Mambo yanayoweza Kunyima mtu Urithi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Haki ya Urithi

Kama tulivyoona katika mfululizo wa makala zilizopita katika kuzungumzia masuala ya mirathi, sehemu kubwa tumeeleza juu ya haki ya warithi halali na namna ya kuwawekea mazingira kwa wosia ili waweze kurithi mali ya marehemu. Katika mgawanyo wa aina za mirathi tumeona mirathi zinazofuata dini ya kikristo na kiislam pia mirathi kwa misingi ya mila. Aina hizi zote zinaelekeza katika kutambua walio warithi halali wa marehemu ili wapatiwe haki yao kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo katika suala la haki ya kurithi kwa marehemu yapo mazingira ambayo yanaweza kusababisha mrithi halali kunyimwa haki ya urithi na marehemu. Vipo vitu au matukio yanayoweza kusababisha mwosia kumwondoa mrithi wake katika urithi hata kama ni mtoto au mtu anayepaswa kumrithi kwa mujibu wa sheria za kimila au taratibu nyingine zozote.

 

Mazingira yanayosababisha kuondolewa kwa haki ya urithi

Katika mfumo wa mirathi kufuata mila, sheria za kimila na taratibu za mirathi zinaeleza juu ya mwosia kuwa na haki ya kumwondoa mrithi katika urithi wake. Sababu hizo ni kama ifuatavyo;

  1. Endapo mrithi ametenda vitendo vya zinaa na mke wa mwosia

Kama tunavyofahamu mfumo wa familia za kimila zinaweza kuhusisha ndoa ya wake wengi. Hivyo endapo mtoto wa mwosia akalala na mama yake mzazi au mama mdogo yaani mke mdogo wa baba yake basi baba ana haki ya kumwondoa mtoto husika katika haki ya kumrithi. Kitendo hiki ni cha kuchukiza na hakifai na mara nyingi adhabu yake ni kutengwa na familia au ukoo. Katika mila za kiafrika mahusiano ya karibu yaani ya ndugu au mtoto kwa mzazi hayakubaliki kabisa hivyo mtu anaweza kupoteza haki yake ya urithi kama adhabu.

  1. Endapo mrithi amefanya jaribio la kumuua mwosia au kumpiga na kumsababishia majeraha makubwa.

Tumeshuhudia mara kwa mara vitendo vya watoto ama kutishia uhai wa wazazi wao au kuchukua hatua kabisa na kuwadhuru au kuwaua kwa sababu mbalimbali ikiwepo mali na masuala ya kishirikina. Sheria na taratibu za kimila zinaeleza kuwa endapo mrithi atachukua hatua za kumdhuru mwosia basi mwosia anayo haki ya kumwondoa mrithi husika katika haki ya kumrithi kutokana na vitendo vyake.

  1. Endapo mrithi bila sababu ya msingi alishindwa kumuuguza mwosia au kumsaidia wakati wa njaa.

Yapo mazingira ambayo mwosia anaweza kuingia katika dhiki au ugonjwa na akahitaji msaada wa warithi wake. Endapo mrithi amekataa pasipo sababu za msingi kumhudumia mwosia wakati wa dhiki yake au ugonjwa wake basi mwosia anayo haki ya kimila kumwondoa muhusika kutoka katika wosia wake.

Utaratibu wa kumwondoa mrithi

  • Suala la kumwondoa mrithi katika haki ya kurithi kutoka kwa marehemu linatakiwa lifanywe na muhusika mwenyewe yaani mwosia. Mwosia akiwa na sababu kati ya hizo hapo anaweza kutoa wosia wake ikiwa kwa mdomo au maandishi juu ya sababu ya kumwondoa mrithi katika haki ya urithi.
  • Mrithi anayeondolewa haki ya kurithi anaweza kupewa nafasi ya kusikilizwa na familia au ukoo husika. Ikiwa mwosia bado yupo hai na tamko lake limetolewa la kumwondoa mrithi katika urithi, mrithi anaweza kuomba kusikilizwa na familia au kikao cha ukoo na kuwasilisha utetezi wake.
  • Endapo utetezi wake utakubalika na mwosia kuridhika au kupatanishwa basi tamko lile litabatilishwa, la endapo utetezi wake hautakubalika basi tamko la wosia ule litatekelezwa.

 

Hitimisho

Mfumo wa kuondoa warithi kwenye wosia ni mfumo wa tangu vizazi na umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali. Lengo hasa ni kuweka nidhamu na heshima kwa wale waliotutangulia katika maisha hasa wazazi wetu katika kipindi chote walichopo hapa duniani. Maisha ya sasa yamekuwa na upungufu mkubwa wa maadili si kwa watoto bali hata wazazi pia. Muhimu kuzingatia nafasi ya kila mmoja wetu katika jamii ili tuweze kuwatunza na kuwa na heshima stahiki kwa wale waliotutangulia ili na sisi tuweze kupata heshima hiyo kwa vizazi vyetu.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Karibu kwenye Darasa la Uliza Sheria 2018 jiunge sasa fuata link hii DARASA LA ULIZA SHERIA 2018

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili