Nafasi ya Mwanamke katika Mirathi -2

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Historia ya Nafasi ya Mwanamke katika Mirathi baada ya 1984

Katika makala iliyotangulia juu ya nafasi ya mwanamke katika mirathi, tuliangalia juu ya mtazamo hasi wa jamii kuhusu urithi kwa wanawake. Jamii yetu awali kutokana na mila na desturi zetu haimtazami mwanamke kama mrithi halali wa mali za marehemu hususani suala la ardhi.

Hatahivyo, mabadiliko ya 5 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ambayo yalifanyika mwaka 1984 yalibadili mfumo mzima wa sheria za nchi na hususani uwezo wa kumiliki mali kwa watu wote. Mabadiliko haya yaliruhusu kuingizwa kwenye Katiba tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataufa ‘ Universal Declaration of Human Rights’.

Mojawapo ya haki zilizoingizwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki ya kumiliki mali.

Katiba ya JMT inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anayo Haki ya kumiliki mali. Ibara ya 24 (1) ya Katiba ya JMT inasema

kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi ya mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria’

Haki hii ya Kikatiba imetolewa kwa kila mtu pasipo kujali jinsia au umri au nasaba alimradi mali hiyo ipatikane kwa njia halali.

Katika msingi huu wa mabadiliko sheria zilizotungwa kufuatana na haki hii iliyoainshwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ziliakishi matakwa haya ya Katiba.

Sheria ya Ardhi ya 1999 Kifungu cha 3 (2) inaeleza juu ya haki ya mwanamke kupata ardhi, kumiliki na kuitumia ni sawa na haki aliyonayo mwanaume yeyote katika nchi ya Tanzania.

Hali kadhalika mabadiliko hayo ya Katiba yalisaidia kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ndoa ya 1971 Kifungu cha 56 kwamba mke pia anayo haki ya kupata, kumiliki na hata kuitumia au kuuza kama vile mume alivyonayo.

Msimamo wa Sheria baada ya Mabadiliko ya Katiba ya 1984

  • Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 kupitia mabadiliko ya 5 ya 1984, Sheria ya Ndoa ya 1971 na Sheria ya Ardhi ya 1999 vinatilia mkazo juu ya haki ya mwanamke katika masuala ya mali na ardhi kuwa na haki sawa kama mwanaume.
  • Mwanamke anayo haki ya kurithi mali yoyote ya marehemu ikiwa ni mali inayohamishika au isiyohamishika yaani ardhi kama vile mwanamume alivyo na haki hiyo.

 

  • Mwanamke anayo haki ya kurithisha au kuuza mali ikiwa ni pamoja na ardhi aliyoipata kwa njia ya urithi
  • Mila zozote au tamaduni zinazombagua mwanamke katika suala la urithi juu ya mali ikiwepo ardhi ni kinyume cha sheria.
  • Iwapo mwanamke atanyimwa urithi kwa sababu ni mwanamke basi anaweza kupinga hatua hiyo kwa kufungua shauri mahakamani ili aweze kupata haki ya urithi.

Hitimisho

Leo tumeweza kuangalia sehemu ya 2 ya makala juu ya Nafasi ya Mwanamke katika Mirathi na jinsi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoeleza kwa kina juu ya haki hiyo ya kumiliki mali kupitia njia mbalimbali ikiwepo urithi, sheria ya Ardhi na Sheria ya Ndoa. Hivyo ni muhimu jamii yetu kutambua zama za kubagua wanawake au watoto wa kike katika suala la mirathi zimepitwa na wakati, watu wote ni sawa na wanayo haki sawa katika kupata mali ikiwa ni kwa njia ya urithi ama njia nyingine halali.

Mzazi usiache kupatia mtoto wako wa kike urithi katika mali zako au kumpatia mke wako urithi kwa kuogopa mtazamo wa watu kwani sheria inakutaka kuwatendea warithi wako kwa haki wakati wote.

Ili kuepusha migongano hii ya kimtazamo ni vyema kutumia wataalam wa sheria, wakusaidie kuandaa wosia wako vizuri na mapema.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili