Mgawanyo wa Mirathi ya Kiislam

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Mirathi ya Kiislam

Mgawanyo wa mali kwa kufuata dini ya Kiislam ni mwongozo kwa wale wenye kuishi maisha kwa kufuata dini na mwongozo wa kiislam. Mgawanyo huu unatokana na Koran.

Mfumo wa ugawanyaji wa mirathi ya Kiislam unafuata sheria ya ukaribu wa ndugu na marehemu.

Msingi wa  Mgawanyo wa Mirathi ya Kiislam

 • Kwamba urithi si kwa ajili ya wanaume tu bali hata wanawake wanausika katika kurithi
 • Mali inayoachwa na marehemu hatakama ni ndogo itagawanywa kwa warithi halali kutokana na mgao wao kwa sheria za kiislam
 • Mirathi itahusu mali zote zinazohamishika na zile zisizohamishika
 • Suala la urithi na mirathi linajitokeza pale tu ambapo marehemu ameacha mali
 • Urithi unaenda kwanza kwa wale walio karibu kimahusiano na marehemu kuliko walio mbali kwa uhusiano.

Utaratibu wa mgawanyo wa mirathi

Kwa kawaida endepa marehemu ameacha mali ambayo inapaswa kugawanywa katika mirathi basi mali hiyo inaweza kuhusika katika kulipia

 • Gharama za mazishi
 • Madeni,
 • Kiasi cha 1/3 warithi kwa njia ya wosia
 • Kiasi cha 2/3 kugawiwa kwa warithi kutokana na mgao ulioainishwa kwenye Koran.

Ni muhimu kufahamu kwamba mtu ambaye anaamini katika dini ya Kiislam na mirathi yake kugawanywa kwa msingi wa imani hiyo ana uwezo wa kuusia kiasi cha 1/3 ya mali yake yote na si zaidi ya hapo. Sheria ya kidini inaeleza juu ya sehemu ya 2/3 ya mali ya mirathi ina warithi ambao wameanishwa tayari na haipaswi mali hiyo kutolewa kwa wosia.

Mfano wa mgao wa mirathi ya Kiislam

 • Endapo mume atafariki pasipo kuacha mtoto basi mke/wake atapata ¼ ya mali yote. Pale mume akifariki akiwa na watoto basi mke/wake watapata 1/8 baada ya kutoa mali ya watoto na kulipwa madeni.
 • Endapo mke atafariki pasipo kuacha mtoto basi mume wake atapata ½ ya mali ya mke. Pale ambapo mke ataacha watoto basi mume atapata ¼ baada ya kulipa madeni na 1/3 ya warithi wa mke yaani watoto.

Hitimisho

Leo tumeangalia mfumo wa mirathi kupitia dini ya Kiislam namna ambavyo Koran imeweka mfumo mzuri wa mgawanyo kwa kila mrithi halali. Ni muhimu kuzingatia kwa mtu mwenye imani ya dini ya kiislam kuusia kiasi cha 1/3 kwa wale ambao hawana haki ya moja kwa moja katika mali yake ili kuondoa mgongano baadae.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili