DARASA LA ULIZA SHERIA 2018

Maono

Kuwa kituo cha kwanza cha kutoa maarifa mbalimbali ya kitaaluma ili kuleta ufanisi, tija, manufaa kwa jamii.

Dhima

Kwa nidhamu, uadilifu na weledi tunaweza kufikia maono ya kutoa maarifa kwa jamii.

Misingi ya Darasa

  • Uadilifu
  • Kujifunza
  • Huduma bora kwa wateja

Malengo

  • Kutoa elimu ya sheria kwa jamii ili kuisaidia kutatua changamoto za kila siku za kisheria.
  • Kutoa ushauri kwa wanajamii ambao utawasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kisheria kila wakati.
  • Kusadia Taifa letu kupunguza migogoro ya mara kwa mara kwa wanajamii kupitia elimu ya sheria na ushauri wa kisheria.

 1.0. Utangulizi

Mtandao wa Uliza Sheria ulianza rasmi mnamo mwezi Augusti 2017. Hata hivyo shughuli za Uliza Sheria za utoaji wa elimu ya kisheria na ushauri wa masuala ya kisheria zilianza tangu mwaka 2010 katika ngazi mbalimbali. Mnamo mwaka 2009/2010 waanzilishi wa Uliza Sheria walianzisha Taasisi isiyo ya kiserikali ya msaada wa kisheria iliyoitwa Community Legal Service Centre iliyofanya kazi kati ya mwaka 2009 – 2012. Taasisi hii ilitoa ushauri na msaada wa kisheria hasa kwa wakazi wa Dar es Salaam. Pia waanzilishi kwa nafasi mbalimbali wamekuwa wakitoa elimu ya sheria kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria ambao wanachukua masomo ya Shahada ya Sheria kati ya mwaka 2010 – 2015. Pia kazi za waanzilishi wa Uliza Sheria zimesambaa katika vyuo mbali mbali kwa ajili ya kutoa maarifa kwa wanafunzi wa sheria wa ngazi tofauti.

Uliza Sheria imekuja kutokana na changamoto pana ya uhitaji wa elimu ya sheria kwa jamii nzima. Hapo awali maarifa ya sheria yalikuwa yanatolewa kwa wanafunzi  wa sheria peke yao. Huduma hii haikuweza kukidhi haja kubwa iliyopo kwa jamii ndipo taasisi ikaja na mfumo wa kutoa maarifa kwa jamii pana zaidi ili kusaidia wananchi kuishi kwa mujibu wa sheria.

Kwa takribani kipindi cha miezi 4 tangu Uliza Sheria ianze kutoa mafunzo kwa jamii pana kupitia blog ya www.ulizasheria.co.tz tumeona mafanikio makubwa na kiu ya wananchi kutaka kujifunza zaidi juu ya masuala mbalimbali ya kisheria ambayo wanakutana nayo kila siku. Changamoto kubwa tuliyokutana nayo ni kupata maswali mengi na simu nyingi zikitaka ufafanuzi wa masuala ambayo tunaandika mara kwa mara.

Hivyobasi, uliza sheria imeandaa mpango wa kutoa mafunzo kupitia Darasa la Sheria ambalo litaendeshwa kupitia group ya watsapp kwa watu wote wanaopenda kujifunza zaidi kuhusiana na sheria ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi wakati wote.

1.1. Kwa nini Darasa Uliza Sheria

Zipo sababu kadhaa ambazo ni muhimu kwako ndugu msomaji za kukuwezesha kujiunga na Darasa la Uliza Sheria. Katika maisha kabla ya kuchukua uamuzi wowote ni muhimu sana kufanya tathmini ya kina ili kuona manufaa ya uamuzi wako kwa sasa na baadae. Hapa nitakutajia baadhi ya faida za wewe kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

  • Kupata maarifa ya kisheria kila siku. Hii ina maana utakuwa na fursa ya kujifunza juu ya sheria kila siku katika mwaka yaani siku 365.
  • Kupata fursa ya kuuliza maswali ya kisheria kutokana na masomo husika na kujibiwa na wanasheria katika Darasa
  • Kupata nafasi ya mjadala juu ya mada mbalimbali za kisheria siku moja katika wiki.
  • Kupata fursa ya ushauri wa kisheria katika mambo mbalimbali unayokabiliana nayo.
  • Kupata kipaombele katika kutatua changamoto za kisheria ambazo zinahitaji huduma ya wanasheria.
  • Kupata fursa ya kujifunza kutokana na uzoefu wa watu wengine kwenye Darasa la sheria.

Hizi ni baadhi tu ya faida au huduma utakazopata ndani ya Darasa la Uliza Sheria kwa kipindi cha mwaka mzima.

1.2. Vigezo vya kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

Je, ni vigezo gani vya kukufanya wewe kuwa msomi wa Darasa la Uliza Sheria?

Uliza sheria imeandaa utaratibu wa vigezo na masharti ambayo mtu anapaswa kuzingatia ili kujiunga na Darasa la Uliza Sheria.

  • Msomi wa uliza sheria angalau awe ana umri kuanzia miaka 18 na kuendelea
  • Msomi awe na uwezo wa kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili
  • Msomi kuzingatia kanuni na masharti ya Darasa la Sheria wakati wote
  • Msomi kulipia ada/gharama za mafunzo kabla ya kuunganishwa kwenye Darasa la Sheria
  • Msomi kuzingatia matumizi bora ya lugha na matumizi ya tija katika mtandao. Hii ni kuepuka lugha za matusi, kejeli au ubaguzi wa aina yoyote ile au uvunjifu wa amani na Sheria za Nchi.

Haya ni baadhi ya masharti muhimu ya kuzingatia ili msomi akidhi vigezo vya kujiunga na Darasa la Sheria.

1.3. Gharama za Kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

Je, ni kiasi gani msomi wa sheria anapaswa kulipia kama ada ya mafunzo?

Katika mfumo wowote wa kutoa elimu duniani zipo gharama. Gharama hizi unaweza usizione kwa kuwa zinaweza kubebwa na Serikali au Taasisi nyingine lakini haiondoi ukweli kuwa zipo gharama. Gharama za elimu zinatofautiana kutokana na kiwango cha elimu husika na thamani ya elimu kwa wale wanaoipokea.

Uliza Sheria kwa kuzingatia umuhimu wa huduma hii ya elimu na mengineyo yanayoambatana nayo imefanya tathmini na kuweka kiwango cha ada ambacho kila mmoja mwenye kutaka kujifunza anaweza kumudu kulipia gharama hizo.

Uliza sheria imeweka kiwango cha ada/gharama ya mafunzo ya sheria kiasi cha Tsh.60,000/- kwa mwaka kwa kila msomi mwenye nia ya kujiunga na Darasa la Sheria.

Lengo la kuweka gharama ni kuhakikisha kazi hii inapatiwa thamani kwa wale wanayoipokea na kufidia kwa kiasi kigodo gharama za maandalizi ya masomo na kazi nyingine za mtandao wa uliza sheria.

Ada hii italipwa mara moja yaani kwa mkupuo mmoja wakati wa kujiunga na Darasa la Uliza Sheria.

1.4. Ratiba ya Siku katika Darasa la Uliza Sheria

Kama tulivyoeleza awali nia ni kutoa maarifa ya kisheria kila siku kwa wasomi wa sheria. Hivyo uliza sheria imeandaa utaratibu wa kila siku wa namna maarifa na shughuli za darasa zitakavyoongozwa.

  • Kila asubuhi kutumwa somo/makala ya siku kwenye group ya Darasa la Uliza Sheria
  • Wasomi kujisomea makala na kuuliza maswali na kutaka ufafanuzi juu ya somo la siku husika
  • Waalimu kujibu maswali na kutoa ufafanuzi wa somo husika kwa siku
  • Wasomi wanaweza kuuliza maswali kutokana na makala za uliza sheria zilizowahi kuchapishwa.
  • Kutakuwa na saa 1 kwa siku kwa ajili ya kujibu maswali na kutoa ufafanuzi juu ya hoja mbalimbali kutokana na maswali ya wasomi.
  • Katika siku 1 kwa juma kutakuwa na mada maalum ambayo waalimu watajadili na wasomi katika kipindi cha masaa 2.

1.5. Je, unaweza kunufaika na uliza sheria pasipo kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

Jibu lake ni NDIO bado ndugu msomaji unaweza kunufaika na huduma za uliza sheria hata kama hujajiunga na Darasa la Uliza Sheria. Ikiwa hapo awali ulikuwa ukipata makala kwenye blog ya www.ulizasheria.co.tz basi makala hizo zitaendelea kuwepo. Pia kama ulikuwa ukipata kwa njia ya e-mail au watsapp basi utaendelea kuzipata kila siku.

Hatahivyo, nafasi ya kuendelea kupata huduma za kujibiwa maswali au ushauri zitaratibiwa sawa na maelekezo yaliyopo kwenye blog ya www.ulizasheria.co.tz juu ya kuandika maswali yako kwa njia ya e-mail.

Hivyo wewe uliyekuwa unapata makala na elimu kama hapo awali usihofu kwani utaendelea kupata. Mpaka sasa zipo zaidi ya makala 130 tayari zimechapishwa tangu mwezi Augusti 2017, unaweza kuzipitia zinazohusu masuala ya sheria za kazi, Katiba, Ardhi, Mirathi n.k. utaweza kusoma makala hizo kupitia ukurasa wa;

  • Sheria Leo
  • Elimu ya Sheria

1.6. Masomo katika Darasa la Uliza Sheria

Sheria ni msitu mnene sana hata kwa wanasheria wenyewe. Yapo mambo mengi na karibu mambo yote kwenye maisha yana sheria zake. Hatahivyo kutokana na uzoefu, utafiti tuliofanya katika kipindi cha zadi ya miaka 10 katika taaluma hii ya sheria tumeona maeneo ya msingi ambayo jamii inakabiliana nayo siku kwa siku.

Maeneo haya ya kisheria ambayo tumeyaainisha kushirikiana kwa mwaka 2018 ndiyo maeneo ambayo yana migogoro mingi sana mahakamani. Mojawapo ya sababu kubwa ya migogoro hii kuwepo mahakamani ni ukosefu wa elimu sahihi kwa wananchi.

Hivyo masomo yatakayoendeshwa katika Darasa la Sheria yatahusisha sheria zifuatazo;

  • Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
  • Sheria za Ardhi
  • Sheria za Mirathi
  • Sheria za Mikataba
  • Sheria za Kazi
  • Sheria za Jinai
  • Sheria za Biashara/Makampuni
  • Sheria za Familia (Sheria ya Ndoa na Mtoto)

Haya ni maeneo muhimu ya kisheria ambayo yatahusishwa kujadiliwa siku kwa siku na katika mada za wiki katika mwaka wa 2018.

1.7. Namna ya Kujiunga na Darasa la Uliza Sheria

Kama tulivyoeleza awali juu ya vigezo na masharti ya mtu kujiunga na Darasa, kimojawapo ni kulipia ada ya mwaka kiasi cha Tsh.60,000/- . Ada hii italipwa mara moja tu yaani kwa mkupuo mmoja.

Darasa la Uliza Sheria limekusudia kuanza rasmi tarehe 1/1/2018. Hivyo ni muhimu kuanza kulipa mapema ili kuunganishwa kwenye group ya watsapp.

  • Endapo msomi atalipia ada kabla ya tarehe 1/1/2018 atapata punguzo la kiasi cha Tsh.10,000/- hivyo atalipia ada ya mwaka kwa 50,000/-
  • Ada itaanza kuhesabika tangu tarehe 1/1/2018.
  • Endapo msomi atajiunga ndani ya mwezi Januari 2018 ada yake itaanza kuhesabika tangu 1/1/2018. Kama akijiunga tarehe yoyote Februari 2018 basi ada yake itaanza kuhesabika tangu tarehe 1/02/2018. Hivyo mwaka wa msomi utaanza kuhesabiwa ndani ya mwezi husika uliolipia ada.

Utaratibu wa kulipa ada

Kwa sasa ada zote zitalipiwa kupitia mawasiliano ya simu kwa tigopesa0713 888 040 yenye majina ya ISAACK DAWSON ZAKE. Mara baada ya kulipia ada husika. Tuma majina yako, kwenye namba hiyo ya 0713 888 040 kwa ujumbe wa watsapp nawe utaunganishwa kwenye Darasa la Uliza Sheria.

Karibu sana kwenye Darasa la Uliza Sheria tujifunze kwa pamoja kwani kujua sheria ni haki yako na kujifunza sheria ni wajibu wako.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Karibu sana.

Isaack Zake, Wakili

Zake Advocates.

www.ulizasheria.co.tz