Mambo ya Msingi ili Mirathi itolewe

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Mambo ya msingi ili kutoa Mirathi

Katika makala zilizotangulia tumeweza kuangalia mambo kadhaa yanayohusu mirathi na juu ya urithi. Kila kitu kilichofundishwa kina msingi sana kwa kuweza kuelewa zaidi dhana ya mirathi na kuweza kuitumia katika maisha ya kila siku, kwani ni jambo lisiloepukika miungoni mwetu.

Hatahivyo, katika makala hii tunakwenda kujifunza mambo ya msingi ambayo yanaweza kusababisha mirathi itolewe au mchakato wa mirathi uanzishwe kwa mujibu wa sheria.

  1. Kudhibitishwa kifo cha mwenye mali

Ili mchakato wa mirathi uweze kuanzishwa ni lazima kiwepo kifo cha mtu mwenye mali ya mirathi. Sheria haitambui mirathi yoyote pasipo kifo cha mtu ambaye ana mali ambazo zinaweza kurithiwa na warithi wake halali. Endapo mtu atatoa mali zake kabla ya kifo chake utoaji huo hauwezi kuitwa mirathi bali ni zawadi kwa watu wake. Kifo kinadhibitishwa kwa uwepo wa cheti cha kifo kinachotolewa katika Mamlaka ya Vizazi na Vifo. Endapo cheti hakijapatikana basi hati ya kiapo cha mtu aliyeshuhudia kifo cha marehemu na maziko yake kinaweza kutumika. Mara nyingine wapo watu ambao wanapotea kwa muda mrefu kiasi kwamba matumaini kama wapo hai yanapotea, familia inaweza kufanya mchakato wa kuomba kutangazwa kwa kifo cha muhusika kupitia utaratibu wa kimahakama. Hii inaitwa dhana inayokanushika ya kifo ambapo mtu akipotea zaidi ya miaka 5 mahakama inaweza kumtamka kuwa marehemu.

  1. Uwepo wa warithi wa marehemu

Hatua muhimu katika mchakato wa mirathi ni uwepo wa warithi wa marehemu. Mirathi siku zote inaenda kwa warithi na si mtu mwengine. Hivyo warithi wanao wajibu wa kuchukua hatua muhimu mara baada ya kifo cha ndugu yao na kuanzisha mchakato wa mirathi.

  1. Uwepo wa mali

Msingi mkuu wa mchakato wa mirathi ni uwepo wa mali za kurithisha. Hii ni dhana ya kweli kabisa kwani hata kwa jamii za kawaida inafahamika endapo atafariki mtu masikini hutaona ndugu wengi wakijishughulisha na hatma ya familia hiyo, tofauti anapofariki mtu mwenye mali, wanajitokeza hata watu wasiohusika kutaka kudai haki kutoka kwake. Hivyo katika mchakato wa mirathi ni muhimu mali za marehemu zikafahamika na kuingizwa katika mirathi ili warithi halali waweze kupata mgao unaostahili.

  1. Barua za utekelezaji mirathi kutoka Mahakamani

Baada ya kukamilika kwa hatua au vigezo vitatu hapo juu, sasa ni hatua ya kufungua shauri la mirathi katika Mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mirathi. Endapo marehemu aliacha wosia basi mtekeleza wosia atadhibitishwa na mahakama ili kutimiza wajibu wake wa kutekeleza wosia. Wakati kwa upande mwengine, endapo marehemu hakuacha wosia, basi mahakama itamdhibitisha au kuteua msimamizi wa mirathi na kumpatia nyaraka zitakazomtambulisha katika kutimiza wajibu wake.

Hitimisho

Leo tumeweza kuangalia vigezo muhimu sana vya kutusaidia kujua hasa mchakato wa mirathi unahusisha mambo gani ya msingi. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua za kuorodhesha mali zetu na kuzitambulisha kwa warithi wetu mapema. Endapo tunahitaji kuzigawa mapema basi pia zinaweza kufanyika taratibu ili mali hizo zitolewe kama zawadi kwa wale tunaokusudia kuwapatia. Mali yoyote ambayo itabaki mara baada ya kufariki kwa mwenye mali itahesabiwa katika mchakato wa mirathi.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili