Nafasi ya Mtoto wa Nje ya Ndoa katika Mirathi -1

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Historia ya Nafasi ya Mtoto wa nje ya Ndoa katika Mirathi

Katika masuala ya mirathi jambo mojawapo ambalo limekuwepo katika jamii na limeibua changamoto kubwa ni nafasi ya mtoto wa nje ya ndoa kurithi mali ya mzazi wake.

Suala hili limeibua migogoro ya kila aina kwenye familia mara baada ya misiba kujitokeza. Wenzi wengi wamekuwa si waaminifu katika kueleza wenzi wao endapo walikuwa na watoto au wamepata watoto wengine nje ya ndoa. Mara baada ya msiba masuala haya yanaibuka na kuleta mgongano wa familia nyingi za kiafrika.

Kwa kujifunza kutokana na historia ya mtazamo wa kisheria juu ya suala la mtoto wa nje ya ndoa na haki zake zinazoambatana naye katika suala la mirathi tunaweza kuepusha au kupunguza migogoro mingi katika jamii yetu.

Mtazamo wa Sheria kabla ya 2009

Kama utaratibu wa ugawaji au mwongozo wa mirathi unavyoanishwa katika sheria mbalimbali ikiwa ni zile za kimila, kislam au kikristo, zinaonesha kuwa mtoto wan je ya ndoa hakuwa na nafasi ya kurithi mali kutoka kwa mzazi wake.

Msingi huu ulisababisha watoto wengi ambao wamezaliwa nje ya ndoa kupata wakati mgumu wa kuendesha maisha yao hata kujua hatma yao kulingana na asili ya wazazi wao.

Mirathi ya Kiislam kuhusu mtoto wa nje ya ndoa

Kulingana na utaratibu wa mirathi kufuatana na dini ya Kiislam, inaeleza mtoto nje ya ndoa hawezi kurithi mali ya baba. Hii ni kwa sababu na inaaminika huyo ni mtoto wa mama husika na atapata urithi kutoka kwa mama yake. Hii inaendelea hata kama baba mtoto baada ya muda atakuja kuoana na mama wa mtoto husika. Mtoto atahesabika ni haramu kwa kigezo tu alizaliwa nje ya ndoa.

Hivyo basi msingi wa Koran kwa mzazi wa kiume ambaye angependa mtoto wake wan je ya ndoa apate urithi angeweza tu kufanya hivyo kupitia wosia. Katika dini ya Kiislam sheria inaongoza kuwa mwosia anaweza kuusia mali yake isiyozidi 1/3.

Mirathi ya Kikristo kuhusu mtoto wa nje ya ndoa

Mchakato wa mirathi ya wakristo unaongozwa na Sheria ya Urithi ya India ya 1865 ambayo inatumika hapa Tanzania. Katika sheria hii inaeleza kuwa mtoto wa nje ya ndoa hana haki ya kurithi mali ya baba yake. Mtoto huyo atahesabiwa katika urithi wa mali ya mama yake pekee.

Mirathi ya Kimila kuhusu mtoto wa nje ya ndoa

Hali kadhalika mtazamo wa sheria za kimila kuhusiana na mtoto wa nje ya ndoa ni kama ule ambao ulionekana katika sheria nyingine yaani hana haki ya kurithi kwa upande wa baba yake. Taratibu nyingine ili kumuhalalisha mtoto husika basi baba anapaswa kumtambulisha kwenye ukoo kama ni mtoto wake na taratibu za kiukoo kufuatwa. Katika mazingira hayo mtoto husika anaweza kuhesabiwa kama mtoto halali wa marehemu na kupata haki ya urithi.

Hitimisho

Leo tumeangalia historia ya nafasi ya mtoto wa nje ya ndoa kuhusiana na mirathi kwenye maeneo ya mirathi kidini na kitamaduni. Tumeona mtazamo huo na utekelezaji wake kwa watoto hawa kutopewa urithi kwa wazazi wao wa kiume yaani baba zao. Haki yao ya urithi iliishia tu kwa wazazi wao wa kike.

Tuendelee kuwa pamoja kuona nini kimetokea kwenye sheria ya mirathi na nafasi ya watoto wa nje ya ndoa mara baada ya kutungwa Sheria ya Mtoto ya 2009. Fuatilia makala zinazofuata uendelee kujifunza.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili