Nafasi ya Mwanamke katika Mirathi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Historia ya Nafasi ya Mwanamke katika Mirathi

Kama tunavyojua na tulivyoweza kueleza katika makala zilizotangulia juu ya haki ya kurithi ni ya watu wote yaani wanaume na wanawake alimradi tu mrithi ni halali yaani mwenye uhusiano na marehemu.

Suala la mirathi limekuwa kwa muda mrefu au kutokana na tamaduni, mila na miiko ya kijamii, likihusianishwa na watoto au warithi wa jinsia ya kiume kuliko wanawake. Mila nyingi na mtazamo wa watu wengi kuwa mrithi ni mtoto wa kiume pekee. Tamaduni hizi zimeshika mizizi sana katika familia na makabila mbalimbali. Dhana nii imeathiri hata masuala ya uzazi katika familia kiasi kwamba wazazi wa kiume na hata wa kike wanatamani kuwa na mtoto wa kiume yaani mtu atakayerithi na kuendeleza jina la ukoo fulani.

Mtazamo huu katika jamii ndio unaibua suala zima la kutazama nafasi ya mwanamke na historia yake katika nchi yetu juu ya mirathi.

Mtazamo wa Sheria kabla ya 1984

Kwa kuwa masuala ya mirathi kwa jamii kubwa ya makabila na tamaduni za nchi yetu ya Tanzania yalikuwa yakiongozwa na utaratibu wa mila, mwanamke hakuwa na nafasi ya kurithi mali ya mzazi wake haswa ardhi.

Ni mtazamo wa kitamaduni kuwa mwanamke akiwa mtu mzima atakwenda kuolewa na kuanzisha mji mwengine mbali na nyumbani hivyo kumrithisha mwanamke ardhi hasa ya ukoo utasababisha ardhi hiyo baada ya muda imilikiwe na wageni yaani wale waliooa mwanamke au wanawake wa ukoo fulani.

Mtazamo huu wa kimila ulikuwa ukiungwa mkono hata katika mashauri mbalimbali yaliyoletwa mahakamani na wanawake waliokuwa wakipinga mila za ubaguzi dhidi yao katika kipindi husika.

Hivyo mazingira ya utamaduni na kutolewa maamuzi ya mahakama kuunga mkono juu ya utamaduni wa wakati huo kulisababisha kwa kiwango kikubwa wanawake kupoteza haki zao za urithi.

Masharti ya mirathi juu ya wanawake

  • Mwanamke hana haki ya kurithi mali ya mirathi, bali atarithi ikiwa  marehemu hakuacha mtoto wa kiume
  • Kama mtu anafariki pasipo kuwa na watoto basi mali ile hairithiwi na mkewe bali inakwenda kwa ndugu zake wa kiume
  • Mwanamke au mtoto wa kike hawezi kurithi ardhi ya ukoo bali anaweza kuitumia tu
  • Mwanamke hawezi kurithisha ardhi hata kwa wosia ikiwa ni ardhi ya ukoo aliyoipata kwa urithi, bali itarudi kwa ukoo husika.

Hitimisho

Leo tumeangalia kwa sehemu mtazamo wa kitamaduni na kisheria kabla ya mwaka 1984 jinsi wanawake walivyokuwa wakibaguliwa kwa masharti magumu ya kuweza kurithi mali za wazazi wao hasa suala la ardhi. Mtazamo huu hasi umeendelea kuwepo kwa baadhi ya mila na tamaduni hata baada ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kufanyiwa marekebisho kupinga ubaguzi huo. Ni muhimu sana kuondokana na dhana hii dhaifu na kuwapatia urithi watoto wa kike kwa mujibu wa sheria. Katika makala inayofuata tutaendelea kuchambua nafasi ya mwanamke kwenye mirathi, usikose kufuatilia.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  1. Abubakar Juma
    Abubakar Juma says:

    shukrani kaka kwa makala zako nzuri, nimepata hii site leo, ila kuna vitu ving sana tumejifunza, nitaenedelea ukufuatilia kaka, je una facebook ac pia kwa ajili ya aya mambo?

Comments are closed.