiliki halali wa eneo husika kabla halijaingizwa kwenye mchakato wa mirathi.

  1. Lazima kiwepo kifo cha mtu anayerithisha ile ardhi aliyokuwa anaimiliki.

Ardhi ya kurithishwa haiwezi kwenda kwa warithi pasipo kutokea kifo cha mwenye ardhi husika. Kifo ndicho kinatoa haki wa ndugu au watoto wa marehemu kuanza mchakato wa ugawaji na umiliki wa ardhi husika. Hatahivyo mazingira ya sasa kutokana na tamaa za watu, wamekuwa wakiua ndugu zao au wazazi ili wapate ardhi au mali nyingine ya urithi hii si tabia nzuri kwani mali hiyo haiwezi kuwa na manufaa endapo mrithi atakuwa kwa namna yoyote amehusika kusababisha kifo cha marehemu iwe kwa makusudi au kwa kupuuzia matunzo ya marehemu.

  1. Kufungua shauri la mirathi mapema

Baada ya kudhibitisha kifo cha marehemu ambaye alikuwa na umiliki wa ardhi au maeneo kadhaa, wanafamilia wanao wajibu wa kufungua shauri la mirathi katika mahakama yenye uwezo wa kusikiliza mashauri hayo. Mara nyingi mashauri hufunguliwa mahakama ya mwazo au mahakama kuu kulingana na ukubwa wa shauri na mali zinazohusika. Kumekuwa na tabia wanafamilia wengi kwa kujua au kutokujua wanaacha kufungua shauri la mirathi wakiogopa labla migogoro itajitokeza endapo wataanza mgao wa mali za marehemu. Hii ni dhana potofu na inaweza kusababisha migogoro zaidi hapo baadae na pia upotevu wa mali za marehemu kwa kuwa hazina msimamizi wa kisheria anayetambulika.

  1. Uteuzi wa msimamizi wa mirathi au mtekeleza wosia

Baada ya ufunguzi wa shauri na kuorodheshwa mali za marehemu ikiwa ni pamoja na mashamba au ardhi, mahakama inao wajibu wa kumteua msimamizi wa mirathi endapo marehemu alifariki pasipo wosia au mtekeleza wosia endapo marehemu aliacha wosia. Ni muhimu sana watu kuandaa wosia mapema ili kuepusha migogoro inayojitokeza baina ya ndugu wa kuzaliwa kwa kuwa kila mmoja angependa kupata eneo zuri kuliko mwenzake.

  1. Ugawaji wa ardhi kama urithi

Kazi ya msimamizi wa mirathi si kutumia mali au ardhi anavyotaka bali kugawa kwa warithi halali wa marehemu kulingana na taratibu za kisheria au kimila au kidini ikiwa hakuna wosia. Hali kadhalika mtekeleza wosia ana wajibu wa kugawa mali sawa na wosia unavyoeleza. Baada ya ugawaji wa mali ikiwepo ardhi basi ikiwa hakuna mapingamizi yoyote shauri la mirathi linafungwa rasmi na warithi kuchukua hatamu za umiliki wa maeneo au ardhi walizopewa kwa mujibu wa mirathi.

  1. Usajili wa ardhi kwa jina la mrithi

Hatua hii ya usajili wa ardhi ya urithi kwa jila la mrithi ni muhimu ili kuepusha migongano hapo baadae. Mrithi baada ya kupewa eneo lake katika mirathi ana haki zote za kubadilisha majina ya umiliki kutoka kwa jina la marehemu au kama ilikuwa chini ya msimamizi wa mirathi kwenda kwenye majina yake mrithi. Hii inamsaidia yeye na wengine ambao wanaweza kurithi kutoka kwake.

Hitimisho

Kama tulivyoweza kuchambua mchakato mzima wa umiliki kwa njia ya urithi unavyoweza kufanyika iwe ni ardhi iliyopatikana kimila au kiserikali muhimu mchakato ufuate taratibu zote za mirathi. Katika umiliki wa ardhi kwa njia ya mirathi kama sheria inavyofafanua na Katiba ya JMT ya 1977 kwamba watu wote ambao ni raia wa Tanzania pasipo kujali jinsia wanayo haki ya kurithi ardhi endapo haki hiyo itawaangukia kwa kufiwa na marehemu aliyewahusu mwenye ardhi au maeneo.

Muhimu zaidi ili kuepusha migongano ikiwa mtu unayo ardhi au maeneo kadhaa sehemu mbalimbali ni vizuri ukaandaa wosia kupitia wanasheria ili utakapofariki ardhi na mali nyingine ziweze kufahamika zilipo, zikusanywe na kugawiwa kwa warithi wako halali pasipo kupotea au kutumiwa vibaya.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili