26.B. Usitishaji wa Ajira kwa sababu ya Utendaji  Usioridhisha.

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa sababu ya uwezo mdogo wa kazi kutokana na Utendaji Usioridhisha.

Maana ya Utendaji Usioridhisha

Katika makala iliyopita tumeweza kuangalia maana ya utendaji usioridhisha kuwa ni aina ya utendaji wa mfanyakazi chini ya viwango vilivyowekwa na mwajiri.Uchambuzi wa Sheria.26. Usitishaji wa Ajira kwa sababu ya Utendaji  Usioridhisha.

Tukajifunza juu ya sababu zinazoweza kupimwa ili kuonesha juu ya kiwango cha utendaji wa mfanyakazi.

Katika makala hii ya leo, tunaenda kutazama utaratibu wa haki ambao mwajiri anapaswa kuuzingatia ili kuanzisha mchakato wa kusitisha ajira kwa sababu ya utendaji usioridhisha.

Utaratibu wa Haki wa Kusitisha Ajira kwa Utendaji usioridhisha

Sheria ya Ajira inaaisha juu ya utaratibu wa haki ambao mwajiri anapaswa kuzingatia endapo anakusudia kusitisha ajira ya mfanyakazi kwa sababu ya utendaji usioridhisha. Katika kuzingatia utaratibu huo, mwajiri anapaswa kufanya yafuatayo;-

  1. Mwajiri ni lazima afanye uchunguzi kujua sababu inayosababisha utendaji usioridhisha wa mfanyakazi

Hii ni hatua muhimu na ya kwanza ambayo mwajiri anatakiwa kuichukua. Mwajiri hapaswi kukurupuka na kuchukua uamuzi tu wa kusitisha ajira kwa sababu ya uzembe pasipo kufanya uchunguzi. Uchunguzi utasaidia pande zote kujua kiini cha utendaji usiofikia viwango. Kama tulivyoeleza katika makala iliyopita kuwa utendaji usioridhisha unaweza kusababishwa na mfanyakazi au mwajiri mwenyewe au mazingira ya kazi. Hivyo njia pekee ni kufanya uchunguzi ambao utamuhusisha na mfanyakazi husika.

  1. Mwajiri kutoa nafasi ya mfanyakazi kuboresha utendaji

Kabla mwajiri hajachukua hatua za kusitisha ajira ya mfanyakazi kwa sababu ya utendaji usioridhisha ni vyema kumpa mfanyakazi nafasi ya kuboresha utendaji wake. Hii inaweza kufanyika kwa kutoa semina au maelekezo au mafunzo ya ziada katika kazi. Suala la kutoa nafasi ya kuboresha utendaji inaweza isitolewe endapo mfanyakazi husika yupo katika ngazi ya uongozi au mahitaji ya kazi husika yanahitaji utaalam maalum kiasi kwamba hautaruhusu makosa ya mara kwa mara.

  1. Mwajiri anapaswa kutoa muda wa kutosha ili kuimarisha utendaji

Hii ni hatua muhimu sana kabla ya kuchukua hatua za kusitisha ajira ya mfanyakazi. Mwajiri anapaswa kutoa kipindi Fulani cha kumwezesha mfanyakazi kuboresha utendaji wake endapo itaonekana ana upungufu wa kazi zake. Si sahihi mara baada ya kubaini utendaji usioridhisha basi mwajiri anatakiwa kutoa muda kiasi wa mfanyakazi kuboresha utendaji.

  1. Mwajiri anaweza kutoa onyo ikiwa utendaji haujaimarika

Endapo itaonekana baada ya kutoa nafasi ya kujirekebisha na kuboresha utendaji na muda lakini bado utendaji wa mfanyakazi haujaimarika, mwajiri anaweza kutoa onyo kwa mfanyakazi husika, kwamba utendaji usipoimarika anaweza kusitishiwa ajira.

  1. Mwajiri anapaswa kuitisha kikao cha kusikiliza usitishaji wa ajira kwa utendaji usioridhisha

Endapo mwajiri ataona kuna haja ya kusitisha ajira kutokana na utendaji usioridhisha basi anawajibika kuitisha kikao na mfanyakazi. Katika kikao hiki mfanyakazi anaweza kuwakilishwa na mwakilishi

  1. Maamuzi ya mwajiri ya kusitisha ajira yanapaswa kuwasilishwa kwa maandishi

Mwajiri anapaswa kumwandikia mfanyakazi usitishaji wa ajira kutokana na utendaji usioridhisha kwa kuonesha sababu katika barua ya usitishaji wa ajira.

Hitimisho

Leo tumejadili juu ya mchakato wa usitishaji wa ajira kutokana na utendaji usioridhisha. Mchakato huu ni uratatibu wa haki ambao mwajiri anapaswa kuzingatia wakati wote. Waajiri wengi wanaingia kwenye mgogoro wa kiajira kwa kutofuata sheria au kuchukua hatua pasipo kuwa na sababu za msingi. Ni muhimu sana kufuata taratibu ili kuepusha uonevu kwa wafanyakazi na pia kuzingatia maslahi ya uzalishaji wa mwajiri.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.