Sheria Leo. Kutokuwa na Imani kwa Mahakama ni sababu ya watu Kujichukulia Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunakwenda kuangalia sababu mojawapo ya watu kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni Kutokuwa na imani na Mahakama. Karibu tujifunze.

Imani kwa Mahakama

Kama tulivyoeleza katika makali iliyopita imani katika mfumo wa kutenda haki ni sehemu kubwa sana ya kufanya mfumo husika kufanya kazi. Tumeona pia changamoto au mojawapo ya sababu za watu kuchukua sheria mkononi mwao ni kutokuwa na imani katika mfumo wa upelelezi. Tuliangalia kwa kina na sababu hasa zinazochangia ufanisi katika upelelezi kutokuwa wa kuridhisha.

Sababu nyingine ambayo tunaitazama leo ni hali ya watu kutokuwa na imani na mfumo wa kimahakama katika utatuzi wa mashauri au kesi zinazowasilishwa. Hakuna tofauti kubwa kati ya changamoto zinazoikumba mahakama na mfumo wa upelelezi.

Mahakama ndio chombo pekee ambacho kimeundwa kikatiba kwa lengo la kuamua mashauri na kutoa haki kwa pande zinazofikishwa mbele yake. Tulieleza pia katika makala iliyopita juu ya mchakato wa kisheria unavyochukua muda mrefu eneo moja wapo muda mwingi unachukuliwa ni mahakamani.

Zipo sababu kadhaa zinazofanya mahakama ikumbane na hali ya kutoweza kutimiza majukumu yake kama wananchi wanavyotarajia. Mfano wa sababu hizo;

  • Uhaba wa watendaji wa kutosha katika mahakama kulinganisha na idadi ya kesi zinazowasilishwa kila siku.
  • Majengo machache ya mahakama kulinganisha na ongezeko la watu katika maeneo mbalimbali
  • Uhaba wa vitendea kazi vya kutosha katika kutimiza majukumu ya kimahakama
  • Changamoto ya matumizi ya tehama katika kutimiza majukumu kwa kasi inayotakiwa.
  • Mchakato mrefu wa kufuata taratibu za kisheria kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote kwa kadri inavyowezekana.
  • Udhaifu wa ushahidi unaowasilishwa una upande wa mashitaka na kupelekea watuhumiwa kuachiwa huru mara kwa mara.
  • Uwepo wa vitendo vya rushwa kwa watumishi wa mahakama wasio waadilifu na waaminifu.

Kutokana na changamoto hizi zinazoikabili mahakama ambazo nyingine zipo nje ya uwezo wake na nyingine zinasababishwa na watendaji ni dhahiri wananchi wanakosa imani na mfumo mzima wa uendeshaji wa mahakama na kupelekea vitendo vya uvunjifu wa amani na kujichukulia sheria mkononi katika kufanya hukumu za kijamii ikiwepo na mauaji mbalimbali.

Hatua za kuchukua

  • Mfumo wa mahakama ni vyema ukatazamwa upya hasa katika suala zima la fedha za kuendesha shughuli za mahakama. Fedha zitasaidia kuongeza idadi ya watendaji, idadi ya mahakama na vitendea kazi vingine kurahisisha na kuwezesha mashauri kukamilika kwa haraka.
  • Uundaji wa mahakama maalum katika kushughulikia masuala maalum kunaweza kusaidia kwa kiwango kupunguza mzigo wa mashauri eneo moja hasa pale mahakama za kijinai zinapohusika tena na masuala ya madai.
  • Kuwepo na mfumo mbadala wa utatuzi wa migogoro hasa unaoongozwa na jamii katika eneo husika. Kwa mtazamo wangu mingi ya migogoro haikupaswa kuwa mahakamani bali kutokana na mtazamo mbovu au ushauri mbaya watu wanajikuta wapo mahakamani wanapoteza muda wao kwa kulumbana kwa vitu ambavyo wangeweza kukubaliana.

Suala la mahakama ni aina ya mfumo ambao jamii zote ulimwenguni zilizostaarabika zinatumia ili kukata mashauri. Kama tumeamua kuwa na mahakama ambapo haki zetu na wajibu wetu vinakwenda kuamuliwa kwa mujibu wa sheria basi tunao wajibu wa kufuata mchakato unaotakiwa. Tusiendelee na tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kupitisha adhabu kwa watu pasipo wao kupata nafasi ya kujitetea. Tukumbuke tu hata katika vitabu vya dini kwa kosa lake Adam na Hawa bado Mungu aliwapa nafasi ya kujitetea kabla ya adhabu kutolewa. Pata picha wewe umejikuta katika hali ya jamii ambayo wanakutuhumu kwa jambo Fulani ambalo kimsingi si kweli, nadhani ungependa kupewa nafasi ya kujitetea. Ndivyo ilivyo kwa kila mwanadamu anayo hiyo asili ya kutaka kujitetea hata kama ana makosa.

Tuheshimu mahakama kama tumeamua kuwa nazo basi tuzipe nafasi na kutoa mawazo mazuri ya kuboresha utendaji wake na kupinga vitendo vyote vinavyofanywa na watumishi wasio waaminifu.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili