Nafasi ya Mtoto wa Kuasili kwenye Mirathi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu  kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Maana ya Mtoto wa Kuasili

Kuasili ni kitendo cha kufanya taratibu za kisheria kumdhibitisha mtoto ambaye si wa kumzaa kuwa mtoto wako kisheria. Sheria ya Mtoto ya 2009 inazungumzia juu ya watoto wanaoweza kuasiliwa. Kwa lugha ya kiingereza ni ‘adoption process’.

Dhana hii ya kuasili watoto imekuwepo tangu enzi. Hata hivyo katika mataifa ya magharibi imekuwa sehemu kubwa ya utamaduni wake. Familia nyingi zimekuwa zikiasili watoto kutoka maeneo mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na Afrika.

Sababu za kuasili watoto

Zipo sababu kadhaa ambazo zinaweza kuelezwa kuchangia kuasili kwa watoto katika maeneo mbalimbali

  1. Familia kukosa watoto wa kuzaa. Zipo familia mbalimbali pamoja na kujaliwa mambo mazuri lakini hawana watoto wao wa kuwazaa binafsi. Kiu ya kujenga familia na kulea watoto inawasukuma kutafuta watoto ambao watawaasili kuwa wao kisheria.
  1. Familia kutaka kusaidia hali za watoto walio katika mazingira magumu au hatarishi. Wapo watoto katika maeneo mbalimbali wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi kiasi kwamba ustawi wao unakuwa mashakani. Katika kuokoa watoto hao zipo familia zinazojitolea kuwaasili na kuwawekea mazingira ya makuzi kama watoto wengine.
  1. Watoto husika kukosa wazazi na ndugu wa karibu wa kuwatunza na kuwalea. Watoto ambao wanaingia katika vigezo vya kuasiliwa mara nyingi ni wale ambao hawana wazazi yaani ni yatima na hawana ndugu wa karibu wa kuwalea.

Nafasi ya Mtoto wa Kuasili kuhusiana na Mirathi

Ni mtazamo wa sheria kuwa mtoto wa kuasili kama alivyo mtoto wa asili yaani yule aliyezaliwa na wazazi husika anayo haki ya kurithi.

Kama tulivyoeleza katika makala iliyotangulia juu ya hadhi ya watoto na jinsi sheria inavyosisitiza haki ya kila mtoto ya kutokubaguliwa kutokana na hali yake. Vivyo hivyo kwa mtoto wa kuasili anachukuliwa na mzazi au wazazi husika waliomuasili kama mtoto wao wa kumzaa.

Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mtoto ya 2009 inaeleza wazi kuwa ‘mtu hatoruhusiwa kumnyima mtoto haki ya kufurahia au kutumia mali ya mzazi wake’

Kwa mtazamo huu wa kisheria mtoto yeyote anayo haki ya kurithi mali ya mzazi wake ikiwa ni baba au mama yake  wa kuasili pasipo ubaguzi wowote ule au kumtofautisha na watoto wale waliozaliwa kwa asili na wazazi husika. Mtazamo huu wa sheria ya Mtoto ya 2009 unaendana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inayoeleza kwenye Ibara ya 12 inayosema;

‘Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa’

Pia Sheria ya Mtoto ya 2009 Kifungu cha 3 kinaeleza wazi kuwa mtoto hapaswi kubaguliwa kwa namna yoyote ile kwa misingi ya jinsia, rangi, umri, dini, lugha, mtazamo wa kisiasa, hali ya afya yake, mila zake au kabila lake, mahali alipotoka, kuzaliwa kwake, hali yake ya kijamii na kiuchumi au kwa hadhi yake yoyote ile.

Katika tafsiri juu ya neno mzazi linahusisha mtu yule aliyezaa mtoto kwa asili yaani ‘biological parent’ na pia yule aliyemwasili mtoto kwa njia za kisheria yaani ‘adopting parent’

Ni muhimu kuzingatia kwa jamii yetu kuwa mtoto wa kuasili ana haki sawa juu ya mali za mzazi au wazazi wake wa kuasili kama alivyo mtoto aliyezaliwa na mzazi au wazazi husika kwa asili. Mtoto wa kuasili hapaswi kubaguliwa na mzazi au wazazi au ndugu na jamaa za wanafamilia kwa sababu tu yeye si mtoto wa kuzaliwa kama wengine. Dhana hii ya kuasili katika jamii yetu kwa kuwa si ya muda mrefu na matumizi yake si ya kawaida sana, watoto hawa wanakuwa katika changamoto ya kutokukubaliwa na familia au jamii husika.

 

 

Hitimisho

Leo tumeangalia tena kwa undani juu ya Nafasi ya Mtoto wa Kuasili katika sula la mirathi. Tumeona haki zake ni kama zile za mtoto wa kuzaliwa katika familia husika. Kama familia imepata mtoto kwa njia ya kuasili basi inapaswa kuzingatia masharti na mwongozo wa kisheria kuhusu haki za mtoto husika ikiwepo na haki ya urithi kama watoto wengine. Kwa mtazamo huu mtoto wa kuasili anapata haki ya kurithi kwa wazazi wake waliomuasili na si kwa wazazi wake waliomzaa.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili