28. Usitishaji wa Ajira kwa Kutokuhitajika
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Leo tunaendelea aina nyingine wa Usitishaji wa Ajira kwa sababu ya Kutokuhitajika.
Maana ya Kutokuhitajika
Kama tulivyoanisha mazingira ya usitishaji wa ajira ya mfanyakazi, mwajiri anaweza kusitisha ajira husika endapo mfanyakazi haitajiki katika ajira. Hii
Kutokuhitajika kunaweza kuonekana kwa namna zifuatazo
- Mfanyakazi kutofaa katika kazi kwa sababu ya tabia au hulka yake.
- Mfanyakazi kuwa na uhusiano mbaya na wafanyakazi wenzake, wateja, wabia, wasambazaji au watu wengine muhimu kwa ofisi.
Katika kushughulikia suala la kutokuhitajika kwa mfanyakazi, mwajiri anapaswa kuzingatia taratibu kama zile ambazo anazingatia endapo anakusudia kumwachisha mfanyakazi kwa uzembe kutokana na utendaji usioridhisha.
Utaratibu wa kusitisha ajira kwa kutokuhitajika
Ufuatao ni utaratibu unaopaswa kuzingatiwa endapo mwajiri anataka kusitisha ajira ya mfanyakazi kwa sababu ya kutohitajika;
- Mwajiri ni lazima afanye uchunguzi kujua sababu inayosababisha tabia ya mfanyakazi
Hii ni hatua muhimu na ya kwanza ambayo mwajiri anatakiwa kuichukua. Mwajiri hapaswi kukurupuka na kuchukua uamuzi tu wa kusitisha ajira kwa sababu ya kutokuhitajika pasipo kufanya uchunguzi. Uchunguzi utasaidia pande zote kujua kiini cha tabia husika. Uchunguzi unaweza kuonesha namna mfanyakazi anavyohusiana na wafanyakazi wengine au wateja.
- Mwajiri kutoa nafasi ya mfanyakazi kuboresha utendaji
Kabla mwajiri hajachukua hatua za kusitisha ajira ya mfanyakazi kwa sababu ya kutokuhitajika ni vyema kumpa mfanyakazi nafasi ya kuboresha tabia yake na namna anavyohusiana na wateja au wafanyakazi wenzake.
- Mwajiri anapaswa kutoa muda wa kutosha ili kuimarisha tabia na mwenendo wake
Hii ni hatua muhimu sana kabla ya kuchukua hatua za kusitisha ajira ya mfanyakazi. Mwajiri anapaswa kutoa kipindi fulani cha kumwezesha mfanyakazi kuboresha tabia yake na mahusiano yake kazini endapo itaonekana ana upungufu. Si sahihi mara baada ya kubaini tabia isiyoridhisha basi mwajiri anatakiwa kutoa muda kiasi wa mfanyakazi kuboresha utendaji.
- Mwajiri anaweza kutoa onyo ikiwa tabia ya mfanyakazi haijaimarika
Endapo itaonekana baada ya kutoa nafasi ya kujirekebisha na kuboresha tabia na mwenendo lakini bado utendaji wa mfanyakazi haujaimarika, mwajiri anaweza kutoa onyo kwa mfanyakazi husika, kwamba tabia isipoimarika anaweza kusitishiwa ajira. Aidha kabla ya kuitisha kikao cha kujadili juu ya usitishaji wa ajira mwajiri ni lazima awe;
- Na kumbukumbu za matukio aliyoyafanya mfanyakazi husika na kusababisha matatizo au kuvurugika kazi
- Amemuonya mfanyakazi au amependekeza hatua za kurekebisha hali hiyo.
- Mwajiri anapaswa kuitisha kikao cha kusikiliza usitishaji wa ajira kwa kutokuhitajika
Endapo mwajiri ataona kuna haja ya kusitisha ajira kutokana na kutokuhitajika basi anawajibika kuitisha kikao na mfanyakazi. Katika kikao hiki mfanyakazi anaweza kuwakilishwa na mwakilishi.
- Mfanyakazi kupata nafasi ya utetezi katika kikao
Mara baada ya mwajiri kuwasilisha tuhumu dhidi ya mfanyakazi basi mfanyakazi atapewa nafasi ya kujibu tuhuma, au kuondoa chanzo cha tatizo au kupendekeza njia mbadala za usitishaji wa ajira.
- Maamuzi ya mwajiri ya kusitisha ajira yanapaswa kuwasilishwa kwa maandishi
Mwajiri anapaswa kumwandikia mfanyakazi usitishaji wa ajira kutokana na kutokuhitajika kwa kuonesha sababu katika barua ya usitishaji wa ajira.
Hitimisho
Usitishaji wa ajira kutokana na kutokuhitajika ni mojawapo ya sababu inayoweza kumwondoa kazini mfanyakazi. Wafanyakazi wanatakiwa kuwa waangalifu kuchunga mwenendo wao kitabia kuhusiana na wateja au wafanyakazi wenzao mahali pa kazi.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili.