Changamoto ya Mali ya Pamoja kwenye Mirathi.

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Maana ya Mali ya Pamoja

Mali ya pamoja ni kitu au vitu ambavyo vinamilikiwa na zaidi ya mtu mmoja. Yapo mazingira mbalimbali ambayo yanaweza kusababisha upatikanaji wa mali ya pamoja yaani mali inayomilikiwa na zaidi ya mtu mmoja. Katika makala zilizotangulia tumekuwa mara kwa mara tukigusia mirathi ambayo inahusu mali ya marehemu. Hata hivyo zipo changamoto zinazojitokeza endapo marehemu alikuwa ana umiliki kwenye mali ambayo ana mbia au wabia katika mali hiyo.

Mazingira ya umiliki wa mali ya pamoja

Ipo mifano mingi ya umiliki wa mali ya pamoja ambapo watu wanaweza kuipata na kuimiliki kwa pamoja. Mfano wa mazingira hayo ni kama ifuatavyo;

  • Mali ya pamoja inaweza kupatikana kutokana na juhudi za watu katika kazi fulani, na wakaamua mali husika iwe yao pamoja.
  • Mali ya pamoja kutokana na urithi. Pia yapo mazingira ambayo watu wanaweza kupata mali ya pamoja ikiwa wamerithishwa mali hiyo kwa pamoja.
  • Mali ya pamoja kutokana na ubia kwenye kampuni au biashara. Katika nyakati za sasa na kutokana na utendaji wa kazi kuhusisha uundwaji wa makampuni tumeona watu wengi wakiungana kuweka mtaji na nguvu za pamoja katika kufanya biashara au kuunda makampuni.
  • Mali ya pamoja kutokana na uwepo wa ndoa. Kwa mujibu wa sheria ya Ndoa ya 1971 wanandoa wanaweza kuwa na mali zao kabla ya kuona na pia ndani ya ndoa wanaweza kuwa na mali za pamoja au za tofauti kama watakavyokubaliana.

Katika mifano hii ya umiliki wa mali ya pamoja, eneo mojawapo linaloleta changamoto hasa katika masuala ya mirathi ni mali za wanandoa. Maeneo mengine ni rahisi kama marehemu ameacha maagizo au wosia kuweza kujua kiasi cha umiliki wake na kuweza kurithishwa kiasi hicho ikiwa ni kwa njia ya hisa au maslahi fulani kutokana na kiwango cha umiliki.

 

Mali ya Pamoja katika Ndoa na Athari zake katika Mirathi

Sheria ya Ndoa ya 1971 kama inavyoeleza kuwa inatambua kila mwanandoa anaweza kupata mali kabla ya ndoa na hata baada ya ndoa. Tumekuwa mashuhuda hasa pale ndoa inapofikia tamati kwa njia ya talaka tunaona pande zote wanagawana mali zile walizochuma kwa pamoja.

Hata hivyo, changamoto inakuja kwenye ndoa pale ambapo mmojawapo anafariki hasa inapokuwa mwanaume, suala la mali na mchango wa mke katika upatikanaji wa mali husika linaonekana kusahaulika. Mara nyingi mali zile zote ambazo aliacha mume na zile ambazo mke ameshiriki kuzizalisha bado zinaingizwa katika mgao wa mirathi. Hivyo mwanamke anajikuta mali ambazo ana haki nazo katika kuzichuma kwenye ndoa yake zinaingizwa katika mgao wa mirathi huku yeye akiwa bado yu hai.

Hii ni changamoto kubwa sana na wapo wajane wengi wamedhulimiwa uhalali wa mali zao kuingizwa katika mgao wa mirathi za mume pasipo wao kutambua au kupata utetezi wowote.

Mambo ya kufanya kuepuka athari husika

  1. Wanandoa kuwa na tathmini ya mali zao binafsi na zile za pamoja

Pamoja na kwamba baada ya ndoa watu wengi wanachukulia mali zote ni zao kwa pamoja, lakini upo umuhimu wa kujua asili ya mali husika ni nani aliyeizalisha zile zilizopatikana kabla ya ndoa. Pia wanandoa kila mmoja wapo anaweza kupata mali yake binafsi kutokana na shughuli zake. Ni muhimu kukubaliana juu ya mali zinazopatikana kwa juhudi za pamoja na zile binafsi na namna ya kuzishughulikia.

  1. Wanandoa kuandika wosia wa pamoja

Hii imekuwa changamoto kubwa kwa wanandoa wengi kutokuchukua hatua hii kwa pamoja. Wengi hawaandiki wosia, na endapo wanaandika basi wanafanya kwa kificho pasipo kumtaarifu mwenzi. Wengi wa wanandoa wanakuja kufahamu juu ya wosia wa wenzi wao baada ya kifo chao. Hii ina athari kubwa kwani unaweza kukuta marehemu ameusia mali isiyo yake bali ya mwenzi wake na mwenzi aliyebaki hana namna ya kudhibitisha juu ya mali husika kuwa yake.

Ili kuepuka changamoto hii ni vyema wanandoa wakashirikishana na kuandika wosia wa pamoja juu ya mali zao endapo mmoja wapo atatangulia basi mwengine aendeleze mali husika na yeye azigawe kwa warithi wao halali.

  1. Wanandoa kuandikisha mali katika majina yao kwa pamoja

Kumekuwa na utaratibu uliozoeleka wa wanandoa wengi ingawa mali ni ya pamoja kutumia jina la mmoja wao kama mmiliki. Tumeshuhudia mke anaweza kuwa amenunua kiwanja mume akajenga lakini hati ya kiwanja ikaandikwa jina la mume. Pasipo kujua hali ya baadae endapo kifo kitajitokeza warithi wa mume wanaweza kuleta changamoto pasipo kujua historia ya eneo husika kuwa mke alihusika katika ununuzi. Njia pekee ya kusaidia mwenzi kubaki na uhalali juu ya mali waliyopata pamoja.

Hitimisho

Mali zinazopatikana kwa pamoja zina changamoto endapo zimepatikana katika ndoa na mwezi anafariki pasipo wosia. Hali hii inasababisha mbia katika mali husika kukosa haki zake hasa pale ndugu na warithi wengine wanapodhani kuwa mali husika ni ya marehemu peke yake. Wanandoa wanapaswa kuchukua taadhari za kisheria kuhakikisha mmoja wapo hapotezi haki zake.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

karibu kwenye Darasa la Uliza Sheria 2018 jiandikishe sasa kupitia link hiiDARASA LA ULIZA SHERIA 2018

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili