23.C. Usitishaji wa Ajira kwa Utovu wa Nidhamu

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa Utovu wa Nidhamu sehemu ya 3. Karibu tujifunze.

Utovu wa Nidhamu

Katika makala iliyopita tuliweza kuangalia juu ya sababu ya kihalali inayoweza kusababisha mfanyakazi kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Tumechambua mambo ya msingi kabla ya mwajiri kuchukua hatua za kinidhamu kuhusu sababu ya msingi na uhalali wa sababu husika.

Leo tunaangalia sehemu cha utaratibu wa haki katika kuchukua hatua za kinidhamu kwa mfanyakazi mwenye tuhuma za utovu wa nidhamu mahali pa kazi.

Utaratibu wa Haki kushughulikia Utovu wa Nidhamu

Mara baada ya mwajiri kujirithisha kuwa kwa vitendo fulani vya mfanyakazi vinaashiria utovu wa nidhamu anapaswa kuchukua hatua stahiki kushughulikia hali hiyo. Hatua hizo zinaitwa utaratibu wa haki katika mchakato wa kushughulikia nidhamu mahali pa kazi.

Kabla ya kuchukua hatua za nidhamu dhidi ya mfanyakazi, mwajiri ni lazima afanye uchunguzi wa awali kujiridhisha iwapo ipo haja ya kuitisha kikao cha nidhamu. Endapo mwajiri ataona haja ya kuitisha kikao cha nidhamu anapaswa afanya mambo yafuatayo;-

  1. Kumpatia mfanyakazi taarifa ya tuhuma zinazomkabili kwa namna ambayo atazielewa kikamilifu tuhuma hizo.
  2. Mfanyakazi apewe na muda wa kutosha kuandaa utetezi kwa kuzingatia uzito wa kosa, muda usipungue saa 48.

 

  1. Mfanyakazi aelezwe wazi wazi juu ya haki yake ya kuwakilishwa na mfanyakazi mwenzake au kiongozi wa chama mahali pa kazi.

 

  1. Mwajiri anapaswa kuteua mwenyekiti wa kikao ambaye hajausika na suala lililosababisha kikao kiitiswe kusikiliza shauri hilo.

 

 

  1. Ushahidi wa mwajiri ni lazima uwasilishwe wakati wa kusikiliza shauri na ikiwa kuna nyaraka muhimu ambazo mwajiri anatarajia kuzitumia kudhibitisha tuhuma basi mfanyakazi anapaswa kupewa nakala zake na kuzihoji. Pia mfanyakazi anayo haki ya kuomba ripoti ya uchunguzi.

 

  1. Mfanyakazi apewe fursa ya kuita mashahidi na kuweza kuwahoji kwa maswali mashahidi wa mwajiri.

 

 

  1. Ikiwa matokeo ya kikao ni mfanyakazi kukutwa na hatia, adhabu haipaswi kutolewa papo hapo. Nafasi inapaswa kutolewa kwa mfanyakazi kuomba kupunguziwa adhabu kabla ya adhabu kutolewa.

 

  1. Endapo mfanyakazi mtuhumiwa ni kiongozi wa chama cha wafanyakazi katika ngazi yoyote, mwajiri ni lazima atoe nafasi kwa kiongozi huyo kuwakilishwa na mtendaji wa chama katika kikao cha nidhamu.

 

 

  1. Ikiwa adhabu inayotolewa ni kuachishwa kazi, mwajiri ni lazima atoe sababu na aeleze haki ya mfanyakazi kukata rufaa ngazi ya juu au kupeleka rufaa yake Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.

 

  1. Mfanyakazi ni lazima apewe nakala ya fomu ya kusikiliza shauri baada ya kikao cha nidhamu.

Hitimisho

Ndugu mdau wa ajira huu ndio utaratibu ambao unapaswa kufuatwa kwa ajili ya kushughulikia suala la utovu wa nidhamu. Ni muhimu sana kwa mwajiri kufuata utaratibu huu na pia mfanyakazi kuufahamu ili kuepuka madhara ya usitishaji wa ajira isivyo halali.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.