Sheria Leo. Hofu ya Kuhusika kwenye Mkondo wa Sheria ni sababu ya watu Kujichukulia Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunakwenda kuangalia sababu mojawapo ya watu kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni Wanajamii kuwa na Hofu ya kuhusika kwenye mkondo wa sheria. Karibu tujifunze.

Mchakato wa Sheria

Katika makala zilizopita tumegusia juu ya mchakato wa kisheria jinsi ulivyo mrefu na unahusisha vyombo mbalimbali mpaka kukamilika. Kwa ufupi mchakato unaanza mara baada ya tukio kutokea na upelelezi kufanyika, kisha mashataka ambapo ushahidi hutolewa na hatimaye hukumu ya mahakama.

Watu wengi miongoni mwa jamii yetu ni wepesi sana kujichukulia sheria mkononi lakini ni watu wazito sana kukubali au kuwa tayari kuwa mashahidi inapokuja suala la mashitaka ili haki itendeke.

Kumekuwa na dhana ambayo imeenea juu ya mashahidi katika suala lolote la kisheria aidha kupata misukosuko au kusumbuliwa kwa namna yoyote ile ili wasiweze kutimiza wajibu wao. Hofu kubwa imejengeka kwa wanajamii kuogopa kutoa ushahidi wakihofu labda kesi inaweza kuwageukia wao na wakaingia hatiani kwa namna moja au nyingine. Jambo hili halina ukweli wowote. Sheria za ushahidi zinamlinda shahidi alimradi anachotolea ushahidi ni jambo la kweli.

Wengine wanaogopa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya upelelezi ili wasiweze kuitwa kutoa ushahidi katika matukio mbalimbali.

Ipo hofu nyingine kwa wanajamii endapo watajulikana kuwa ni mashahidi katika matukio ambayo yana maslahi fulani au matukio ya uhalifu mkubwa basi maisha yao yanaweza kuwa hatarini.

Haya yote ukiyatazama, yanatoa sababu kubwa ya wanajamii kuona ni heri kuchukua sheria mkononi kumaliza suala la uhalifu ikiwa ni mtuhumiwa wa wizi basi amalizwe pale pale na kutokana na mazingira hayo hakutakuwa na mtu ambaye atajulikana endapo alihusika katika mauaji hayo kwani mara nyingi ni vigumu vyombo vya usalama kufuatilia mara baada ya kifo cha mtuhumiwa.

Lakini ni vyema kufahamu kwamba sisi wenyewe tukiwa katika mazingira ya kuhukumiwa pasipo kusikilizwa tutaona kwamba tumeonewa, je kwa nini tusitoe nafasi kwa wale ambao tunawatuhumu. Kama tunao ujasiri wa kuwachukulia hatua kwa kuwahukumu kwa nini tukose ujasiri kwa kushuhudia mahakamani kuwa ni kweli walitenda makosa?

Kwa kutazama ukweli huu utaona hofu ya watu wengi kuhusiana na mchakato wa kisheria si kwa ajili ya kuwa walengwa wa kisasi cha watuhumiwa bali hatuna hakika na kile ambacho tunawatuhumu.

Hatua za kuchukua

  • Lazima jamii itambue kuwa suala la haki ni mchakato wa kisheria ambao tumeukubali kama taifa na hivyo tunapaswa kuheshimu
  • Tukubali kuwa kama sisi wenyewe tunapokabiliwa na tuhuma tungependa kupewa nafasi ya kujitetea basi hata wengine wapate nafasi hiyo.
  • Kila mmoja akiwa anatekeleza uamuzi wa kuchukua sheria mkononi ajiulize kuwa nina udhibitisho wa kutosha juu ya makosa ya mtu huyu ninayemuhukumu au ninafanya kwa sababu nimesikia kwa watu wengine?

Wanajamii tuepuke kuchukua sheria mkononi mwetu wakati tayari tunavyo vyombo vilivyoundwa kwa makusudi ya kushughulikia masuala ya kisheria kwa mchakato uliowekwa na kukubaliwa na sisi wote. Tujifunze kuwa na subira na kuona haki ikitendeka, ikiwa vyombo vyetu vina mapungufu kadhaa kama tulivyoona tulenge kuviboresha na si kuchukua wajibu wake kama njia mbadala ya kusuluhisha matatizo yetu ya kijamii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema na mwanzo mwema wa 2018.

Wako

Isaack Zake, Wakili