26. Usitishaji wa Ajira kwa sababu ya Utendaji Usioridhisha.
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa sababu ya uwezo mdogo wa kazi kutokana na Utendaji Usioridhisha.
Maana ya Utendaji Usioridhisha
Kama tulivyotambulisha kwenye makala iliyopita juu ya kusitisha ajira kutokana na uwezo mdogo, sababu mojawapo ni kutokuwa na Utendaji usioridhisha.
Utendaji wa mfanyakazi usioridhisha ni hali ya kiwango cha utendaji chini ya viwango vya kazi vilivyowekwa na mwajiri. Sheria ya ajira inatambua haki ya mwajiri kuweka viwango vya kazi, hivi ni viwango ambavyo wafanyakazi wanapaswa kuvizingatia katika utendaji wao.
Muhimu juu ya viwango vinavyowekwa na mwajiri ni kuwa vya haki na vinavyotekelezeka na kufahamiwa na mfanyakazi.
Sababu zinavyoweza kupinmwa kwa Utendaji usioridhisha
Sheria ya Ajira inaanisha vigezo vya sababu endapo mwajiri anataka kusitisha ajira kutokana na utendaji usioridhisha;
- Mwajiri ni lazima ajiridhishe endapo mfanyakazi ameshindwa kukidhi viwango vya utendaji vinavyotakiwa kufikiwa au la
Hapa mwajiri anapaswa kuchunguza kwa muda kama mfanyakazi ameshindwa kukidhi viwango. Msingi wa sababu ya kusitisha ajira ni katika uwepo wa kiwango vya kazi ambavyo mfanyakazi anastahili kuvitekeleza na iwapo ameshindwa kuvifikia.
- Endapo alikuwa na taarifa au ufahamu juu ya viwango vya utendaji kazi anavyostahili kuvifikia au la.
Mwajiri hawezi kuwa na haki ya kuchukua hatua ya kutumia sababu ya utendaji usioridhisha iwapo mfanyakazi hakuwa na taarifa juu ya viwango ambavyo alipaswa kutekeleza majukumu yake. Wakati wa kuajiriwa inashauriwa mwajiri kumwandikia kwenye mkataba au kumpa taarifa mfanyakazi juu ya majukumu anayopaswa kutekeleza na namna mwajiri atakavyokuwa anapima uwezo wa mfanyakazi katika kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa viwango. Kama mwajiri hajaweka viwango si sahihi kusitisha ajira ya mfanyakazi kwa sababu husika.
- Endapo viwango vya utendaji ni vya haki na vinatekelezeka au la
Wapo waajiri wengine wenye tabia ya kuweka viwango vya juu ya utendaji kiasi kwamba havilingani na taaluma au uwezo wa mfanyakazi kuweza kuvifikia. Viwango vya utendaji vinapaswa kuwa vya haki na kuzingatia uwezo na sifa za mfanyakazi husika.
- Je ni sababu zipi zimechangia au zinazochangia mfanyakazi kushindwa kufikia viwango husika.
Kuna nyakati uwezo wa mfanyakazi kushindwa kutimiza majukum yake ipasavyo kunatokana na mazingira ya kazi husika. Mwajiri anapaswa kuandaa mazingira rafiki na wezeshi kwa mfanyakazi ili aweze kupata kilicho bora kwa mfanyakazi husika. Zipo kazi zinahitaji mafunzo ya mara kwa mara na maelekezo, mfanyakazi akikosa kupata elimu kwa vitendo ni wazi utendaji wake unaweza usiridhishe. Hivyo lazima sababu husika zichunguzwe endapo zinatokana na uzembe wa mfanyakazi mwenyewe au mazingira yanayosababishwa na mwajiri au chanzo kingine.
- Endapo mfanyakazi alipatiwa nafasi ya kutosha ili kudhibitisha uwezo wake wa kufikia viwango vya utendaji au la
Ni muhumu kwa mwajiri kabla ya kuchukua hatua za kutumia sababu ya utendaji usioridhisha kumpatia mfanyakazi nafasi ya kuboresha utendaji wake. Mfanyakazi anaweza kupinga hatua za mwajiri kutumia sababu ya utendaji usioridhisha iwapo hatopatiwa nafasi ya kurekebisha au kuboresha utendaji wake.
Pamoja na kwamba mwajiri ana haki na uwezo wa kuweka viwango vya utendaji kazi mahali pa kazi, viwango husika ni lazima viwe vya msingi wa haki na vinavyoweza kufikiwa na mfanyakazi yeyote kwenye nafasi husika.
Hitimisho
Leo tumejadili mambo ya msingi katika kuangalia sababu ya usitishaji wa ajira kutokana na utendaji usioridhisha. Ni muhimu kwa mwajiri kuzingatia vigezo husika ili kuepusha mgogoro wa kiajira mara atakapochukua hatua kutumia sababu hiyo. Katika makala inayofuata tutajifunza juu ya utaratibu ambao mwajiri anapaswa kuutekeleza ili kusitisha ajira kwa mfanyakazi kutokana na utendaji usioridhisha.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili.