Kazi za Msimamizi wa Mirathi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Msimamizi wa Mirathi

Msimamizi wa mirathi ni mtu anayeteuliwa na familia au ukoo kwa ajili ya kutelekeleza majukumu ya kuhakikisha mali ya marehemu inakusanywa na madeni yake yanalipwa kisha kugawanywa kwa warithi halali wa marehemu. Msimamizi wa mirathi anateuliwa na familia kisha anadhibitishwa na Mahakama ambapo shauri la mirathi linakuwa limefunguliwa.

Msimamizi wa mirathi anapatikana pale endapo marehemu hakuacha wosia. Endapo marehemu aliacha wosia na kumteua mtu atakayesimamia mirathi yake basi mtu huyo ataitwa Mtekeleza wosia.

Kazi za Msimamizi wa Mirathi

Msimamizi wa mirathi au mtekeleza wosia wana kazi ambazo kimsingi zinafanana yaani kuhakikisha mali ya marehemu inaenda kwa warithi wake halali. Yafuatayo ni majukumu muhimu ya msimamizi wa mirathi.

  1. Msimamizi wa mirathi kuwa mwakilishi wa kisheria wa marehemu

Mara baada ya msimamizi wa mirathi kuteuliwa na ukoo au familia na kudhibitishwa na mahakama anapata hadhi ya kuwa mwakilishi wa kisheria wa marehemu. Hapa masuala yote yanayohusiana na marehemu juu ya haki zake, mali zake na mambo yote yatasimamiwa na msimamizi wa mirathi kwa niaba ya marehemu.

  1. Msimamizi wa mirathi kulipa madeni na kugawa mali ya marehemu

Huu ndio wajibu mkubwa wa nafasi ya msimamizi wa mirathi yaani kukusanya mali za marehemu na iwapo kuna madeni kuhakikisha yamelipwa na kugawa kiasi kilichobaki kwa warithi halali wa marehemu.

  1. Msimamizi wa mirathi ana uwezo wa kushitaki na kushtakiwa kwa niaba ya marehemu.

Msimamizi wa mirathi ana haki ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote au taasisi yoyote ambayo marehemu alikuwa anadai haki zake. Hivyo anaweza kufungua shauri mahakamani kama msimamizi wa mirathi ya marehemu na kudai haki husika. Endapo yapo madai dhidi ya marehemu basi msimamizi wa mirathi anawajibika kusimama nafasi ya marehemu na kuwasilisha utetezi wake.

  1. Msimamizi wa mirathi ana uwezo wa kuuza au kuweka rehani mali ya marehemu kwa manufaa ya warithi

Kwa kuwa mali zote zinakuwa chini ya usimamizi wake basi kama itakavyofaa kuhusiana na maslahi mapana ya warithi msimamizi wa mirathi anaweza kuuza mali au kuweka rehani mali ya marehemu kwa manufaa ya warithi husika. Ni muhimu sana kuzingatia kwani wasimamizi wengine wamekuwa wakifanya hayo kwa manufaa yao.

  1. Kuwasilisha taarifa ya mgawanyo wa mali za marehemu Mahakamani

Baada ya kumaliza wajibu wake ndani ya miezi 6, msimamizi wa mirathi anapaswa kuwasilisha taarifa juu ya mali za marehemu kwa jinsi ile ambavyo zimegawanywa kwa warithi wake halali. Warithi wanayo haki ya kuchunguza taarifa hiyo endapo ipo sawa sawa na kile kilichofanyika katika mgao wa mirathi. Wasimamizi wengi baada ya kuteuliwa hawatimizi wajibu huu wa kupeleka taarifa za mirathi mbele ya mahakama hayo ni kinyume cha sheria na wanaweza kutiwa hatiani na kuadhibiwa.

Hitimisho

Kama tulivyoona leo juu ya nafasi ya usimamizi wa mirathi na majukumu yanayoambatana nayo. Kazi hii si nyepesi wala si kila mmoja anaiweza. Kama utateuliwa kuwa msimamizi wa mirathi basi ni lazima ujue wajibu huu na kuzingatia sheria ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza endapo utakiuka sheria juu ya usimamizi wa mirathi.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Karibu kwenye darasa la sheria 2018 kwa kufuata link hiiDARASA LA ULIZA SHERIA 2018

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili