27.A. Usitishaji wa Ajira kwa sababu ya Ugonjwa au Kuumia

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa sababu ya uwezo mdogo wa kazi kutokana na Ugonjwa au Kuumia.

Maana ya Utendaji Ugonjwa ua Kuumia

Uwezo mdogo katika utendaji kazi unaweza kusababishwa na hali ya ugonjwa au kuumia kwa mfanyakazi. Mfanyakazi anaweza kuwa katika hali bora kabisa wakati wa kuajiriwa na kuendelea kutimiza majukumu yake kama kawaida. Hatahivyo, hali inaweza kubadilika pindi ugonjwa au kuumia kunapotokea kwa kiwango cha kuathiri utendaji wa kazi wa mfanyakazi.

Sheria ya Ajira inatambua kuwa yapo mazingira ambayo ajira inaweza kusitishwa kutokana na hali ya ugonjwa au kuumia kwa mfanyakazi. Katika kutumika kwa sababu hii, sheria inamtaka mwajiri kuchukua kila hatua kwa msingi wa kusaidia mfanyakazi aendelee kuwepo kazini, hatua ya kusitisha ajira liwe ni jambo la mwisho kabisa kama hakuna mbadala au hatua nyingine za kusaidia mahusiano ya kiajira kuendelea.

Jinsi ya kuchunguza sababu ya kusitisha ajira kwa ugonjwa au kuumia

Kabla mwajiri hajachukua hatua za kusitisha ajira kutokana na sababu za ugonjwa au kuumia ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo;-

  1. Chanzo cha kuumia au ugonjwa.

Mwajiri anapaswa kuchukua hatua za kuchunguza chanzo cha kuumia au ugonjwa. Maeneo mengine ya kazi yamekuwa chanzo kikubwa cha wafanyakazi kupoteza uwezo wao wa kufanya kazi. Waajiri wamekuwa wakiwatelekeza wafanyakazi hawa. Hivyo sheria inamtaka mwajiri kuchunguza chazo cha ugonjwa au kuumia ikiwa vina uhusiano na kazi au la.

  1. Kiwango gani cha uwezo wa utendaji wa mfanyakazi uliopungua

Ni muhimu kujiridhisha kiwango cha utendaji wa mfanyakazi uliopungua. Ugonjwa au kuumia kunaweza kupunguza uwezo wa mfanyakazi au la. Ni kazi ya mwajiri kuangalia kiwango gani cha mfanyakazi kimeathiriwa katika kutimiza majukumu yake.

  1. Endapo ugonjwa au matokeo ya kuumia ni ya muda mfupi au muda mrefu.

Yapo mazingira yanayowezesha ugonjwa au hali ya kuumia ikawa ni ya muda mfupi au muda mrefu. Muhimu ni uchunguzi makini kupitia wataalam yaani Madaktati ambao wanaweza kutoa majibu juu ya kiwango cha kuumia au ugonjwa na athari zake kwa muda.

  1. Mwajiri anapaswa kuangalia uwezekano wa kuendeleza ajira ya mfanyakazi katika hali aliyonayo.

Kipaombele cha Sheria ya Ajira ni kuhakikisha mahusiano ya kiajira baina ya mfanyakazi na mwajiri yanaendelea kwa kadri inavyowezekana pasipo kuathiriwa na hali ya ugonjwa au kuumia.

  1. Kuwepo kwa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi au pensheni

Mwajiri ni muhimu kujiridhisha juu ya uwepo wa fidia au pensheni ambayo inaweza kumfaa mfanyakazi endapo atalazimika kusitisha ajira kutokana na hali ya ugonjwa au kuumia. Kwa sasa sheria ya Mfuko wa Fidia kwa ajili ya wafanyakazi tayari umeanza kufanya kazi na waajiri wanawajibika kuchangia kiasi katika mfuko huo wa fidia.

 

Muhimu kuzingatia katika kufanya uchunguzi juu ya hali ya mfanyakazi, mwajiri ni lazima aongozwe na ushauri wa Daktari ili kubaini kiwango cha uwezo na iwapo ni wa muda mfupi au mrefu.

Ikiwa sababu ya ugonjwa au kuumia ni matokeo ya kazi anayofanya mfanyakazi yaani ameumia kazini au kapata ugonjwa akiwa kazini basi mwajiri ana wajibu mkubwa zaidi kuhakikisha analinda mahusiano ya kiajira baina yake na mfanyakazi.

Hitimisho

Katika mahusiano ya kiajira baina ya mwajiri na mfanyakazi wakati mwengine yanakutwa na changamoto ikiwa ni ugonjwa au kuumia kwa mfanyakazi. Sheria inaweka kipaombele cha kuhakikisha mahusiano haya yanalindwa hatakama changamoto hii imejitokeza. Suala la kusitisha ajira kutokana na ugonjwa au kuumia ni hatua ya mwisho kabisa.

Tuendelee kufuatilia mfululizo wa makala hizi kujifunza juu ya taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kusitisha ajira kutokana na kuumia au ugonjwa.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.