Mgawanyo wa Mirathi ya Kimila

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Mgawanyo wa Mirathi

Katika makala zilizotangulia tuliweza kugusia kuwa mgawanyo wa mali za marehemu unatokana na namna alivyoishi kabla ya kifo chake. Kwa msingi huo tuliweza kujua kuwa mirathi inaweza kugawanywa kimila, au kwa kufuata dini ya Kiislam na pia kwa kufuata sheria ya Bunge kwa wale wa dini ya Kikristo.

Mahakama au msimamizi wa mirathi wakati anasimamia mirathi ya marehemu ni lazima wajiridhishe juu ya mfumo wa maisha ambayo marehemu aliishi pamoja na familia yake.

Mirathi ya Kimila

Hii ni aina moja wapo ya mgawanyo wa mali ya marehemu kwa kufuata taratibu za kimila. Mgawanyo wa mirathi kwa njia za kimila zinaongozwa na Tangazo la Sheria za Kimila la 1963 ‘The Local Customary Law (Declaration) Order, 1963’

Mfumo wa mgawanyo wa mali kimila kwa nchi yetu ya Tanzania unafuata zaidi upande wa kiume, tofauti na makabila machache ambayo yanafuata upande wa kike. Hii ina maana walio na haki ya urithi zaidi ni warithi wa kiume.

Utaratibu wa Mgawanyo wa Mirathi

Endapo marehemu anafariki na kuacha watoto na wajane basi familia itaafanya maandalizi ya maziko na kuanza mchakato wa kushugulikia mirathi ya marehemu.

Kwa kawaida katika usimamizi wa mirathi kwa njia ya kimila, jukumu la usimamizi na mgawanyo wa mali anapewa kaka mkubwa wa marehemu au kama baba mzazi wa marehemu yupo basi ndiye mwenye wajibu huo.

Katika kutekeleza wajibu huo msimamizi wa mirathi ya marehemu atafuata utaratibu ufuatao.

  1. Kulipa madeni ya wadai

Wadai wa marehemu wanapewa kwanza kipaombele katika kulipwa madai yao. Katika kikao wadai wanapaswa kueleza kiasi wanachodai na kiasi husika kitalipwa kutoka katika mali za marehemu. Endapo mali za marehemu hazitoshi basi madai hao yatahamishiwa kwa warithi wake.

  1. Kugawa mali kwa warithi daraja la 1

Mgawanyo wa urithi wa kimila umegawanya warithi katika madaraja 3 yaani wapo warithi wa daraja la 1, 2 na 3. Daraja alilopo mrithi linaamua kiwango cha urithi atakachopata kutoka kwa marehemu.

Warithi wa marehemu daraja la 1 ni mtoto wa kiume wa nyumba kubwa ya marehemu. Huyu anahesabika kama mrithi mkuu, kiwango cha urithi wake ni maradufu ya kile wanachopata wenzake. Kama tunavyojua maisha ya kimila yanahusisha ndoa za mitala. Hivyo mtoto mkubwa wa kiume wa marehemu atapewa urithi zaidi ya wenzake.

  1. Kugawa mali kwa warithi daraja 2

Warithi wa daraja la 2 hawa ni watoto wa kiume wote katika nyumba zote za marehemu. Hawa watapewa urithi pungufu ya yule wa daraja la 1 lakini ni zaidi ya wale wa daraja la 3.

  1. Kugawa mali kwa warithi daraja la 3

Warithi wa daraja la 3 ni watoto wote wa kike wa marehemu wakiwa ni wa nyumba kubwa na zile nyingine. Hawa ndio wanapewa kiasi cha mali kilichobaki kama urithi kutoka kwa baba yao.

Mgawanyo huu wa majaraja unafuata hasa suala la watoto wa kiume. Endapo marehemu hakuacha mtoto wa kiume basi mtoto mkubwa wa kike atapata urithi katika daraja la 1 na wenzake watafutatia. Endapo marehemu ataacha mtoto wa kiume hata kama ni mdogo kwa dada zake bado atakuwa na haki ya kupewa urithi wa daraja la 1.

  1. Nafasi ya mjane/wajane

Katika mgawanyo wa mali za marehemu mjane au wajane kwa kufuata mila hawawezi kurithi mali ya mume wake. Wajane wanaachwa chini ya uangalizi wa watoto wao ambao wamepokea urithi kutoka kwa baba yao. Watoto wana jukumu la kuwatunza mama zao mpaka mwisho wa uhai wao.

Hitimisho

Leo tumeangalia mgawanyo wa mirathi kwa njia za kimila. Muhumu kufahamu kuwa mgawanyo huu unahusipa pale mke na mume wote wanafuata mila za kabila husika. Aina ya mgawanyo huu kwa sasa unapungua nguvu kutokana na hali ya makabila mbalimbali kuoana na hasa watu kuanza kufuata mfumo wa kidini katika maisha yao ya kila siku tofauti na mfumo wa kitamaduni. Hatahivyo tunaona changamoto ya mgawanyo huu ni ubaguzi kwa wanawake na watoto wa kike katika kutokupata urithi kwa mume au baba zao.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili